HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 26, 2013

Mwanza yachemka tamasha la filamu la Grand malt

Na Mwandishi Wetu

WAKAZI wa Mwanza wameanza kuchemka, wakati wakilisubiri kwa hamu Tamasha la Wazi la Filamu Tanzania, maarufu kama ‘Grand Malt Tanzania Open Film Festival’ likalofanyika katika Uwanja wa Nyamagana, jijini humo kuanzia Jumatatu ijayo.
 
Tamasha hilo la filamu, litakaloambatana na burudani mbalimbali zikiongozwa na bendi ya Extra Bongo ni mahususi kwa ajili ya kuonyesha filamu za Tanzania.
 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa jiji hilo walisema, hiyo itakuwa fursa kubwa kwao kukutana na wasanii wa ‘Bongo Movie’ pamoja na kuziona kazi zao walizofanya.
 
“Kwetu ni faraja kubwa mno, kwani tunawaona tu wasanii hao, lakini sasa ni wakati wa kukutana nao ana kwa ana,” alisema John Magesa mkazi wa Kirumba.
 
Elizabeth Mabula mkazi wa Ilemela, alisema ameshangazwa na maandalizi makubwa ya tamasha hilo, hivyo ni lazima ajipange kushuhudia kile kitakachojiri.
 
Mratibu wa Tamasha hilo aliye pia Mkurugenzi wa Sophia Records, Musa Kissoky, alisema amefarijika mno na jinsi wakazi wa Mwanza kwa jinsi wanavyolisubiri kwa hamu kubwa.
 
“Wakazi wa Mwanza wamelipokea kwa furaha mno tamasha hili, yaani tumefarijika mno na tunawaahidi litakuwa la aina yake.
 
“Kwa sasa maandalizi yamekamilika kwa asilimia 90, yaani tunaleta kitu tofauti ambacho watu watashangaa, ndio maana mpaka sasa wengi wanapigwa na bumbuwazi kuhusu kile tutakachofanya siku hiyo,” alisema.
 
Meneja wa kinywaji cha Grand Malt walio wadhamini wakuu wa tamasha hilo, Consolata Adam, naye alisema Mwanza itachemka zaidi kipindi chote cha tamasha hilo.
 
“Mwanza watapata kitu wasichokitarajia katika kipindi chote cha tamasha hilo, wasubiri kuona vitu visivyo vya kawaida,” alisema Consolata.
 
Tamasha la Filamu la Grand Malt linatarajiwa kuanza Julai 1-7, mwaka huu huku kukiwa na filamu mbalimbali zitakazooneshwa katika kipindi hicho. Filamu zote hizo ni kutoka Tanzania.
 

Tamasha hilo la filamu limedhaminiwa na kinywaji cha Grand Malt kisicho na kilevi ambacho kinazalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

No comments:

Post a Comment

Pages