Mshindi wa tuzo tatu za Kilimanjaro Tanzania Music Awards 2013, Kala Jeremiah (katikati) akitoa neno la shukrani. Kushoto ni Mtayarishaji D Classic aliyefanya wimbo Dear God uliompa Jeremiah tuzo hizo.
Mwanamuzi Hussein Jumbe, akichana mistari ya kibao cha Khaleed Mohammed 'TID' kiitwacho Zeze katika usiku huo ndani ya Ukumbi wa Mlimani City.
Mkongwe Zahir Ali Zorro akikitendea haki kibao cha mkali wa Takeu, Lucas Mkenda kiitwacho Kikulacho.
Ommy Dimpoz kulia akipokea kutoka kwa msanii wa filamu nchini Wema Sepetu, tuzo ya Wimbo Bora wa Kushikiana uitwao Me and You aliomshirikisha Vanessa Mdee (katikati).
DAR ES SALAAM, Tanzania
KI-KWETU Kwetu ilikuwa ndio kaulimbiu iliyobeba mchakato wa
Tuzo za Muziki za Kilimanjaro (Kilimanjaro Tanzania Music Awards – KTMA 2013),
zilizofikia tamati Juni 8, katika Usiku wa Tuzo hizo kwenye Ukumbi wa Mlimani
City, jijini Dar es Salaam.
Hali ya mambo ilikuwa ya kuvutia mno katika usiku ule
uliotanguliwa na kimya cha dakika moja kuomboleza kifo cha Albert Mangweha
‘Ngwea’ aliyefariki Mei 28 nchini Afrika Kusini na kuzikwa Juni 6, katika
makaburi ya Kanisa la Mtakatifu Monica, Kihonda mjini Morogoro.
Burudani kali iliupamba usiku ule, huku mambo yakinoga kila
dakika zilivyokuwa zikiyoyoma; kabla, wakati na hata baada ya tuzo hizo
zinazodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya
Kilimanjaro Premium Lager ‘Bonge la Kiburudisho.’
Waliohudhuria ‘Usiku wa Tuzo’ Mlimani City Jumamosi ile,
watakuwa mashahidi wa hili na kwa kutambua thamani ya kilichofanywa na waratibu
na wadhamini wakuu Kilimanjaro, nathubutu kusema; Hongera TBL, lakini pia kwa
Basata na Innovex kwa kufanikisha mchakato.
Hongera kwa kufanikisha mchakato mzima wa KTMA 2013,
ulioambatana na tuzo mili za ‘All of Fame’ iliyoenda kwa Kilimanjaro Band ‘Wana
Njenje na ile ya ‘Individual All of Fame’ iliyoenda kwa nyota wa zamani wa
bendi ya Cuban Marimba, marehemu Salum Abdallah.
Hapa tunakuletea kwa ufupi matukio muhimu katika ‘Usiku wa
Tuzo,’ ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa wa aina yake kwa wasanii Kala Jeremiah,
Ommy Dimpoz na Chalz Baba na Bendi yake ya Mashujaa kwa kutwaa tuzo nyingi kati
ya tuzo 37 zilizotolewa.
Kala Jeremiah, Dimpoz, Mashujaa wang’ara KTMA
Kama ni utabiri uliotimia, gazeti hili linaweza kujivunia
kuwatabiria vema wasanii Kala Jeremiah na Ommy Dimpoz, ambao kupitia moja ya
makala zake iliwataja kuwa ni wasanii walio kwenye nafasi nzuri ya kuibuka na
tuzo nyingi na kujiwekea rekodi. Usiku wa Tuzo KTMA 2013 ukathibitisha hilo kwa
wakali hao kushinda tuzo tatu kila mmoja.
Kala Jeremiah alikuwa na usiku wa aina yake, ambapo alikuwa karibu
atwae tuzo nne, ingawa aliishia kutwaa tatu za Wimbo Bora wa Mwaka (Dear God),
Msanii Bora wa Hip Hop na ile ya Mtunzi Bora wa Hip Hop, huku akiipoteza ile ya
Wimbo Bora wa Mwaka wa Hip Hop (Dear God) iliyoenda kwa Nay wa Mitego kupitia
wimbo Nasema Nao.
