Na Mwandishi Wetu
WADAU wa elimu nchini waliopitia katika shule kongwe ya Sekondari ya Ndanda, wilayani Masasi, mkoani Mtwara wameombwa kuisaidia kwa hali na mali shule hiyo ambayo kwa sasa baadhi ya miundombinu yake iko katika hali mbaya.
Hayo yameelezwa hivi karibuni na Morega Mongate, Mkuu wa Shule hiyo iliyoanzishwa Julai mwaka 1928, ikimaanisha kuwa mwaka huu inatimiza umri wa miaka 85. Na katika kipindi hicho, imebahatika kutoa wasomi mahiri na watu mashuhuri, akiwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu,
Benjamin Mkapa.
Mongate alisema kuwa, miongoni mwa matatizo sugu katika shule hiyo ni pamoja na kukosekana kwa maabara ya uhakika, uchakavu wa mabweni, jiko na hata maktaba ambayo ina uhaba mkubwa wa vitabu, hasa vya sayansi.
Ingawa ilianza ikiwa na wanafunzi chini ya 200, lakini sasa wakifikia zaidi ya 1,000 lakini kwa miundombinu ile ile, Mongate ameomba ushirikiano wa karibu kutoka kwa watu waliosoma, waliowahi kufanya kazi au kuguswa na matatizo ya elimu nchini kuweza kuinusuru shule yake.
“Ni matatizo yanayohitaji utatuzi ili kuyafanya mazingira ya kusomea na hata kulala kuwa rafiki zaidi, lengo likiwa kuinua uwezo wa kitaalumu kishule kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Ndanda ina historia ya kipekee, imetoa watu mashuhuri na wasomi mahiri, lakini kwa sababu dhamira yetu ni kuendelea kubakiza jina zuri la Ndanda katika sekta ya elimu, tumeona ni vyema kero zilizopo
zikapatiwa ufumbuzi,” alisema Mongate.
Alisema kwa ujumla, kiasi cha sh milioni 135 kinahitajika ili kuipa shule hadhi inayostahili, ikiwa pamoja na kufanya ukarabati mkubwa wa mabweni likiwamo la kihistoria alilotumia Rais Mstaafu Mkapa, jiko na ununuzi wa vifaa vya maabara na pia kuipa uhai maktaba.
“Kwa watakaoguswa wanaweza kuwasiliana nami kwa simu 0766 469 670. Misaada mingine inaweza kutufikia shuleni au kupitia akaunti ya Mfuko wa Maendeleo wa Shule ya Sekondari Ndanda yenye namba 7050 1200 175 ya benki ya NMB, tawi la Masasi,” alisema.
Mbali ya Mkapa, wengine waliosoma shule hiyo ni pamoja na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia.
No comments:
Post a Comment