JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
KUREJESHWA
KWA URUSHAJI MATANGAZO RADIO IMAAN FM NA KWA NEEMA FM RADIO
1.0 Utangulizi:
Mnamo tarehe 26/02/2013 Kamati ya Maudhui ya
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ilitoa uamuzi wa kuvifungia vituo vya
utangazaji vya Radio Imaan ya mjini Morogoro na Kwa Neema FM Radio ya jijini
Mwanza baada ya kukiuka Sheria na Kanuni za Utangazaji.
Kamati ya Maudhui iliuita uongozi wa vituo
hivyo tarehe 11/02/2013 na tarehe 14/02/2013 ili kujitetea na vyote vilikiri
kosa. Baada ya kutafakari utetezi wa Radio Imaan na Radio ya Kwa Neema FM na
kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Utangazaji, Kamati iliamua kutoa adhabu kwa
vituo vyote viliwi kama ifuatavyo:-
a)
Vituo
vyote vilipewa onyo pamoja na kufungiwa
kurusha matangazo kwa kipindi cha miezi sita kuanzia tarehe 26/02/2013;
b) Vituo vyote
vilitakiwa kuithibitishia Mamlaka ya Mawasiliano na
Kamati ya Maudhui kwa maandishi kuwa hawatarejea kutenda kosa la aina hiyo au
linalofanana na hilo. Ikiwa vitarudia Kamati ya Maudhui haitasita kuvifutia
leseni zao za utangazaji.
2.0 Kutekeleza adhabu na hatua zilizochukuliwa
na vituo hivyo
na
Mamlaka ya Mawasiliano:
Baada ya Uamuzi huo kusomwa, vituo vyote
viwili vilianza kutekeleza adhabu mara moja kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa
Sheria na Kanuni za Utangazaji. Mamlaka ya Mawasiliano ilipokea barua ya
udhibitisho wa kutofanya kosa tena yaani “Commitment letter” pamoja na sera ya
uhariri (Editorial Policy) na ratiba ya vipindi kutoka kwa vituo vyote viwili.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ilifanya
ukaguzi kwa vituo vyote viwili ili kujiridhisha na kuzipitia sera za uhariri
pamoja na mwongozo wa vipindi kabla ya kuvifungulia.
3.0 Kurejeshwa
kwa Matangazo
Kamati ya Maudhui iliandika barua tarehe
27/08/2013 kuhusu kuvifungulia vituo hivyo vya utangazaji vya Radio Imaan ya
mjini Morogoro na Kwa Neema FM Radio ya jijini Mwanza baada ya kutumikia adhabu
kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utangazaji. Vituo hivi vimeanza kurusha matangazo
yake kuanzia leo tarehe 28/08/2013 baada ya muda wa adhabu kuisha.
Kamati ya Maudhui inapenda kutumia fursa hii
kuvionya vyombo vya habari vya utangazaji vya redio na televisheni kuwa makini
katika kutekeleza masharti ya leseni pamoja na kufuata Sheria na Kanuni za
Utangazaji. Kamati ya Maudhui haitasita kutoa adhabu kali au kuvifungia vituo
vitakavyokiuka Masharti ya leseni, Sheria pamoja na Kanuni za Utangazaji au
hata kuvifutia leseni zao.
Kamati ya Maudhui inatoa wito kwa vyombo vya
habari vya utangazaji kuzingatia Sheria, Kanuni na Masharti ya leseni
ilikuboresha Sekta ya Utangazaji na kudumisha amani nchini.
Eng.
Margaret Munyagi
Mwenyekiti,
Kamati
ya Maudhui Ya TCRA,
S.L.P.
474,
DAR ES
SALAAM.
28/08/2013
No comments:
Post a Comment