DAR ES SALAAM, Tanzania
MAMLAKA ya Mawasiliano nchini (TCRA), imeitaka
Kampuni ya Sahara Media Group kurudisha chaneli yake kwenye mtandao wa
StarTimes kabla ya saa 10:00 jioni.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es
Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Profesa John Nkoma, alisema
kampuni hizo kwa pamoja hazina haki ya kuwanyima wananchi mawasiliano kutokana
na mgongano wao wa kimasilahi.
Alisema agizo la kuitaka Star TV kurudisha
chaneli inatokana na leseni yake ambayo imeambatana na masharti ambayo ni kutoa
huduma na si vinginevyo.
Profesa Nkoma alisema kitendo cha kutorudisha
huduma hiyo kitatafsiriwa kuwa imeshindwa kutoa huduma, hivyo ni vema
wakatambua kuwa wanaweza kunyang’anywa leseni.
“Leo tuliwaita Star TV na kuwauliza ni kwa nini
haikuonekana na tumewataka waeleze ni kwanini wamevunja sheria ya kutotoa
huduma kwa wananchi,” alisema Profesa Nkoma.
Hata hivyo, Profesa Nkoma alisema kuwa imeziita kampuni hizo na
anatarajia kukutana nazo Juni 17 mwaka
huu ili kila mmoja kujieleza ikiwezekana kumaliza mgongano huo unaonekana kuwa
wa kimasilahi zaidi.
Naye Meneja wa Sahara Media Group, Nathan
Lwehabura, akitolea ufafanuzi kuhusu tukio hilo, alisema Mei 23,
mwaka huu Star TV kupitia mwanasheria wake iliwataka StarTimes kuiondoa
kwenye king’amuzi chao ifikapo saa sita usiku wa Mei 31 mwaka huu kutokana na kurusha na kuuza maudhui na
vipindi vyake bila idhini na kukiuka sheria za hakimiliki (copyright laws).
Lwehabura alisema katika barua hiyo Star TV
iliwakumbusha StarTimes kwamba hawakuwa na mkataba wa kurusha kituo hicho kwa
mujibu wa sheria ya mawasiliano (EPOCA) pia hawana haki ya kutumia maudhui yake
bila idhini chini ya sheria ya hakimiliki ya Tanzania na kimataifa.
Alisema Mei 31, mwaka huu StarTimes/Star Media walijibu na kudai
kwamba hawajakiuka sheria yoyote wakasisitiza wataendelea kuirusha Star TV
kutekeleza matakwa ya sheria ya EPOCA na kanuni zake.
Lwehabura alisema Juni 6, mwaka huu, Star TV
iliwaandikia tena StarTimes ikisisitiza nia yake ya kuchukua hatua zaidi
kutokana na wao kuendelea kukaidi ombi hilo
na kuainisha mapungufu kadhaa ya kisheria kwa upande wao yanayoifanya Star TV
ijiondoe kwenye king’amuzi chao ifikapo saa sita usiku wa Juni 08 mwaka huu.
Aidha, Star TV ilieleza Star Media (T) Ltd ambayo inamilikiwa kwa
pamoja na Star Times na TBC ina leseni ya miundombinu ya kurusha matangazo ya
televisheni kupitia mfumo wa DTT (Multiplex Operator License).
Aliongeza kuwa leseni hiyo inawaruhusu kuingia makubaliano (Service
Level Agreement-SLA), na vituo mbalimbali kuwarushia matangazo yao lakini StarTimes hawana leseni ya kutoa
huduma ya maudhui (Content Service Provider License-CSP).
Lwehabura alifafanua kuwa StarTimes ni kampuni
ya kimataifa iliyoandikishwa (China ), inayotoa huduma ya maudhui katika nchi
mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania .
Alisema ili kupata maudhui inalazimika kuingia
mikataba na vituo vya televisheni kabla ya kuviingiza kwenye king’amuzi chake
na baadaye kuuza maudhui hayo (subscription/Pay TV), kwa walaji katika mataifa
hayo.
Alisema StarTimes inachukua vituo vya TV ikiwemo
Star TV bila idhini yao
na kuviweka kwenye king’amuzi chake kwa kisingizio kwamba wanaruhusiwa na
sheria ya EPOCA na kanuni zake.
Sheria hiyo inasisitiza juu ya kuwapo kwa mkataba
wa makubaliano (SLA ) kati ya pande mbili
husika.
Lwehabura alisema kwamba maudhui ya TV za Tanzania yanauzwa kwa walaji katika nchi
nyingine kama vile Rwanda , Burundi , Kenya ,
Uganda , Nigeria na
nyinginezo bila idhini ya wamiliki wake.
Alisema TV zinazomiliki maudhui hapa nchini
hazina uwezo wa kuidhibiti StarTimes isirushe maudhui yao
nje ya Tanzania kwa kuwa
baadhi ya maudhui wanayoyanunua nje kama vile tamthilia na vipindi vingineyo
haviruhusiwi na watunzi au wasambazaji wake yarushwe nje ya Tanzania (Territorial
Rights).
Lakini pia uhusiano wa makampuni haya mawili Star Media (T) Ltd na
Kampuni ya Star Times ambayo ni ya China ,
yenye matawi katika nchi nyingi za Afrika katika uendeshaji wa matangazo ya
dijitali haujabainishwa vizuri ili kujua nani ni nani na nini anachofanya hapa Tanzania katika
misingi ya maelewano ya kibiashara.
Alisema kutokana na mantiki ya hoja hizo Star
Times waliiondoa mara moja Star TV kwenye king’amuzi chao Juni 8, mwaka huu kama walivyoelekezwa na Star TV.
Alisema Star TV haioni sababu ya kulazimishwa na TCRA kurushwa na
Star Times pasipo kuondoa hitilafu hizo za kisheria na bila kuangalia sheria
nyingine zinazolinda haki za TV huru kama
sheria ya hakimiliki na sheria ya ushindani katika soko moja.
Serikali ya Tanzania
ni mwanachama wa WTO na pia WIPO (World Intellectual Property Rights
Organization), hivyo kwa kulazimisha uvunjaji wa sheria za hati miliki ina
maana inavunja haki zetu zilizopo kikatiba!
“Tutakwenda mahakamani kupata haki yetu hii muhimu,” alisema
Lwehabura.
Alisema sheria hii inaweka kinga kwa vipindi vya radio, televisheni,
nyimbo na sanaa zote, kwa kutaka kulazimisha StarTimes kupora vipindi vya Star
TV inadhihirisha kilio cha wasanii wa Tanzania
wasivyolindwa na serikali yao .
Lwehabura alisema taarifa iliyotolewa magazetini
na Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungi,
kwamba chaneli tano za kitaifa lazima zirushwe na ving’amuzi vyote bure
ni za kupotosha, kwa kuwa hata hiyo Star Times haizirushi bure, imekuwa ikibadilika
kama kinyonga.
Alisema lakini makampuni ya kigeni kama vile Dstv na Zuku wao hawarushi matangazo ya TV
nyingine bila makubaliano yanayotambulika kisheria.
Hata hivyo, vituo vikubwa vya TV vikiwamo Star TV, ITV, Channel 10 na
TBC na vinginevyo visivyo vya kitaifa vinarushwa na makampuni ya BTL na TIN
bila malipo yoyote ya mwezi na kwa ubora zaidi kuliko Star Times lakini
inashangaza kuona TCRA inawakingia kifua StarTimes wanaowalipisha Watanzania
badala ya kutetea vituo vya ndani visivyotoza chochote.
No comments:
Post a Comment