Na Clezencia
Tryphone
MUANDAAJI wa Mbio za Mkesha wa mwaka mpya zijulikanazo kwa
jina la ‘MeTL New Year Eve Midnight Marathon 2013’ Sarah Ramadhani ameishukuru
Kampuni ya Mohamed Enterprises kwa udhamini ambao pia umeiwezesha klabu yake ya
Nyro Athletics kupata eneo la heka tano Kibaha mkoani Pwani kwa ajili ya kujenga
uwanja wa kisasa wa riadha.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Sarah ambaye
mwanariadha wa zamani, alimpongeza mdhamini huyo kwa kuona umuhimu na kutoa
udhamini wa mbio hizo, ambao licha ya kufanikisha tukio hilo, wamefanikiwa pia
kununua eneo hilo Kibaha mkoani Pwani, kwa ajili kujenga uwanja huo maalumu kwa
ajili ya michezo ya riadha tu.
Sarah alisema, mara baada ya kupata eneo hilo, tayari
wameanza majukumu ya kuandaa michoro kwa ajili ya uwanja huo utakaokuwa
ukitumika kwa ajili ya michezo mbalimbali ya riadha ikiwamo miruko, mitupo na
mbio za uwanjani.
“Namshukuru sana Mohamed Enterprises kwa kuona umuhimu wa
mchezo wa riadha hapa nchini na kupitia ufadhili wake wa mbio za mwaka mpya,
sisi kama klabu tukaona tutumie sehemu yake kununua eneo Kibaha ajili ya uwanja
wa maalumu wa riadha, ambao utatumika kwa mazoezi na mashindano na imani hii ni
changamoto kwangu mimi kuhakikisha riadha inapiga hatua zaidi kama mdau wa
mchezo huo,” alisema Sarah ambaye ni mwanariadha wa zamani wa Taifa katika
mitupo.
Aidha Sarah, aliwataka makocha wa mchezo huo kuwa wabunifu
na kutafuta vipaji vijijini na sio kila siku wanariadha kuwa walewale katika
michuano yake hiyo yenye kauli mbiu ‘Run for Peace and Health’ na kudai kuwa
mwaka huu anahiyaji kuona mabadiliko kutoka kwa makocha hao.
“Mimi nataka wanariasha ambao watavunja rekodi na sio kila
siku wanakuja tu kukimbia ili wapate fedha na kuondoka kama itakuwa hivi
hatutapiga hatua bali tutakalia hivihivi hivyo basi nawaomba mjirekebishe,”
alisema.
Naye Rais wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka,
amemtaka Sarah kuendeleza asili yake ya uanariadha, kwani katika michezo hapa
nchini majungu ni mengi ususani mtu ukiwa inaelekea katika mafanikio na
kumsihii kuwa mvumilivu ili kufikia malengo yake.
“Kwenye michezo majungu ni mengi, na mtu usipokuwa mvumilivu
unakata tamaa, na mfano hai ni majungu katika chama changu ila namshukutu mungu
toka mwaka jana nimeingia madarakani hakuna majungu wala migogoro ni kitendo
cha kumshukuru mwenyezi Mungu,” alisema Mtaka ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya
Mvomero mkoani Morogoro.
Kwa upande wa mwakilishi wa Mohamed Enterprises, Cosmas
Mtesigwa alimtaka Sarah kutokuwa muoga katika malengo yake huku akimuomba
endapo atakuwa na shida asisite kuwafikia kwa kuwa wao wameamua kujitosa katika
mchezo huo ambao una jina kubwa hapa duniani.
Kwa upande wa wasichana, Sara Ramadhani wa Zanzibar
alishinda akitumia dakika 33:82:31, wa pili Mary Naali wa African Ambassador
Athletics Club (AAAC), ya Arusha akikamata namba mbili kwa dakika 34:10:90, wa
tatu Failuna Abdi wa....dakika 36:02:58 wa nne Banuelia Brighton wa Holili
Running Club ya Kilimanjaro dakika 38:21.12 na watano Asmah Rajab aliyetumia
dakika 45:31.19.
Kwa wanaume Dickson Marwa wa Holili Running Club aliibuka
kidedea akitumia dakika 29:14:45, akifuatiwa na Patrick Nyangero pia wa Holili
dakika 29:16:88, Mohamed Msenduki wa Arusha dakika 29:22:80, Faustine Mussa wa
JWTZ Arusha 29:27.05 huku tano bora ikifungwa na Ramadhan Mnyandeo dakika
29:27.74
Kwa walemavu mshindi aliibuka Shukuru Khalfan dakika
38:51:10, Wilbert Costantino dakika 39:29:02, Mathias Jollo dakika 43:16:07,
Christian Amour 43:27.58 na watano John Stephano dakika 52:31.34.
No comments:
Post a Comment