HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 08, 2013

Je hivi sasa, tuna Viongozi wa siasa au tuna Wababaishaji?

Na Bryceson Mathias
 
LICHA ya kuwa na baadhi ya viongozi wazuri nchini, bado tunao Wababaishaji ambao wangepaswa kusimamia sheria za nchi na kanuni zake, lakini wamekuwa wa kwanza kukiuka taratibu  wakiruhusu uvunjifu wa sheria kwa makusudi, mchana kweupe!
 
Uvunjifu huo wa sheria unaofanywa na baadhi ya watendaji wa sekta mbalimbali, umepelekea kuonekana kwa sasa hatuna viongozi wanaowajibika kwa wananchi na Taifa lao, badala yake tumejikuta tuna viongozi ambao ni bora viongozi.
 
Kwa hivi sasa imekuwa ni jambo la Kawaida kuona Diwani au Mbunge, anaweza kutoa taarifa isiyo ya Uongo, kwamba Mradi fulani kwa mfano wa Zahanati, Maji au Nyumba za Walimu umekamilika au uko kwenye kiwango cha Lenta kumbe hata Msingi bado.
 
Halmashauri nazo kwa kutokuwa na kawaida ya Uwajibika na ufuatiliaji, Utakuja zinabeba taarifa hizo na kuziwakilisha kwenye Serikali Kuu na wakati mwingine kuziwakilisha bungeni katika mijadala ya bajeti kumbe si sahihi.
 
Cha kushangaza, Vyama vya upinzani vinapoanza kupinga kukamilika kwa miradi hiyo kwa vielelezo na hatimae kubainika, Serikali kupitia kwa Mawaziri wamelishwa Uongo, na fedha hizo zimetumika kwa kitu kingine au zimelambwa. Hali huwa tete!
 
Nitoe mfano wa Viongozi Wababaishaji kwa picha! iliyoambatanishwa. Hivi karibuni katika Ujenzi wa Zahanati ya Mlaguzi Kata ya Sungaji Wilaya ya Mvomero, Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo walidanganywa na kupewa taarifa ya Uongo kuhusu ujenzi wa Zahanati ya Mil.30.5/-.
 
Viongozi wa Kijiji cha Mlaguzi na wa Kata ya Sungaji, waliudanganya pia Uongozi wa Halmashauri na Wilaya, Uongozi wa Mkoa na Serikali Kuu, kwamba Ujenzi wa Zahanati hiyo uko kwenye Lenta wakati  hata msingi haujaisha tangu 2011 hadi leo Agosti 2013.
 
Pamoja na uongo huo, hakuna kiongozi yeyote wa Kijiji, Kata, Halmashauri wala Wilaya aliyewajibishwa kwa uzembe wa kiasi hicho.
 
Hadi sasa Viongozi husika wilayani humo, bado wanakalia viti, Ingawa wakaguzi waliwasilisha ukaguzi na taarifa hiyo kuwa ni kweli ujenzi huo hauko kwenye Lenta ila hata msingi haujaisha, na ndicho kilipelekea wananchi kuwakataa viongozi wa Kijiji.
 
Hali hiyo pia imeanza kuvinyemelea na Vyombo vya habari na mitandao ya kijamiii hapa nchini, ambapo hivi karibuni mwananchi mmoja toka Morogoro, Elineus Rwegasira, alivilalamikia kuwa viikuwa na Mdahalo wa Dk. Wilbroad Slaa na Philip Mangula mwepesi.
 
Rwegasira anahoji, “Hivi kilichofanyika kuhusu mdahalo wa viongozi hao ni Uhariri uliorekodiwa au ni nini hasa? Je haiwezekani katika uhariri huo kumefichwa mambo mengi? Sisi tunataka Mdahalo wa Moja kwa Moja kwa viongozi wetu!” alisema Rwegasira akiumia!
 
Hatuwezi kumpuuza Rwegasira kwa kutunyoshea kidole wanahabari wa vyombo vyote kuhusu mtazamo wake, labda tunachoweza kuhamasishana ni kuhakikisha tunaboresha uandishi na mahojiano mbalimbali tunayofanya kwa jamii na viongozi, ili walaji habari wale Mulo kamili.
 
Kwa nini viongozi mnaowahudumia wananchi mnatoa taarifa za uongo? Mnataka kumpendezesha yupi na kumuudhi nani? Ni vema mkaelewa kuwa, Mchezo wenu wa usanii ni hatari kwa Jamii na Taifa zima.
 
Iwapo mnafanya hivyo kwa kudhani wananchi ni mbumbu hawawezi kufuatilia mkawa na nia ya kujirundikia masifa kwenye vikao vyenu vya uongozi, wananchi sasa wana ueledi na uelewa mkubwa wa kujua kila senti ya Kodi yao inatumikaje. Hivyo kuwadanganywa ni kujimaliza.
 

No comments:

Post a Comment

Pages