HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 17, 2013

MWANDISHI WA HABARI MKONGWE, DAVID MAJEBELLE KUZIKWA MAKABURI YA KINONDONI JULAI 18

MWILI  wa mwandishi mkongwe  David Michael Majebelle.  aliyefariki alfajiri ya Jumapili iliyopita unatarajiwa kuzikwa katika makaburi ya Kinondoni JIJINI Dar es Salaam Julai 18

Kwa  mujibu wa taarifa rasmi ya familia iliyotolewa leo, mwili huo utaletwa  kutoka katika hospilai ya Mwananyamala  ulikohifadhiwa kisha kupelekwa nyumbani kwake eneo la Sinza  jirani na Lion Hotel   ambapo heshima za mwisho zitatolewa majira ya saa sita mchana kisha  kulepekekwa katika kanisa katoliki la Maria Mama wa Mwokozi  lililopo Sinza na baadaye saa tisa kupumzishwa katika makaburi ya Kinondoni.

Marehemu Majebele alizaliwa tarehe 03/05/1941 katika kijiji cha Ibiri, Wilaya ya Tabora Vijijini, Mkoa wa Tabora, akiwa mtoto wa tatu (3) wa familia ya watoto 10 wa Mzee Michael Kanyata Majebelle na Mama Theresia Malwa Majebelle ambao wote kwa sasa ni marehemu.

SHULE

Alisoma shule ya Msingi ya Bukene (1950) Puge, Wilaya ya Nzega, Mkoa wa Tabora tangu mwaka 1951, Baadaye katika Shule ya Kati (Middle School) ya Sikonge, Wilaya ya Sikonge, Mkoa wa Tabora, mwaka 1954 mpaka 1957.
Alijiunga na Tabora Boys School kwa masomo ya sekondari mwaka 1958 mpaka mwaka wa 1961.

Marehemu alikuwa mpenzi wa mpira wa miguu na aliwahi kushiriki kwenye mashindano ya SUNLIGHT CUP enzi zake.

KAZI

David aliajiriwa na kampuni ya Almasi ya Williamson Diamonds Ltd ya Mwadui, Shinyanga mwaka 1962 kama Public Relations Trainee. Mwaka 1963 alipelekwa Uingereza kusomea Stashahada ya Uandishi wa Habari/Upigaji Picha za Uandishi. 

Baada ya kuhitimu alibaki nchini humo kwenye Kampuni ya The Anglo American Corporation kupata uzoefu kable ya kurejea Mwadui kuendelea na kazi ya Afisa Uhusiano wa kampuni ya Williamson Diamonds Ltd hadi Septemba 1967 alipojiuzulu na kuajiriwa na Shirika la Ndege la Africa Mashariki (East African Airways) na kituo chake cha kwanza kikiwa ni Uwanja wa Kimataifa wa Embakasi – Nairobi. Oktoba 1971 alipewa uhamisho na kupelekwa London Uingereza kuwa mwakilishi wa Shirika hilo kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa HEATHROW – London.

Julai 1974 alihamishwa kutoka Uingereza na kuletwa Tanzania kuwa Meneja Mauzo wa Kampuni Tanzu ya Shirika lililojulikana kwa jina la SIMBA AIR. Lilipovunjika Shirika la Ndege la Africa Mashariki (East African Airways)’

David Majebelle alijiunga na Shirika jipya la Ndege la Tanzania (Air Tanzania) kama Meneja Mauzo. Mwaka 1978 aliacha kazi katika Shirika hilo na kujiunga na wamiliki wa magazeti ya AFRICA NEWS na baadaye NEW AFRICA mpaka mwaka wa 1990 kituo chake kikiwa Uingereza. Baada ya pale alianzisha Kampuni yake binafsi kwa jina la MEDIA ADVERTISING CO.Ltd iliyojihusisha na Uhusiano, Matangazo, Upigaji Picha ikiwemo za magazeti mbalimbali kama;

The Financial Times of London, New Africa African Business, Profit Magazine ,The African Review  na magazeti ya hapa nyumbani
Kadri umri wake ulivyokwenda aliandamwa na magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu. Ilibidi apunguze kasi ya kushughulikia Kampuni hiyo mpaka alipoifunga.

FAMILIA

David Michael Majebelle alifunga ndoa mwaka 1975. ameacha mke na watoto wane (4), wa kiume mmoja na wa kike watatu.

UMAUTI

Katika miaka miwili ya mwisho wa maisha yake, marehemu amekuwa akisumbuliwa na kisukari na shinikizo la damu. Jumatano iliyopita alifanyiwa vipimo huko hospitali ya Agha Khan ambako aligundulika kuwa amepata “multiple mild strokes”. Jumamosi kuamkia Jumapili iliyopita alifariki dunia.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi, Amina.

Raha ya milele umpe ee Bwana; na mwanga wa milele umuangazie, apumzike kwa amani, Amina.

No comments:

Post a Comment

Pages