Na Bryceson Mathias
NG’OMBE ni Mfugo, lakini kwa walio wengi unatafsiriwa kama Kiwanda chenye mazao mengi yanayozalishwa kama bidhaa adimu.
NG’OMBE ni Mfugo, lakini kwa walio wengi unatafsiriwa kama Kiwanda chenye mazao mengi yanayozalishwa kama bidhaa adimu.
Mbali ya bidhaa nyingi zinazotolewa na ng’ombe, kubwa ambayo inafahamika hata na mtoto mdogo ukimtaja ng’ombe ni zao la kumkamua maziwa.
Mazao mengine ya ng’ombe ni Kwato, Ngozi, Samli, Mbolea, Pembe, Zana ya Kilimo, Usafiri, Chombo cha kubebea Mizigo, Nyama, Usinga wa kutegea Ndege, Kifaa cha Kufyekea Majani, na wakati huohuo ni Chombo cha kuharibu mazao kisipochungwa kwa uangalifu.
Kwa kawaida, Ng’ombe hawezi kutoa maziwa mengi kama hakulishwa ipasavyo, na mbali ya malisho anatakiwa atunzwe na kutibiwa maradhi pindi yanapomkabili, ili kumuepusha kifo kitakachopelekea hasara kwa mfugaji.
Kwa nyakati hizi, Mtanzania wa kawaida na Mlalahoi, hivi sasa anafananishwa kama ng’ombe anayekamuliwa kila siku mithili ya ng’ombe wa maziwa ambaye hata hivyo mfugaji wake amemwacha akonde na kunyongea kwa kutompa malisho ya kutosha.
Ingawa wafugaji wazuri wa nyumbani hudiriki hata kuwapa pumba, kuwatafutia nyasi au laa hata jiwe la chumvi la kulamba wakati wa kumkamua apate kunenepa; watanzania wameachwa wabebe mzigo wa Kodi, kupanda kwa bei za bidhaa, Ada, Nauli kiasi maisha yanawawia magumu.
Ng’ombe huyu alijinasibu kwamba, pengine akitoa Kwato, Ngozi, Samli, Mbolea, Pembe, akilima, akatoa usafiri, akabeba Mizigo, atoa Nyama, Usinga wa kutegea Ndege, atasababisha majani ale ili akikamuliwa atoe maziwa, mambo yamekuwa sivyo! Anakamuliwa bila lishe hadi anatoa damu.
Hali hiyo inaakisi watanzania, wanazo rasilimali nyingi, Madini, Wanyama, Mazao ya Misitu, hivi sasa Gesi, Fursa za Utalii, Uwekezaji wa aina mbalimbali, Mazao ya Bahari, Mito, Maziwa na Ardhi na nyingine nyingi. Lakini vijijini na mijini watanzania bado ni maskinii wa kutupwa.
Kukamuliwa kwa Kodi mbalimbali, Matokeo ya mfugo au Kiwanda hiki Mtanzania, sasa amekamuliwa hadi damu inamtoka mwilini, huku akiwa amefungwa kamba miguuni na kukosa uhuru wa rasilimali zake alizonazo, ambazo hunufaisha wageni (Wawekezji) walio miungu watu!
Tufanye Mkamuaji ni Serikali! Naye anatokwa Jasho jembamba usoni, anahangaika kwa udi na uvumba huku na kule kusaka maziwa (Fedha ya Bajeti ) ambayo nayo imebadilika rangi na kuota mbawa ikawa nyekundu, maana kila msaada ukija kutoka nje, una riba ambayo watu lazima waulipe.
Ipo mifano mingi ya jinsi ambavyo Watanzania wanavyokamuliwa hadi wanatoka damu, Wingi wa kodi ambazo hakika zimewekwa na serikali na hazielekei kuwapunguzia wananchi mzigo.
Kwa wale ambao wamo kwenye kundi la utumishi wa umma, kampuni binafsi au wote wanaoishi kwa ujira kwa maisha yao yote, wanalia kwa nyongeza za nauli, bei vyakula, Mafuta ya taa, Mavazi, Kodi za Nyumba, gharama za matibabu, Elimu, vifaa vya Ujenzi, na kadharika.
Aidha watanzania walalahoi, kwa sasa wamebaki wanasubiri kudra ya Mungu iwanusuru, maana hata wakiwageukia Wawakilishi baadhi waliowachaguwa (Madiwani na Wabunge), ikiwemo mihimili Mitatu Serikali, Mahakama na Bunge), pia hawaoni tumaini, ni kusikia Rushwa, Ufisadi, Matusi bungeni badala ya kuwatetea.
Wengine wanadiriki kusema, hata tume zinazoundwa ili yu mkini zifuatilie na kubaini maumivu na mateso ya watanzania walala hoi, zimekuwa si tume bali tu-u-me tu! Hivyo hawana msaada na mahali salama pa kugeukia.
Jamani, anayetukamua, aelewe tumekamuliwa kiasi cha kutosha! Sasa tunatoa damu, tunataka malisho.
nyeregete@yahoo.co.uk 0715-933308
No comments:
Post a Comment