‘Mbwa hawezi kumbeba Paka Mgongoni’
Na Bryceson Mathias
Tafadhali, naomba leo katika Hoja hii nianze na swali! Je
hivi samba akitaka kumla mtu anaweza kupewa siku saba ajirudi iwapo anataka
kumla mtu au huwa anamrarua tu? Twebde pamoja kwenye kisa hiki.
Hivi karibuni madiwani wa Mkoa wa Kagera
wanaokemea ufisadi na kuchukiwa na watawala,
tulihabarishwa walitakiwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) Taifa, Phillip Mangula na Katibu Mkuu
wake , Abdulrahman Kinana, wamalize mgogoro wao “kwa busara.”
Mbali ya juhudi za Viongozi hao wa juu wa CCM, ni swali
langu kwa wenye uchungu na nchi hii, Je, Ufisadi ni Busara? Lakini swali langu
la pili lisilo na kigugumizi ni hili, Simba akitaka kukutafuna anaweza kupewa
muda ajirudi ili asikutafune? Si kweli, atakurarua tu!
Kusudi la makala hii ni namna gani maslahi ya Taifa na haki
za maendeleo ya wananchi zinachakachuliwa na kubarikiwa kwa kukutazamisha
mgogoro sugu uliopo baina ya meya, Anatory Amani , na Madiwani wa CCM, CHADEMA
na CUF, ambao Agosti 5, walimfukuza rasmi Meya wa Manispaa yao ya Bukoba.
Sababu Madiwani hao wa wananchi kuamua kumfukuza Meya Amani,
ni kunatokana na kile wanachodai hawana Imani naye,
kufuatia kuwepo tuhuma za Ufisadi wa Mradi
wa viwanja Bukoba,
Mradi wa Soko, Mradi wa ujenzi wa stendi kuu ya mabasi na
mtafaruku wa nyaraka.
Aidha kutokana na kuwepo ufujaji wa tuhuma hizo za mamilioni
ya fedha za miradi ya walipa kodi , wadau tunapata shida, Je kwa hali kama hiyo
Viongozi wa CCM Taifa wanaweza kuona ni jambo tu la kusema tu mtuhumiwa na
wanaosigana, wamalize tofauti zao? La hasha kuna hatua lazima zichukuliwe.
Vilevile haitoshi viongozi wanaotegemewa na wananchi
kusimamia na kutatua kero zao, kama viongozi wa Mkoa, Meya na
Madiwani, kusema wamalize mgogoro kwa busara, wakati busara inayotakiwa katika
ufujaji huo wa fedha ni kuwajibishwa! Tangu lini wizi ukaitwa
kusogeza?
Tumehabarishwa kuwa, CCM na serikali mkoani humo hawataki
Meya aondoke, na inadaiwa kunapangwa mpango wa kuwafukuza madiwani wao
walioweka sahihi zao kumfukuza meya. Je hii maana yake ni kuukumbatia ufisadi
huo au ni kuupaka rangi?
Kuna hofu kwamba, madiwani wa CCM waliosaini kumfukuza Meya
huyo, hivi sasa wanatembea na kadi zao mfukoni tayari kwa kuzikabidhi iwapo
uongozi wa chama chao utaamua kulinda ufisadi wa meya na kuwachukulia hatua
wao.
Pengine sasa ifike mahali viongozi wetu waanze
kujitathimini, kwa nini wanapofanya makosa ya tuhuma za ufisadi, wanakimbilia
kujikinga mahakamani ili waendeleze michezo hiyo michafu?
Ilifahamika, Mkurugenzi Amani alipotakiwa aitishe kikao cha
baraza la madiwani wa Bukoba na kukataa akihofu ndicho kingemfukuza, Meya na
mkurugenzi wa manisapaa walikimbilia mahakamani kuweka pingamizi la kuzuia
madiwani kuitisha kikao cha kumwondoa.
Ninaipongeza mahakama kwa kutupilia mbali shauri hilo, ili
kutojiingiza kwenye tabia ya kukumbatia waharifu wanaodhulumu haki za wananchi
wakiitumia taasisi hiyo kama kofia ya Chuma ya kulinda maovu.
Tunadokezwa kuwa, uamuzi wa meya na mkurugenzi kwenda
mahakamani ulitokana na agizo la Mkuu wa Mkoa ambaye alimwandikia Mkurugenzi akimzuia
kuitisha kikao cha baraza la madiwani kama alivyokuwa ametakiwa na madiwani hao
kwa mujibu wa kanuni.
Kama viongozi tunaowaamini na kuwategemea kama Mkuu wa Mkoa,
Mangula, Kinana, wanaweza kuongoza kundi la kutoa mawazo Mtuhumiwa huyo abebwe,
ilihali wanafahamu fika uovu unaolalamikiwa dhidi ya Kiongozi huyo, wananchi
waende kulalamika kwa nani?
Binafsi ninaunga Mkono hatua za Madiwani 16 wa Kagera kumng’oa
Kiongozi wao kufuatia tuhuma zilizowekwa mbele yake, kimsingi tunahitaji
viongozi watakaoongoza mapambano ya kukataa wananchi na Ulalahoi
waliosababishiwa, wasidhulumiwe haki na maslahi yao.
Aidha nawashauri Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe,
Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Mangula na Katibu Mkuu Kinana kwamba, hatua ya
kuwafukuza madiwani hao haimalizi mgogoro, na hakuna busara inayoweza kutumika
kwenye ufisaji zaidi ya mtu kuwajibiaka.
nyeregete@yahoo.co.uk 0715933308
No comments:
Post a Comment