HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 02, 2013

KIZAZI HIKI KINARITHISHWA TAIFA LA AINA GANI?

Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi

Na Bryceson Mathias

BAADA ya matusi ya nguoni yaliyorindima bungeni hivi karibuni, nimesikitishwa kuona kwamba hakuna kiongozi wa kutegemewa aliyeumizwa na uchafu ule kiasi cha kuamua kuukemea.

Si Mwanasheria Mkuu, Spika wa Bunge, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais au Rais, wote kimya kana kwamba hawakusikia kilichotolkea huko, au kana kwamba hawaelewi lugha walizotumia watukanaji na waropokaji hao waliovikwa majoho ya Uheshimiwa na kuutumia vibaya..

Waliotoa matusi yale na mengine yaliyofuata, wameachwa watambe kana kwamba wameleta Kombe la Ushindi, na wengine wanaoitwa hawaambiliki, wameendeleza na utoto huo bila kuguswa wala kukemewa.

Nimeendelea kujiuliza sipati jibu. Hivi hawa wanasiasa wasiopevuka ufahamu wakapata Busara na Hekima, wanakirithisha Kizazi Kipya cha Watanzania, Taifa la aina gani? Kama baadhi ya wabunge wanaotegemewa na Taifa leo wako hivyo; Je, kizazi cha kesho kitakuwaje?

Kutokana na matusi ya baadhi ya wanasiasa uchwara ambayo hawalipii kodi, ndiyo maana wengi wao Misikiti au Makanisa ikiadibu watu kumcha Mungu na kuongezeka, wanalalamika sana!

Lakini Baa na Vilabu vya Pombe vinavyowafundisha matusi vikiongezeka, hawasemi! Wako Kimya!

Sasa huwa natafakari kama falsafa ya Mungu haitakiwi humo mjengoni, mbona wengine humo humo mnaomba wananchi wawaombeee? Kama falsafa ya Mungu si nzuri kuitumia bungeni, kwa nini Spika akianza Bunge anaanza kwa Sala ya kuliombea Bunge!

Anaomba kwa nani?

Sio kwa Mungu Muumba wa Mbingu na Ardhi? Mungu huyu anayeomba kuliongoza Bunge na kuwawezesha Wabunge busara na uvumilivu wanapojadili maslahi ya jamii na Taifa, anakubali upuuzi wa matusi na vijembe?

Wabunge wasifanye mchezo wa matusi yanayoinajisi nchi yetu, kama amekosekana Kiongozi wa kuwakemea kwa tabia mbaya ya matusi bungeni kiasi cha kukifanya kizazi kinachopevuka kilaaniwe! Sasa wananchi tutawakemea kwa maneno makali, na kuuweka ubunge wenu rehani.

Wabunge chonde Msilewe Upepo wa Amani iliyopo mkadhani ni rahisi! Wapo watu wanalia kwa maombi usiku kucha hawalali, wapo waombolezaji ambao wanajitesa Hawali wala hawanywi, ili Taifa hili lisiingie hatarini, likaangamizwa na nguvu za shetani kama mataifa mengine yalivyo.

Ni Rai yangu wabunge wasidhani kuwa na majeshi makini ya Ulinzi na Usalama nchini ndiko kunakosababisha kuwe na Amani! Unaweza ukawa na hivyo vyote lakini bado nchi ya ikawa haina Amani na kuwa watu wenye matusi bungeni hadi nyumbani kama baadhi yenu mlivyo.

Ni vema wakaelewa wako watu nchini ambao wameota sugu na magaga kwenye magoti, wengine wameota sugu na sijida kwenye paji za nyuso zao kiukweli, wakimlilia Mungu aliepushe Taifa hili na uvunjifu wa Amani, ambao miongoni mwenu humo mnautamani.

Niliporejea salama toka nchi za Msumbiji, Comorro, Uganda, Sudan, Shelisheli na kwingineko nilikokwenda, ndipo nilipotambua kuwa kuna watu wanaomba usiku na mchana ili pia majeshi yetu yetu yaweze kushinda hata kama yana Askari wazuri na silaha. Siku wananchi wakichachamaa kwa kodi yao mnayochezea; Mtajuta!

Ipo sheria ya Kijamii si ya Kiroho inasema, “Ni heri Dereva aue Mtu mmoja barabarani, kuliko kumkwepa mmoja huyo, halafu akaua walio wengi kwenye Gari lake”.

Wanaoitakia mema Tanzania, hawataki hata mmoja apotee, bali wote wafikirie toba wapone, wakiwemo wanaotokana matusi ovyo bila kujiheshimu.

Yesu katika Yohana 17:12 alisema hivi; “Nilipokuwapo pamoja nao, mimi niliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.” Kama walinzi wa wakilishi wetu hatutaki hata mmoja apotee.

Wazungu fulani (nawahifadhi),  kwa ujinga wao walikuwa na udanganyifu huu; Kitu kizuri akifanya Mwafrika walisema hicho siyo kizuri Kafanya Shetani. Lakini Mzungu akifanya Kibaya wanasema hicho ni Kizuri kafanya Mungu.  Wananchi siyo Shetani, ni Waheshimiwa.

Maoni, Maswali ama ushauri wasiliana na mwandishi kwa;
Barua pepe: nyyeregete@yahoo.co.uk 
Simu namba: 0715 933 308

No comments:

Post a Comment

Pages