HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 02, 2013

WAZIRI NCHIMBI: MAMBO YA NGOSWE MWACHIE NGOSWE


Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi

Na Bryceson Mathias 

‘Mtu akinywa Mchuzi amekula nyama, na akila nyama amekula’

NIANZE kwa kumuuliza Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi; Je Kunguru analiwa? Mayai yake nayo je, yanaliwa?

Ikitokea mtu anasema, hali Mayai ya Kunguru, ila anakula nyama ya Kurunguru, maana yake huyo si anakula Kunguru? Naye anayesema anakula Kunguru, bali hali Mayai yake, huyo ni muongo anakula vyote.

Siku moja tulibishana; watu watatu kutoka mikoa fulani, mmoja alisema hanywi Ulanzi ila Togwa yake anakunywa. Wa pili akaniambia, anakunywa Togwa, ila Pombe hanywi. Watatu akadai, anakunywa Mbege, Pombe ya ndizi hanywi.

Kwa msingi wa Mchuzi wa Nyama na Kunguru, Mtu akinywa Mchuzi amekula nyama, na mtu akila mayai amekula Kunguru.

Tukiwa Katika ubishi huo, alitokea mfanyabiashara wa ndizi, kunguru na supu ya nyama na kutukuta tukijadili biashara anayofanya. Aliomba atoe mchango wake, lakini kabla hajatoa mchongo huo, nilimtahadharisha kuwa asiitetee kazi yake ila azingatie hoja iliyoko mbele yetu akakubali.

Cha kushangaza alipoanza kutoa mawazo yake, alianza kueleza sifa za uzuri wa  Supu ya Nyama, Uzuri wa mayai ya Kunguru yalivyo chakula kitamu kwa Kenge na Mamba, na akamalizia kwa kusema Machicha ya Pombe ya Ndizi na Mianzi inavyojenga Nyumba akivutia kwake.

Hivi karibuni, Dk Nchimbi aliibukka na kumshambulia Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa (Chadema), akipinga madai  yake kwamba Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kuwa anajihusisha na mtandao wa ujangili nchini.

Tafsiri ya Chakula ni Afya, ukiona mtu anakula lakini hapati afya, hicho chakula anachokula hakina kitu ndani yake. Lakini ukiona mtu anakula Lishe na Afya yake inaboreka, basi chakula hicho kinafaa kwa mustakabali wa maisha.

Binafsi sikuona kama Tafsiri ya chakula cha Kinana kama ni afya kwa Dk. Nchimbi. Waswahili wanasema ya  Ngoswe mwachie Ngoswe mwenyewe.

Ninaamini bila shaka, Kinana ana majibu mazuri, na ndiye ambaye atatakiwa ajibu na kusikiwa na Watanzania ili wamuelewe.  Maana Nchimbi, naye anayo anayopaswa kuwajibu wabunge dhidii ya Jeshi la Polisi kutuhumiwa kutowesha nyara mikononi mwao.

Nchimbi angesimama kujibu tuhuma za wabunge kwamba, Polisi hawahusiki na kutoweka kwa vidhibiti vya pembe za ndovu, ambazo wabunge wengi wamedai zikifikishwa Polisi zinayeyuka au kugeuzwa kuwa kitu kingine na watuhumiwa wanaachiwa.

Namshauri Nchimbi asicheze upande wa adui, aelewe Darubini ni watu, vyombo ni msaada tu! Tuanachotaka Watanzania, si kusikiliza ubishani wa kuagizwa, tunataka Serikali ikae pamoja na wapinzani, ikubali kukosolewa, ipate uelekezi wa msaada tufaidi rasilimali zetu, na isiwe kila wanachosema wapinzani ni kibaya.

Habari ya “aliandikiwa tu akaenda kusoma, au vijembe vya uelewa wake unakuwa na utata mkubwa”, sisi wananchi kinachotusaidia hiki, kwa nini tumekupa Dhamana ya kuwa waziri wa mambo ya ndani Askari wapewa vidhibiti (Exhibits), vinabadilishwa au kutoweka bila kuchukuliwa hatua?

Tunafahamu bungeni na maofisini, ripoti mnaandikiwa halafu mnasoma tu. Wakati mwingine hampitii mkarekebisha makosa na mnatuaibisha ugenini!

Aliyekuwa anaandika na kutayarisha hotuba mwenyewe bila kuvuja wala siri kutoka nje, alikuwa ni Rais Benjamini Mkapa pekee.

Siri za Ofisi yake zilikuwa nadra kuzisikia nje ovyo ovyo, lakini si leo hii. Kila kitu kimekuwa na matobo kama waya Mbu kila mmoja anaona ndani. Hata habari hizo yawezekana wapinzani wameona ndani!  

 Maoni, Maswali ama ushauri wasiliana na mwandishi kwa;
Barua pepe: nyyeregete@yahoo.co.uk 
Simu namba: 0715 933 308

No comments:

Post a Comment

Pages