Na Mohammed Mhina wa Jeshi la Polisi, HANDENI, Tanga
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kwemakumbi katika kijiji cha Kireguru wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Hamza Rajabu Ngaramilo (56), leo amehukumiwa kifungo cha miaka minne jela baada ya kupatikana na hatia ya kuomba na kupokea rushwa ili kugawa ardhi kwa wahamiaji wageni kijijini hapo.
Akisoma hukumu katika kesi nambari 113/12 iliyosomwa kwa mara ya kwanza Mei 7, mwaka jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Handeni mkoani humo Patrick Maligana, amesema kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa Serikali na hivyo anamtia hatiani mtuhumiwa huyo kama alivyoshtakiwa katika kosa hilo.
Awali Mwendesha Mashtaka wa (TAKUKURU) wilayani Handeni Bw. George Magoti, alidai kuwa Septemba mwaka 2012 siku na wakati usiofahamika, mtuhumiwa akiwa ni mtumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilindi kwa nafasi ya Mwenyekiti wa kitongoji cha Kwemakumbi katika Kijiji cha Kireguru, aliomba na kupokea rushwa ya shilingi 300,000.
Mtuhumiwa huyo wakati huo akiwa na umri wa miaka 55, alipokea fedha hizo kutoka kwa Gwandu Gaheri Langida na Kesi Safari Tlatlab ambao wote ni wahamiaji wageni kutoka katika kijiji cha Mang’ola Barazani wilaya ya Karatu mkoani Arusha ili awapatie ardhi kwa ajili ya kilimo.
Mwendesha Mashitaka huyo alisema, mtuhumiwa huyo aligawa ardhi hiyo yenye ukubwa wa ekari 40 jambo ambalo alisema ni kinyume cha sheria za ugawaji wa ardhi vijijini.
Bw.Magoti ameifafanulia mahakama hiyo kuwa, kwa mujibu wa taratibu za ugawaji wa ardhi vijijini, Mwenyekiti wa kitongoji ama kijiji anao uwezo wa kugawa ardhi isiyozidi ekari kumi kwa malipo ya shilingi 5,000 kwa mwanakijiji mkazi na shilingi 10,000 kwa mwanakijiji mhamiaji tofauti na alivyofanya mtuhumiwa kwa wahamiaji hao wageni.
Mwendesha Mashtaka huyo wa TAKUKURU ameiomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho kwa Wenyeviti wengine wanaokiuka utaratibu wa ugawaji wa ardhi vijijini na kuwafanya wananchi kutoa fedha nyingi kinyume na utaratibu kama ilivyo kwa mtuhumiwa huyo kitendo kinachotafsiriwa kuwa ni rushwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Maligana alisema kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na kwa kuzingatia umri mkubwa wa mtuhumiwa huyo, anamhukumu kulipa faini ya shilingi 150,000 ama kwenda jela miaka minne kama atashindwa kulipa faini hiyo.
Lakini ili kujua kwamba maisha ni magumu hasa huko vijijini waliopo Wanzania wengi, Mtumiwa huyo alipelekwa Gerezani kuanza kifungo cha miaka minne jela baada ya kushindwa kulipa faini hiyo ya shilingi 150,000 na hivyo kuanza maisha mapya ya kifungwa Gerezani.
Hata hivyo pamoja na Mshitakiwa huyo kubadilishwa jina na kuitwa mfungwa, lakini Hakimu amesema anaweza kutoka Gerezani wakati wowote endapo atatokea ndugu ama rafiki wa kumlipia faini hiyo na stakabadhi ya malipo ya serikali ikapelekwa kwa Mkuu wa Gereza la Handeni. Ardhi husika itaendelea kubaki mikononi mwa walalamikaji.
No comments:
Post a Comment