Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BENKI ya CRDB imeingia makubaliano na waandaaji wa shindano la Bongo Star Search (BSS) kwa lengo la kukuza vipaji vya wasanii nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa benki hiyo, Stephen Adili, amesema CRDB imeingia mkataba wa miaka mitatu kuanzia msimu wa mwaka 16, hadi msimu wa 18 kwa ajili ya kusaidia vijana kuibua na kukuza vipaji vyao.
Amesema benki hiyo imejidhatiti kifedha kuhakikisha vipaji vinaibuliwa na kugeuzwa kuwa ajira kwa vijana wengi zaidi nchini.
Aidha, Adili amesema pamoja na zawadi zinazotolewa na waandaaji wa shindano hilo, benki ya CRDB itatoa si chini ya shilingi milioni 30 kwa mshindi wa mwaka huu bila kuathiri utaratibu wa BSS.
Ameongeza kuwa kwa washindi wa misimu ya 17 na 18, benki hiyo pia itatoa fedha taslimu kama sehemu ya kuunga mkono maendeleo ya vipaji vya washiriki wa shindano hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bongo Star Search, Rita Paulsen, amesema tayari vipindi karibu 10 vimesharushwa na sasa maandalizi ya kuelekea fainali yanaendelea.
Amesema fainali ya shindano hilo inatarajiwa kufanyika Juni 26 au 27 mwaka huu, huku akiwataka wadau wa burudani kujiandaa kwa mambo makubwa zaidi kutokana na udhamini wa CRDB ambao utaendelea hadi msimu wa 18 wa shindano hilo.





No comments:
Post a Comment