DAR ES SALAAM, Tanzania
WAZIRI wa Fedha, William Mgimwa, amesaini mkataba wa sh. Bilioni
28.2 zilizotolewa na Serikali ya Japan kwa ajili ya miradi mitatu ya kiuchumi na
kijamii.
Serikali ya Japan itafadhili miradi hiyo kupitia Shirika lake la
ushirikiano wa Kimataifa (JICA).
Akizungumza jana jijini Dar Es Salaam, Mgimwa alitaja miradi
hiyo kuwa ni upanuzi wa barabara ya Kilwa ili watu kuweza kufika kwa wepesi
katikati ya mji na eneo la bandari.
Mgimwa alisema kuwa mradi huo utakuwa wa kilometa 1.3 na
utaanzia eneo la Gerezani linalokutana na Kamata mpaka barabara ya Kilwa ujenzi
utakaosababisha barabara hizo kuwa nne tofauti na sasa ambapo zipo mbili na
mradi huo utagharimu sh. Bilioni 20.
Pia alisema kuwa mradi wa pili ni kubuni na kujenga barabara za
juu (flyover) ilikuondoa foleni katika barabara ya Mandela na Nyerere ikiwemo
kujenga daraja eneo la Tazara mradi ambao utagharimu sh. Bilioni 1.26.
Alisema kuwa mradi wa tatu utahakikisha tatizo la ukosefu wa
chakula linakwisha hasa katika mikoa yenye uhaba.
“Mradi wa tatu utahakikisha usalama wa chakula na mradi huu
unalengo la kutimiza sera ya kilimo kwanza na kutoa nafasi ya kuzalisha kwa
wingi na kujenga usalama wa chakula kwa watu wenye hali ya chini mradi ambao
utagharimu sh. Bilioni 6.92” alisema Mgimwa.
Naye Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaki Okada, alisema kuwa
nchi ya Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania na kuitaka Serikali
kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika kwa mradi husika ili kuhakikisha nchi
inapata maendeleo.
No comments:
Post a Comment