Kwa upande wa Dimpoz, nyota pekee aliyekuwa akiwania tuzo
nyingi zaidi (saba) katika kinyang’anyiro hicho, alipata tuzo tatu za Wimbo
Bora wa Bongo Pop (Me and You aliomshirikisha Vanessa Mdee), kibao kilichompa
pia tuzo ya Wimbo Bora wa Ushirikiano.
Dimpoz akapokea tuzo ya tatu ya Video Bora ya Mwaka kupitia
kibao cha Baadae, huku akichemka katika kategori nne za Wimbo Bora wa Mwaka,
Msanii Bora wa Mwaka wa Kiume, Msanii Bora wa Mwaka wa Kiume wa Bongo Flava na
Mtunzi Bora wa Mashairi wa Bongo Flava.
Bendi ya Mashujaa waliibuka kidedea zaidi katika mchakato
huo, baada ya kujizolea tuzo tano, kupitia mbili za bendi (Wimbo Bora wa Bendi
– Risasi Kidole) na Bendi Bora ya Mwaka, huku ikitwaa tatu za wasanii wake,
ambao ni Chalz Baba aliyetwaa mbili za Mtunzi Bora wa Mashairi – Bendi na
Msanii Bora wa Kiume – Bendi.
Pia nyota wake Fagasoni aliibuka kidedea katika kategori ya
Rappa Bora wa Bendi, alikowabwaga Greyson Semsekwa, J4, Jonico Flower na Sauti
ya Radi. Ndo kusema Mashujaa wakiongozwa na Chalz Baba, ‘walitisha mno’ usiku
ule na kuzipoteza bendi na wanamuziki mahiri wa dansi nchini.
Dimpoz na ushindi wa ‘neno bora’ la ‘Usiku wa Tuzo’
Kwangu mimi, msanii Ommy Dimpoz alikuwa zaidi ya mshindi,
kwani licha ya tuzo zake tatu, aliibuka mshindi pia kwa kutoa kauli nayoweza
kuiita ‘bora zaidi’ kuliko zote zilizotolewa na washiriki wengine zaidi ya 100
waliofika ama kutuma wawakilishi wao.
Nyuma ya ‘neno bora,’ Dimpoz aliitoa tuzo moja kwa Vanessa
Mdee, kati ya mbili alizoshinda kupitia kibao alichomshirikisha cha ‘Me and You’
na kutafsiriwa kama ‘aliyempoza’ binti huyo aliyebwagwa katika kategori ya
Msanii Bora Anayechipukia, ambayo ilienda kwa Ali Nipishe.
“Napenda kumshukuru kila aliyefanikisha mimi kupata tuzo
hii, ambayo nina furaha kwani nimekabidhiwa tuzo hiyo shemeji yangu
(akimaanisha Wema Sepetu aliyemkabidhi),” alisema Dimpoz huku akimtania; ‘Kama
vipi tukutane baadaye shemeji.’
Akionekana kuiva na semina elekezi kwa wateule ‘nominees’
iliyotolewa na TBL kupitia Bia ya Kilimanjaro, Dimpoz alisema: “Kama msanii na
Mtanzania, napenda kusema kuwa, tumechoka kuwazika wasanii maskini wenye majina
makubwa katika ‘game.’
“Ifike kipindi kila mmoja kwa nafasi yake aumizwe na hali
duni kimaisha na kimapato tuliyonayo wasanii na kuzikwa tukiwa maskini licha ya
majina makubwa tuliyonayo na kuyapata katika tasnia hii wakati wa uhai wetu,”
alisisitiza Dimpoz huku akiamsha hisia za mashabiki ukumbini.
Ni kauli ambayo haiitaji ufafanuzi, ingawa mwenyewe hakusita
kuifafanua: “Serikali na wadau wa muziki nchini, ndio wawezeshaji watakaofanikisha
ukubwa wa majina yetu kwenda sambamba na pato letu.
“Serikali itusaidie kupitia michakato sahihi ya hatimiliki
na wadau watoe kipaumbele kwa wasanii wa nyumbani. Sio tunafanya tamasha, huku
maonesho yetu yakipambwa na picha za kina Messi (Lionel), kama wao ni zaidi
yetu, basi waitwe tuone kama watashangiliwa,” alisema.
Dimpoz akawa ametoa ujumbe bora ambao kwangu mimi naupa
ushindi wa ‘Neno Bora Zaidi’ la Usiku wa Tuzo, ambalo ni aghalabu kusikia
likitamkwa na msanii, badala yake tungetegemea kulipata kutoka kwa Mgeni Rasmi,
ambaye KTMA umfanya kuwa ni ‘Brand Manager’ na usiku ule alikuwa ni George
Kavishe, Meneja wa Bia ya Safari.
Hussein Jumbe, Zahir Ali ‘Zorro’ Jose Mara wafunika
Burudani ukumbini zilianza saa 3:30 usiku kwa Mrisho Mpoto
na wakali wanaounda Mjomba Bendi, waliopanda jukwaani baada ya dakika moja ya
maombolezo ya kifo cha Ngwea – ambaye picha za msanii zilioneshwa katika kila
‘screen’ iliyokuwa ukumbini hapo.
Ahadi ya burudani kali kwa watakaohudhuria ‘Usiku wa Tuzo’
iliyotolewa na Kavishe ikaanza kudhihiri wasanii waliotumbuiza walipokuwa jukwaani.
Amini Mwinyimkuu ‘Amini’ alifuata ‘Kikwetu Kwetu’ akiuchanganya wimbo wake wa
Ni Wewe na ngoma ya Kabila la Wamakonde ‘Sindimba.’
Mtangazaji na Mtayarishaji wa Kipindi cha Supa Mix cha East
African Radio na Uswazi cha East African TV, Hillary Daudi ‘Zembwela,’ akafuata
mara kadhaa jukwaani na visa vilivyovunja mbavu vya Bure Mbaya kilichohusisha
Dereva wa gari ya vichaa na kile cha Busara Haiuzwi kilichohusisha muuza
mahindi mwenye kigugumizi.
Licha ya Zembwela kufunika na simulizi ya visa hivyo na
vingine kibao, bado mashabiki hawatowasahau wakali wa muziki nchini Hussein
Jumbe na Zahir Ali ‘Zorro,’ waliowapagawisha kwa aina ya muziki usio wao na
nyimbo zisizokuwa zao pia huku wakizitendea haki.
Zilikuwa dakika 10 za kukata na shoka, ambapo Jumbe aliingia
ukumbini saa 5:32 na kibao cha Zeze kilichoimbwa na Khaleed Mohammed TID. Zeze
la Jumbe likaacha gumzo ukumbini, huku nyota huyo wa dansi akikitendea haki
stejini kwa kukicheza na kunata na mistari.
Katika staili ya bandika-bandua ‘non-stop,’ saa 5:37, Jumbe
akampisha Zorro aliyepanda na kibao cha Kikulacho kinguoni mwako, kilichoimbwa
na mkali wa TAKEU, Lucas Mkenda ‘Mr Nice.’ Manjonjo ya Zorro wakawakumbusha
wengi zama za Mr Nice. Hakika Zorro na Jumbe wakaacha midomo wazi mashabiki.
Mfululizo huo wa burudani za bandika bandua, ukaendelea saa
6:22, ambapo Barnabas Elias ‘Barnaba’ na Snura ‘Mama Majanga’ walifululiza kwa
burudani kali, kisha kupisha tuzo kadhaa, kabla ya saa 6:55 mizuka ya wengi ukumbini
kupandishwa tena na Jose Mara.
