Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeshindwa kusikiliza pingamizi mbili zilizowasilishwa mbele yake dhidi ya waombaji uongozi wawili baada ya kukosa sifa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za TFF.
Kwa mujibu wa Ibara ya 11 (3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, pingamizi ni lazima iwekwe na mwanachama wa TFF (vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu) au kiongozi wa kuchaguliwa wa TFF.
Pia pingamizi yoyote ni lazima iwe kwa maandishi ikieleza wazi sababu za pingamizi pamoja ushahidi wa kuunga mkono pingamizi hilo, jina kamili, anuani ya kudumu na kusainiwa na mweka pingamizi au Mwenyekiti/Katibu wa mwanachama husika.
Pingamizi hizo ziliwasilishwa na Shamsi Rashid Kazumari na Samwel Nyalla dhidi ya Wallace John Karia anayeomba kuwania nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF na Vedastus Kalwizira Lufano anayeomba kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda Namba Mbili ya mikoa ya Mara na Mwanza.
Kwa upande wa Kazumari ambaye alikiri hata kutowahi kuiona Katiba ya TFF pamoja na Kanuni za Uchaguzi, pingamizi lake halikusikilizwa kwa vile si mwanachama wa TFF wala kiongozi wa kuchaguliwa wa TFF. Wakati pingamizi la Nyalla halikusikilizwa kwa vile hakukuwa na ushahidi wowote uliowasilishwa, hivyo kushindwa kukidhi matakwa ya Ibara ya 11(3) ya kanuni husika.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment