Na Bryceson Mathias
IMEBAINIKA, Muundo wa sasa wa Muungano una matatizo. Kwa mfano, Mbunge wa Zanzibar anawakilisha watu wachache zaidi ukilinganisha na mbunge wa Bara. Lakini cha kushangaza utaona wanalipwa sawa wakati wangetakiwa walipwe kwa Ngwe ya kazi yake.
Tabia ya kulipana fedha nyingi ya Kodi ya Walalahoi ambao hawamudu kula hata Mulo mmoja kwa siku, lakini wanalipwa kwa kazi kidogo, huku wabunge miongoni wengine wakilipwa fedha kidogo kwa kazi kubwa.
Mchezo huu mchafu, ni kama ufujaji wa Kodi ya wananchi, ambao kimsingi wakitambua kuna Wabunge wanalipwa fedha nyingi wakati wanafanya Kazi kidogo na wengine wanalipwe kidogo wakati wanafanya kazi kubwa, ni lazima ifike mahali wananchi warudishiwe haki yao.
Muda huo unaopotea bila kufanya kazi kutokana na maeneo yao kuwa madogo kiuwajibikaji, hali hiyo ndiyo inayosababisha wabunge wengine kuwa watoro majimboni mwao na kuwa na muda wa kuzurula nje ya majimbo.
Moja ya Matatizo yanayowafanya Wabunge wawajibike kidogo, ni kutokana na kwamba wengi wao hawaishi kwenye majimbo hayo bali wanaishi Dar es Salam ambapo wengi wao wana Miradi yao huko au kuwa na Ofisi Binafsi za kazi zao.
Kutokana na majukumu ya kibinafsi, hawapati muda wa kuzungumza na wananchi wao ili kujua kero na matatizo yanayowasumbua, kwa nadra hufika majimboni pale Viongozi wa Kitaifa wanapokuwa na ziara za kikazi majimboni mwao, ndipo wanapoonekana.
Wakati mwingine ambapo wabunge hunusa majimboni na kuondoka bila ya kuwa na mawazo na michango ya wananchi isipokuwa mawazo yao na viongozi wachache, ni kipindi cha kuelekea bungeni, ambapo hufika majimboni na kuwaita watendaji wachache ambao huwapotosha!
Kibaya wakati wa chaguzi ukifika, huanza kuhaha kununua mapombe na kujihangaisha kupika Ma-Ubwabwa Masufulia kwa Masufulia, huku wakijihangaisha kwa kuwarubni wananchi kwa Vijisumuni visivyo na tija wakijikuta wanarejea miaka mingine mitano ya Mateso.
Kutokana na wabunge kupata taarifa zisizo sahihi kwa watendaji wanaowachagua wakifikamajimboni, kunawafanya wakurupuke katika kuchangia hojs bungeni, ambapo wananchi wakibaini huwapigia wabunge wa upinzani kulalamika.
Waswahili wanasema Fimbo ya Mbali haiui Nyoka. Pengine ni vizuri wananchi kwenye majimbo yao wakapata uelewa na kutambua kuwa, nyakati za Michakato ya Uchaguzi wsibabishwe na Fimbo za Mbali zisizoua Nyoka, bali watumie walizonazo karibu wazionazo!
Aidha nawakumbusha wananchi, Shahada za kura zenu zina thamani kubwa sana ya kubadilisha hali ya maisha magumu yanayowatesa na kuwa mazuri! Shahada ni zaidi ya Almasi, Lulu, Madini, na kitu kingine chochote.
Shahada si ya kubadilishwa na Pombe, Mchele, Sukari Kilo Moja au Mshikaki wa Nyama. Shahada ni zaidi ya hapo, maana ina uwezo wa Kumtoa Diwani, Mbunge na Rais Madarani katika Maisha yako, Watoto wako, Taifa na Jamii kwa Ujumla.
Ukimuuzia Mtu Shahada, ni Sawa umemuuza Mwano kwa Chinjachinja (Mumiani), ni sawa Umeua Familia yako, Ni sawa Umemtoa Kafara Mwanao, Mzazi, Kitongoji, Kijiji, Kata, Tarafa, Wilaya, Mkoa na Taifa zima kwa Wachuna Ngozi.
Shahada za Kura ni Urithi wa Maisha yako kwa vizazi vya Uzao wako. Ni Rai yangu Vijana, Kina Mama, Kina Baba, muelewe, Shahada ni Shule, Zahanati, Sekondari, Barabara, Maji, na ni Vyuo Vikuu kwa Taifa la Kesho. Wabunge walipwe sawa na wanavyowajibika
nyeregete@yahoo.co.uk 0715-933308
No comments:
Post a Comment