Jose mmoja wa nyota wanaounda kundi la Mapache Watatu,
alijikusanyia fedha nyingi zaidi za kutuzwa jukwaani, ‘alipowakimbiza’
mashabiki kupitia kibao cha ‘Kinyaunyau’ cha Kilimanjaro Band ‘Wana Njenje,’ na
kufanya mfuko wa shati lake la Kinigeria kujaa noti na nyingine kumwagwa chini.
Lady Jaydee, Diamond wazua manung’uniko
Diamond Platnumz, aliyeibuka mshindi wa medali mbili za
Msanii Bora wa Kiume na ile ya Msanii Bora wa Kiume wa Bongo Flava, haikuelezwa
nini kilisababisha kutofika ukumbini, ambapo tuzo zake hizo zilipokelewa kwa
niaba yake na binti ambaye hata hivyo hakujitambulisha ni nani.
Hamu ya mashabiki kumuona Diamond iliyoanzia katika ‘Red
Carpet’ ikaamshwa upya kila alipotajwa kushinda tuzo na kuzua maswali miongoni
mwa mashabiki wake, kama ilivyokuwa pia kwa
‘swahiba’ wake wa siku za karibuni, Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la Ney
wa Mitego.
Ilikuwa hivyo kwa Jaydee. Mrembo wa Tanzania 2012, Brigite
Alfred ndiye aliyepanda jukwaani kumtangaza mshindi wa kategori ya Msanii Bora
wa Kike, ambapo Isha Mashauzi, Khadija Kopa, Lady Jaydee, Mwasiti Almasi na
Recho walikuwa wakichuana.
Brigite akashika karatasi yenye jina la mshindi aliyoitoa
katika bahasha na aliposema: Mshindi wa Msanii Bora wa Kike niii…..mashabiki
wakalipuka kwa kelele ukumbini na kumalizia Lady Jaydeeeeeee!!!! Na wakarudia
jina hilo mara
kadhaa, kuionesha kukosa kwake mpinzani.
Ndipo aliposoma kwa kutaja jina la Jaydee kuwa mshindi na
kuamsha shangwe ukumbini, iliyokuja kusindikizwa na maneno; shemejiii,
shemejiiii, kufuatia mume wa Jaydee, Gadna G. Habashi kupanda jukwaani
kumpokelea tuzo hiyo ya kategori pekee kwa nyota huyo mwaka huu.
Licha ya utetezi wa Gadna kuwa Jaydee yu safarini mkoani
Shinyanga alikoenda kutumbuiza katika kinyang’anyiro cha kumsaka mrembo wa mkoa
huo, bado kiu ya mashabiki hao haikuweza kukatwa.
Ndipo Gadna alipowaamsha upya mashabiki hao alipowapa ujumbe
wa nyota huyo wa kuwakaribisha katika tamasha la Juni 14 la kuadhimisha Miaka
13 ya Jaydee katika muziki, litakalofanyika kwenye Ukumbi wake wa Nyumbani
Lounge, ambapo waliitikia: Tutakujaaaaaaaaa!!!!
Kauli ya mama wa Sharo Milionea/Ahadi za washindi
Kama ilivyotarajiwa, washindi wa tuzo mbalimbali walikuwa na
kauli tofauti, zilizotanguliwa na ile ya Mama wa aliyekuwa mkali wa maigizo na
muziki wa Bongo Flava, Ramadhani Mkieti ‘Sharo Milionea,’ Zaina Mkieti,
aliyekuwa ndani ya Ukumbi wa Mlimani
City kumwakilisha mwanaye
aliyekuwa akiwania tuzo mbili.
Sharo Milionea alikuwa akiwania tuzo za Wimbo Bora wa Bongo
Pop na Wimbo Bora wa Kushirikiana kupitia Chuki ni Bure aliomshirikisha Dully
Sykess na akiwa katika ‘Red Carpet,’ Zaina akafunguka kuhusu tuzo hizo na namna
anavyojisikia miezi sita tangu kifo cha mwanaye.
