Na Elizabeth John
SHIRIKISHO la Filamu Tanzania (TAFF), limetoa
shukrani kwa Watanzania kwa ushiriki wao katika hatua zote za maradhi, msiba na
mazishi ya aliyekuwa msanii mwenzao, Said Juma Kilowoko ‘Sajuki’.
Sajuki alianza kusumbuliwa na tumbo Septemba
2011 ambapo TAFF kwa kushirikiana na wadau wa filamu nchini, pamoja na viongozi
mbalimbali wa serikali walimsaidia kumpeleka India kwaajili ya matibabu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais wa
TAFF, Simon Mwakifwamba alisema baada ya kutoka India alipata nafuu na Desemba
mwaka jana akauugua ghafla ugonjwa wa kansa ya ngozi hadi alipofikwa na umauti Januari
2 mwaka huu.
“Kifo cha Sajuki kiliwavuta Watanzania wengi
hasa kutokana na historia ya maradhi kwa muda mrefu, TAFF tunawashukuru wote
ambao waliweza kushiriki kwa hali na mali kipindi chote cha maradhi mpaka
umauti, hatuwezi kumkumbiuka kila mmoja kwa nafasi yake,” alisema Mwakifwamba.
Mwakifwamba alisema arobaini ya Sajuki
itafanyika Februali 8 mwaka huu nyumbani kwake Tabata jijini Dar es Salaam.
Aidha, TAFF wamewataka Watanzania kuendelea
kushirikiana na wasanii katika nyanja tofauti, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari
kuendelea kutoa habari zinazohusu tasnia ya filamu ambazo zitaonya, kuelimisha
na kukumbusha wajibu wa wasanii katika jamii kwa maendeleo ya taifa letu.
Katika hatua nyingine, Mwakifwamba alikanusha
taarifa ya kifo cha msanii wa kundi la Komedi Joseph Shamba ‘Vengu’ zilizosambaa
kwa watu mbalimbali pamoja na baadhi ya vyombo vya habari.
“Mwenyewe taarifa hizo nimezipata, lakini sio
kweli, tumuombee apone haraka kwani hali yake bado mbaya anasumbuliwa na
mtikisiko wa ubongo, kuna muda anapoteza fahamu,” alisema Mwakifwamba.
No comments:
Post a Comment