Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo
Jumatano Juni 12, 2013 amekutana na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Klaus
Peter Blandes, ambaye amefika ofisini kwa Mheshimiwa Makamu wa Rais Ikulu Jijini
Dar es Salaam kwa lengo la kumuaga.
Balozi
Blandes alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa katika kipindi chake kama
Balozi nchini Tanzania, Ujerumani imeendelea kuwa mshirika mzuri wa Tanzania na
kwamba anaamini alikuwa anaendeleza historia ya mahusiano mema ambayo Tanzania
imekuwa nayo kwa miaka mingi.
Katika
maeneo ambayo Ujerumani imekuwa katika uwekezaji Tanzania ni sambamba na eneo la
Nishati ya umeme na usafirishaji ambapo tayari makampuni kadhaa ya Ujerumani
yameonesha nia ya kuwekeza katika Reli ya Kati kwa lengo la kufungua soko kwa
nchi za Afrika Mashariki. Pia, Ujerumani ina uwekezaji mkubwa katika sekta ya
ujenzi hususani viwanda vya saruji.
Kwa upande wa Mheshimiwa Makamu wa Rais
alimueleza Balozi Blandes kuwa amefanya kazi nzuri katika kuhamasisha mahusiano
baina ya Tanzania na Ujerumani na kwamba katika kipindi chake akiwa Balozi hapa
nchini, uhusiano wa Ujerumani kwa Tanzania umezidi kuimarika na mchango wa nchi
hiyo katika shughuli mbalimbali za maendeleo nchini Tanzania ni kiashirio kizuri
cha urafiki na udugu.
Mheshimiwa
Makamu wa Rais alimueleza pia Balozi Blandes kuwa, Ujerumani imeendelea kuwa
rafiki wa Tanzania na sasa pia rafiki wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Balozi Blandes anasema; “Ujerumani inaitazama Afrika Mashariki kama eneo ambalo
ni muhimu kwa uwekezaji na pia Tanzania inayo maeneo mengi ambayo yanaweza
kuboreshwa na hivyo kuzidisha uzalishaji kwa soko la ndani na nje.”
Balozi
Blandes anafafanua pia kuwa, Tanzania ina mengi ya kujivunia na ni nchi
inayoheshimika sana duniani. “Mheshimiwa Makamu kama hapa kwenu wanakuja
viongozi mbalimbali wakubwa wa Dunia mnachotakiwa kufanya ni kuendeleza pazuri
mlipo ili nchi yenu ipate tija,” anasema.
Katika
mkutano huo sambamba na Balozi Blandes kumshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa
ushirikiano aliompatia katika kipindi akiwa Balozi, pia Mheshimiwa Makamu wa
Rais alimtaka Balozi Blandes kuendelea kuwa rafiki wa Tanzania kwa kutumia
nafasi yake ya uwakilishi sambamba na yeye kama Balozi aliyefanya kazi vema hapa
Tanzania.
Imetolewa
na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Ikulu, Jumatano Juni 12, 2013
No comments:
Post a Comment