“Nashukuru kwa yote, michakato iliyofanikisha mimi kuwa hapa
leo, lakini pia mwanangu kuwa mteule ‘nominees’ bila kujali kama
atashinda ama atashindwa. Miezi sita sasa tangu kufariki kwa mwanangu, tukio
hili linanipa faraja kuona kuwa Watanzania bado wanathamini kazi za marehemu
mwanangu,” alisema Zaina.
Pia mtangazaji wa kituo cha televisheni cha Citizen cha
nchini Uganda (ambaye jina lake halikupatikana), aliyepokea tuzo Jose
Chameleon, aliyeshinda kategori ya Wimbo Bora wa Afrika Mashariki, kupitia
kibao cha Valu Valu, alikuwa na machache kuhusu muziki Afrika Mashariki.
Mtangazaji huyo alitoa ujumbe wa Chameleon kwa Watanzania,
akiwataka wasanii na mashabiki wake kutoachwa nyuma na michakato mbalimbali ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki, badala yake wajiunge ili kupaa pamoja kimuziki nje
ya ukanda huo unaojumuisha nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi.
“Ahsante Mungu kwa kunipa tuzo nyingine, ingawa hii nayo
haitokani na wimbo mwingine, nakuomba wewe unijalie kazi nyingine, itakayoweza kutisha
na kutwaa tuzo za mwaka mwingine,” alishukuru na kuahidi Kala Jeremiah
akiigizia kibao chake cha Dear God kilichompa tuzo zake.
Jeremiah akaamsha simanzi ukumbini kwa kauli hii: “Katika
Dear God, nilikuwa na maombi maalum kwa waliokuwa wagonjwa wetu; Sadick Juma
Kilowoko (Sajuki) na Fatma Bint Baraka ‘Bi Kidude.’ Niliwaombea kwa Mungu
kuonesha navyowapenda, lakini Mungu kawapenda zaidi.”
Jeremiah akawataka Watanzania kupendana kila mmoja kwa
nafasi yake, ambapo yeye atawaenzi Sajuki na Bi Kidude aliowaombea katika wimbo
huo, pamoja na ‘msela wake’ Ngwea kwa kuhakikisha anafanya kilicho bora kila
mwaka. Akamaliza kwa kumtakia uponaji mwema na wa haraka, Rita Poulsen ‘Madam
Rita.’
“Amenitoa mbali Madam na alipaswa kuwa hapa kushuhudia
matunda haya pamoja na kupokea moja ya tuzo hizi, lakini kutokana na tukio la
ajali lililompata, hayuko ukumbini hapa na sisi, namuombea kwa ‘Dear God’ apone
haraka,” alisema Jeremiah na kushangiliwa na mashabiki.
Msanii Chalz Baba, aliahidi kuwalipa mashabiki waliompigia kura
yeye na bendi yake ya Mashujaa kwa kuwadondoshea ‘kibao’ kipya cha ‘Ushamba
Mzigo,’ huku Luiza Mbutu aliyeshinda tuzo ya Msanii Bora wa Kike wa Bendi,
‘akii-dedicate’ tuzo hiyo kwa mashabiki wa Twanga Pepeta.
Washindi wa tuzo ya Wimbo Bora wa Mwaka wa Raggae, kundi la
Warriors From The East, wakatoa shukrani za dhati kwa waasisi wa muziki huo
nchini Innocent Garinoma, Innocent Nganyagwa ‘Ras Inno’ na wengineo kwa
harakati zilizoifikisha reggae mahali ilipo sasa.
Fred Maliki ‘Mkoloni’ aliyepanda jukwaani kupokea tuzo ya
Wimbo Bora wa wa RnB kwa niaba ya Rama Dee aliyeshinda kupitia kibao Kuwa na
Subira alichowashirikisha Mapacha, alisema nyakati za ‘vinega kuwa busy’ kikazi
unaendelea kutokana na vita dhidi ya wanyonyaji kushika kasi.
Makala hii imetayarishwa na Salum Mkandemba
Maoni, mswali kwa mwandishi: Simu namba 0789 947 744
Barua Pepe: mkandemba@yahoo.com
No comments:
Post a Comment