NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Rose Tweve, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, akisema hatua hiyo imeongeza fursa za kiuchumi kwa makundi mbalimbali ya wananchi.
Akizungumza katika mkutano wa Waziri Mkuu uliofanyika Kata ya Kihorogota, Jimbo la Ismani, Rose alisema Serikali ilifanya uamuzi sahihi wa kuboresha utaratibu wa utoaji wa mikopo hiyo na kuwezesha fedha kuwafikia walengwa kwa ufanisi zaidi.
Alieleza kuwa katika Halmashauri inayohudumia Majimbo ya Ismani na Kalenga, zaidi ya shilingi bilioni moja zimetolewa kwa vikundi zaidi ya 188 kuanzia Julai mwaka wa fedha 2024/2025 hadi Mei mwaka huu.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, vikundi 88 vya wanawake vimepata zaidi ya shilingi milioni 470, huku vikundi 67 vya vijana vikipokea zaidi ya shilingi milioni 470. Aidha, vikundi 33 vya watu wenye ulemavu vimenufaika na zaidi ya shilingi milioni 60 zilizotolewa kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.
Hata hivyo, Rose aliiomba Serikali kuendelea kuboresha mfuko huo kwa kuweka utaratibu utakaowezesha wananchi mmoja mmoja wenye mawazo na miradi mizuri ya biashara kupata mikopo moja kwa moja, badala ya kutegemea mfumo wa vikundi pekee.
Alisema pamoja na kuwepo kwa mifuko mbalimbali ya uwezeshaji nchini, wananchi wengi bado wanaifahamu zaidi mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuiboresha ili iwafikie Watanzania wengi zaidi.
Katika mkutano huo, Mbunge wa Viti Maalum wanawake, Fatma Rembo, alimshukuru Waziri Mkuu kwa kuendelea kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Fatma alisema wanawake wa Mkoa wa Iringa wanathamini juhudi zinazofanywa na Serikali kupitia Waziri Mkuu ambaye amekuwa akifika moja kwa moja kwa wananchi, kusikiliza kero zao na kufuatilia utatuzi wake.
"Kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Iringa tunakushukuru sana kwa kazi kubwa unayoifanya ya kuwasikiliza wananchi na kuhakikisha changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi," alisema.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Rita Kabati, alisema Mkoa wa Iringa unaendelea kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa viongozi wake, hali inayochochea maendeleo na ustawi wa wananchi.
Wabunge hao walitoa kauli hizo wakati wa mkutano wa Waziri Mkuu uliofanyika katika Kata ya Kihorogota, Jimbo la Isimani, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani Iringa.





No comments:
Post a Comment