HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 27, 2013

Ligi Kuu ya Grand Malt yashika kasi Z’bar
Na Mwandishi Wetu
Ligi Kuu ya Zanzibar, maarufu zaidi kama Grand Malt Premier League, kwa sasa ni tishio kutokana na ushindani mkubwa uliopo baina ya timu shiriki.

Kumbuka miaka michache nyuma wakati ligi hiyo ilipokuwa inahaha kusaka wadhamini, lakini pale Grand Malt moja ya kinywaji bora kabisa kisicho na kilevi ilipojitokeza na mambo yote yalikaa sawa.

Msimu uliopita udhamini ulikuwa ule wa kuzisaisia timu zaidi na uendeshaji wa mambo mengine, lakini msimu huu mambo yamebadilika, hivyo kuifanya iwe ngumu zaidi.

Ndio maana si ajabu kuona mabingwa watetezi KMKM wakiwa ‘katika hali mbaya zaidi’, huku Mtende wakiongoza ligi hiyo kwa kujikusanyia pointi 11 kutokana na michezo mitano iliyocheza.

Mtende mpaka sasa haijapoteza mchezo hata mmoja, ikiwa imefunga mitatu na kutoka sare miwili na inaonekana ni ngumu zaidi kwani imefunga magoli nane na kufungwa matano.

KMKM wanaowania taji hilo kwa mara nyingine wapo nafasi ya tano wakiwa na pointi saba kwa michezo mitatu, huku wakiwa wameshinda miwili na kutoka sare mmoja. Wana magoli sita ya kufunga na wamefungwa mawili.

Chuoni ambao msimu uliopita walishika nafasi ya pili, mpaka sasa na wao wako katika nafasi hiyo wakiwa na pointi tisa kwa michezo minne waliyocheza, huku wakifungwa mchezo mmoja.

Wazee hao wa dufu wameweka kimiani mabao saba na kufungwa mawili, huku Miembeni ‘Wazee wa Kale’ wakiwa nafasi ya nane kwa pointi tano walizonazo. Wameshinda mmoja, sare mbili na kufungwa miwili, ikiwa imepachikwa wavuni mabao nane na yenyewe kushinda matano.

Mafunzo wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi tisa, lakini yenyewe ikiwa imeshinda mabao saba na kufungwa matatu, huku Fufuni ikiwa ya nne kwa pointi kama hizo ikiwa imeshinda mabao matano na kufungwa matatu.

Polisi ni ya sita ikiwa na pointi saba kwa kushinda michezo miwili, kufungwa na kutoa sare mmoja, ina mabao matano ya kufunga na kufungwa manne, ikifuatiwa na Chipukizi yenye pointi sita iliyoshinda michezo miwili na kufungwa mitatu.

Malindi ni ya tisa ikiwa na pointi nne ikiwa imeshinda mchezo mmoja, kutoa sare mmoja na kufungwa miwili, Kizimbani ikiwa ya kumi kwa pointi nne, lakini imefungwa mabao mengi, huku Zimamoto ikiwa ya 11 kwa pointi moja iliyonayo kibindoni.

Jamhuri inashika mkia ikiwa na pointi moja tu, kwani katika michezo yake mitano imetoa sare mmoja na iliyobaki ikiwa imefungwa, huku ikishinda mabao matatu tu na kufungwa 10.
Timu hii ndiyo inayoongoza kwa kufungwa mabao mengi ikifuatiwa na Kizimbani na Chipukizi zilizofungwa mabao tisa kila moja,  pamoja na Miembeni iliyofungwa mabao nane.

Zilizo na ukuta mgumu ni Mafunzo na KMKM zilizofungwa mabao mawili kila moja, wakati zinazoongoza kwa kufunga ni Mtende na Chipukizi zikiwa na mabao nane kila moja.

Mchezaji anayeongoza kwa mabao ni Faki Mwalim wa Chipukizi aliyepiga nne mpaka sasa, akifuatiwa na Abdi Kassim ‘Babi’ (KMKM), Ahmed  Omar (Chipukizi), Ali Salum (Mtende), Erik Klaudi (Fufuni) na Yahya Said (Mtende) walio na mabao matatu kila mmoja.   
     
Mambo yatakuwaje msimu huu? Msimu uliopita kipa bora aliibuka Khamis Uzidi wa Zimamoto ambaye alikabidhiwa kombe pamoja na fedha taslimu sh 500,000 huku mfungaji bora wa ligi hiyo akiwa, Juma Mohamed Juma wa Chuoni, akiondoka na sh milioni 1 na kombe.

Mchezaji bora wa Grand Malt Premier League msimu uliopita alikuwa ni Abdullah Juma wa Jamhuri ya Pemba, alikabidhiwa sh milioni 1 pamoja na kombe.

Meneja Masoko wa Grand Malt, Fimbo Butallah, anasema wao wamefurahishwa kwa kiasi kikubwa na udhamini wa kinywaji chao, kwani kwa kiasi kikubwa imesaidia kukuza soka la Zanzibar.
“Tunataka kuhakikisha tunalikuza soka la Zanzibar na kufika mbali zaidi, hivyo Grand Malt itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na ZFA, katika kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa.”

Ligi Kuu ya Zanzibar kwa sasa inadhaminiwa na kinywaji kisicho na kilevi cha Grand Malt, ambacho kimekubali kuidhamini kwa misimu mitatu mfululizo, huku ikisema itahakikisha inazidi kuiboresha kila msimu.

No comments:

Post a Comment

Pages