HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 28, 2013

Warembo Redd’s Miss Tanzania watamba

Na Mwandishi wetu
WAREMBO wanaoshiriki shindano la Redd’s Miss Tanzania, kwa nyakati tofauti wametamba watafanya kweli katika kinyang’anyiro hicho pale walipokutana na waandishi wa habari katika hoteli ya Giraffe iliyopo Kunduchi, Dar es Salaam jana.
Wengi wao walionekana kujiamini zaidi na kudai wana uhakika mkubwa wa kushinda taji hilo, ambalo kwa sasa linashikiliwa na Brigette Alfred.
“Kwangu nataka kufanya kweli zaidi, kwani najua wapi naweza kuwashinda wenzangu hawa,” alisema mrembo Elizabeth Pert anayetoka mkoa wa Pwani.
Janet Awet wa Lindi naye alijisifu kwa hilo na kudai ana sifa zote za kutwaa taji, hivyo wenzake wajiandae kuwa wasindikizaji katika shindano hilo.
Lucy Charles wa Mwanza na Esha Rashid kutoka Mara nao walitoa tambo zao, huku Severina Lwinga na Mariam Manyanga (Kanda ya Vyuo), walitamba wao ndio wana uhakika wa mmojawapo kuondoka na taji.
Mkurugenzi wa Kampuni Lino, Hashim Lundenga ambao ndio waandaaji wa Redds Miss Tanzania alisema, kwa sasa kila kitu kimekamilika na anaamini warembo hao wote wana sifa zinazostahili..
“Wasichana wote waliopo hapa wana sifa za kutosha, naamini kwa dhati kabisa Redd’s Miss Tanzania kwa mwaka huu atakuwa na sifa zote zinazotakiwa.”
Meneja wa Redd’s, Victoria Kimaro naye alisema, kama wadhamini wapo tayari kuhakikisha shindano hilo linafanikiwa kwa kiasi kikubwa zaidi na kumtoa mrembo bora.
“Tunaamini kabisa kama Redd’s shindano hili litatoa mrembo bora zaidi kuliko kipindi chote kwani ukiwatazama unaona wana sifa zote,” alisema.
Warembo wanaoshiriki na kanda wanazotoka zikiwa kwenye mabano ni Happiness Watimanywa (Dodoma), Sabrina Juma (Tabora), Nice-Jack Herman (Singida), Anastazia Donald (Tabora), Linah Allan (Rukwa), Jacqueliene Luvansa (Mbeya), Neema Mality (Iringa), Diana Laizer, Sabra Islam (Moro), Janet Awet (Lindi) na Elizabeth Pert (Pwani).
Wengine ni Lucy Charles (Mwanza), Esha Rashid (Mara), Salsha Isdory (Geita), Severina Lwinga, Mariam Manyanga (Kanda ya Vyuo), Lucy James (Chuo Kikuu Huria), Svetlana Nyameyo (Kurasini), Narieth James (Chang’ombe), Latifa Mohamed (Kigamboni).
Wapo pia Lucy Tomeka (Dar Indian Ocean), Prisca Clement (Sinza), Philios George (Ubungo), Sarah Martin, Dorice Mollel (Tabata), Alice Isaac na Carol Bayo (Dar City Centre).

Redd’s Miss Tanzania kwa sasa inadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

No comments:

Post a Comment

Pages