HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 18, 2013

25 WACHUKUA FOMU UCHAGUZI TFF



Wanamichezo 25 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) unaotarajiwa kufanyika Oktoba 27 mwaka huu.

Fomu hizo zilianza kutolewa juzi (Agosti 16 mwaka huu) ambapo wawili wamechukua nafasi ya Rais na wengine wawili Makamu wa Rais wakati waliobaki wanaomba ujumbe wa Kamati ya Utendaji wakiwakilisha kanda mbalimbali.

Waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwa wagombea urais ni Jamal Malinzi na Omari Musa Nkwarulo wakati umakamu wa rais hadi sasa umewavutia Wallace Karia na Ramadhan Nassib.

Waliochukua fomu za ujumbe ni Athuman Kambi, Charles Komba, Davis Mosha, Elias Mwanjala, Eliud Mvella, Epaphra Swai, Farid Nahdi, Hussein Mwamba, Jumbe Magati, Kamwanga Tambwe na Khalid Mohamed.

Wengine ni Muhsin Balhabou, Omari Abdulkadir, Omari Walii, Samwel Nyalla, Shaffih Dauda, Stanley Lugenge, Twahir Njoki, Vedastus Lufano, Venance Mwamoto na Wilfred Kidao.

Kwa upande wa Bodi ya Ligi Kuu aliyechukua fomu mpaka sasa ni Hamad Yahya anayeomba kuteuliwa kugombea nafasi ya uenyekiti.

Fomu za maombi pia zinapatikana kupitia tovuti ya TFF ambayo ni www.tff.or.tz Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni saa 10 kamili jioni ya Agosti 20 mwaka huu.

Fomu zikiambatanishwa na risiti ya malipo (receipt) au malipo ya benki (deposit slip) kupitia akaunti ya TFF namba 01J1019956700 iliyoko CRDB tawi la Holland House zirejeshwe kwa Katibu Mkuu wa TFF kwa mkono au kwa barua pepe (email) ambayo ni tanfootball@tff.or.tz .

MECHI YA NGAO YA JAMII YAINGIZA MIL 208
Mechi hiyo ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa 2013/2014 iliyochezwa jana (Agosti 17 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 208,107,000. Washabiki 26,084 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa Yanga kushinda Azam bao 1-0.

Mgawanyo wa mapato ya mechi hiyo uliokuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 31,745,135.59, asilimia 10 ya mchango wa kusaidia jamii sh. 20,810,700, gharama ya tiketi sh. 7,309,866.

Uwanja sh. 22,236,194.76, gharama za mchezo sh. 13,341,716.86, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 5,188,445.44, TFF sh. 13,341,716.86 na Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 6,670,858.43. Kila klabu imepata mgawo wa sh. 43,731,183.03.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages