HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 06, 2026

Simba yaifuata Azam FC nusu fainali NMB Mapinduzi Cup

WEKUNDU wa Msimbazi Simba SC, wamefuzu nusu fainali ya mashindano ya NMB Mapinduzi Cup 2026, baada ya kuwachapa Fufuni SC ya Pemba kwa mabao 2-1 kwenye dimba la New Amaan Complex, hapa Zanzibar na sasa ni rasmi wataumana na Azam FC katika nusu fainali.


‎Haikuwa rahisi kwa Simba inayonolewa na Steven Barker kuibuka na ushindi huo, kwani ililazimika kutoka nyuma kwa bao 1-0, baada ya Fufuni SC kutangulia kwa bao la mapema dakika ya 14 likiwekwa kambani na Mboni Steven Kibamba. 

‎Baada ya bao hilo, Simba ilitulia na kurejea mchezoni taratibu na kusawazisha kwa bao la beki Hussein Mbegu kunako dakika ya 22 na kuzipeleka timu hizo mapumziko kwa sare ya bao 1-1.

‎Wakati wengi wa mashabiki wakiamini  Simba itafuzu nusu fainali kwa sare hiyo, mtokea benchi Naby Camara akawaandikia bao la pili katika dakika za nyongeza za mtifuano huo, bao ambalo likampa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi na kuzawadiwa Sh. Mil. 1.

‎Naye Karimu Ali Khamis wa Fufuni SC, alitangazwa kuwa mshindi wa Tuzo ya Mchezaji Mwenye Nidhamu Zaidi 'NMB Most Discipline Player' wa mechi hiyo na kujitwalia kitita cha Sh. 500,000 kutoka kwa wadhamini wakuu wa Mashindano hayo, Benki ya NMB. 


‎Simba SC watarejea dimbani New Amaan Complex Alhamisi Januari 8 kuumana na Azam FC katika nusu fainali kali ya kukata na shoka, huku Singida Black Stars wao wakimsubiri Yanga ama TRA United kujua mpinzani wao wa nusu fainali ya pili itakayopigwa Ijumaa Januari 9.

‎Washindi wa nusu fainali hizo watakwea pipa kuelekea Pemba, itakounguruma fainali ya aina yake ya mashindano hayo hapo Januari 13 kwenye Uwanja wa Gombani, ambako Bingwa atazoa Sh. Mil. 150, huku mshindi wa pili akivuna Sh. Mil. 100 kutoka kwa wadhamini NMB.

No comments:

Post a Comment

Pages