HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 09, 2013

Marwa, Sakilu wang’ara Ngorongoro Marathon

Baadhi ya wanariadha wakichuana katika mbio za Tigo Ngorongoro Half Marathon zilizofanyika mjini Karatu Arusha juzi. Mbio hizo ziliandaliwa na Zara Tanzania Charity zikihimiza kupiga vitaugonjwa wa  Malaria.
Mkimbiaji mkongwe zaidi, Joram Molel mwenye miaka zaidi ya 70 akivishwa medali baada ya kufanikiwa kumaliza mbio hizo.

KARATU, Arusha
WANARIADHA Dickson Marwa na Jackline Sakilu jana waliibuka washindi katika mbio za Ngorongoro Half Marathon zilizofanyika mjini hapa.
Mbio hizo ambazo zilikuwa maalumu kwa ajili kuhamasisha vita dhidi ya ugonjwa wa malaria, zikiwa na kauli mbiu; ‘Run Against Malaria’ zilianzia lango la kuingilia Hifadhi ya Ngorongoro na kumalizikia viwanja vya Mazingira Bora mjini hapa, Marwa alishinda kwa upande wa wanaume akitumia saa 1:04.49 huku Sakilu akitesa upande wa wanawake kwa saa 1:16.26.
Marwa kutoka klabu ya Holili Kilimanjaro, alifuatiwa na Stephane Huche wa ASTC ya Arusha aliyetumia saa 1:04.56 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Alphonce Felix wa Winning Spirit pia ya Arusha saa 1:05.56.
Kwa upande wa wanawake, Sakilu kutoka JWTZ Arusha, alifuatiwa na Zakia Mrisho wa Team 100 saa 1:17.47 huku akifuatiwa na Mary Naali wa AAAC saa 1:18.17.
Mbio hizo maalumu kwa ajili ya kupiga vita ugonjwa wa malaria, ziliandaliwa na Zara Adventure ambao pia ni wadhamini wakishirikiana na Tigo, zilikuwa na ushindani mkali hasa kutokana na kushirikisha wanariadha wengi maarufu kama Faustine Mussa, Peter Sulle, Damian Chopa, Andrew Sambu, Catherine Range, Banuelia Brighton na wengineo.
Pia katika mbio hizo, mkimbiaji mkongwe zaidi, Joram Molel mwenye miaka zaidi ya 70 alikuwa kivutio baada ya kufanikiwa kumaliza mbio hizo na kugeuka gumzo miongoni mwa mashabiki na viongozi mbalimbali waliokuwepo.
Kutoka na tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Highview Hotel na Mkurugenzi wa mbio hizo, Leila Ansell, alimzawadia sh 500,000 Mzee Molel, huku Waziri Nyalandu naye akiongeza sh 500,000 Rais wa RT, Sh 100,000, RT sh 50,000 huku Tigo ikimpa simu yenye thamani y ash 175,000 na muda wa maongezi wa sh 50,000.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mgeni rasmi katika mbio hizo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, mbali na kuwapongeza waandaaji na wadhamini, Zara Adventure na Tigo, aliwashukia watendaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kushindwa kuonekana katika mbio hizo.
Nyalandu, aliwapongeza waandaaji na wafadhili hao kuishirikisha Ngorongoro katika vita hivyo ya Malaria, ambao ni ugonjwa hatari kwa maisha ya binadamu hususan, lakini uongozi wa mamlaka huo haukuonesha mwitikio chanya.
“Hili jambo muhimu katika vita dhidi ya malaria, kwani tunaendelea kuunga mkono vita iliyoanzishwa na Rais Jakaya Kikwete, ikiwa na kauli mbiu ya ‘Zinduka Malaria Haikubaliki’ lakini inasikitisha watu tuliowakabidhi madaraka wanatuchelewesha,” alisema na kuongeza;
Namuagiza uongozi wa Ngorongoro Jumatatu nipate ripoti ofisini kwangu, kwanini hawakuonekana hata mtu mmoja hapa. Mimi na Waziri wangu Balozi Kagasheki, hatusiti wala kumuonea haya mtu yeyote aliyekabidhiwa madaraka na kutekeleza sera na ilani ya serikali ya  CCM, kwani 2015 tutaulizwa tumewashirikishaje wananchi.
Naye Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka, aliwapongeza waliofanikisha tukio hilo, na kuwataka wazidi kuwekeza kwenye mchezo wa riadha na kushirikiana na RT ili kufuta aibu ya Tanzania kuwa wasindikizaji katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment

Pages