EMMANUEL ADEBAYOR NAYE AUPONDA UWANJA WA MBOMBELA
NELSPRUIT, Afrika Kusini
EMMANUEL Adebayor amelalamika kwa Shirikisho la Soka barani
Afrika (Caf) na Kamati ya Maandalizi ya michuano ya Mataifa Afrika juu ya hali
mbaya katika sehemu ya kuchezea ‘pitch’ ya Uwanja wa Mbombela ulioko jijini
hapa.
Nyota huyo wa timu ya taifa ya Togo
anayekipiga Tottenham Hotspur, aliulalamikia uwanja huo waliocheza na kuambulia
sare ya bao 1-1 dhidi ya Tunisia
na kufanikiwa kutinga robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi
hiyo.
Katika mechi yao ya robo
fainali hapo Jumapili, Togo inatarajia kushuka dimbani kuwavaa Burkina Faso katika
mtannange wa kukata na shoka unaosubiriwa kwa hamu.
Nahodha wa Zambia,
Chris Katongo pia mapema wiki hii aliutaja uwanja huo kuwa mbovu uliochangia
kuwanyima nafasi ya kushinda mechi zao, kutokana na sehemu ya kuchezea kukosa
ubora.
"Kwa mara nyingine tena sisi tuko Afrika – Afcon ni
michuano mikubwa kwa bara la Afrika na ulimwengu mzima unafuatilia nini
kinafanyika kupitia michuano hii. Huwezi kucheza soka safi
katika ‘pitch’ kama hii," alilalamika Adebayor.
NAHODHA NIGERIA
JOSEPH YOBO AWAONYA TEMBO WA IVORY COAST
JO’BURG, Afrika Kusini
NAHODHA wa timu ya taifa ya Nigeria,
Joseph Yobo ameitaja robo fainali ya Mataifa Afrika kati yao
na Tembo wa Ivory Coast
ni moja ya mechi kali na kubwa kuwahi kutokea katika historia ya michuano hiyo.
"Hakutakuwa na mechi kubwa barani Afrika kama hiyo na, bila shaka, tutakuwa kikosi kisichopewa
nafasi yoyote, dhidi ya timu ya daraja la juu mno Afrika. Lakini mchezo
utaamuliwa ndani ya uwanja," alisema Yobo, ambaye hii ni michuano yake ya
sita.
"Kila mmoja anatutarajia sisi
kwamba tutapoteza mechi hii, lakini sisi kama wachezaji hilo
liko akilini mwetu na tutahakikisha tunaingia dimbani Jumapili kuzuia hilo dhidi ya Ivory Coast,"
aliunga mkono winga wa Chelsea Victor Moses, ambaye alifunga mara mbili dhidi
ya Ethiopia
na kufuzu hatua hii.
"Wana wachezaji wazuri na bora
kama Didier Drogba, mmoja wa washambuliaji
hatari zaidi Afrika. Lakini sisi kama timu
tutakuwa makini na kiwango chetu wenyewe mchezoni," alimaliza Moses.
WAZIRI WA MICHEZO WA AFRIKA KUSINI FIKILE MBALULA ATAMBIA MAFANIKIO
JO’BURG, Afrika Kusini
WAZIRI wa Michezo wa Afrika Kusini, Fikile Mbalula Alhamisi
amezungumza na vyombo vya habari na kusema nchi yake imefanikiwa kuandaa kwa
mafanikio makubwa michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2013).
"Hadi hatua hii ya Afcon 2013... tunaweza kutangaza
kwamba imefanikiwa kwa kiasi kikubwa," alisema Mbalula jijini hapa, huku
hatua ya makundi ikitimishwa na robo fainali ikitarajia kuanza kupigwa
Jumamosi.
"Tangu kuanza kwa michuano hii hadi sasa, kumekuwa na
ongezeko kubwa la mahudhurio viwanjani. Afrika Kusini daima wanabaki kuwa
wenyeji bora na wazuri. Hakuna ishara hasi kutoka kwa mashabiki wa hapa."
No comments:
Post a Comment