HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 19, 2013

Mikoa ilivyojiandaa kulipokea Tamasha la Krisimasi

Na Mwandishi Wetu

WAKATI siku za kusherehekea sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo zikikaribia, Wakuu wa mikoa itakayofanyika tamasha hilo wanalisubiri kwa hamu tamasha hilo ambalo litashirikisha mikoa mitano ya Tanzania bara.

Sikukuu hiyo inayotarajia kuadhimishwa Desemba 25 duniani kote, kupitia tamasha hilo la kumsifu na kumuabudu Mungu kupitia nyimbo za Injili  zitakazoshirikisha waimbaji mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania.

Mikoa ambayo inatarajia kusherehekea kwa pamoja tamasha hilo ni pamoja na Dar es Salaam (Desemba 25), Morogoro (Desemba 26), Tanga (Desemba 28), Arusha(Desemba 29) na Dodoma (Januari 1 mwakani).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama anasema maandalizi ya tamasha hilo yamekamilika kwa kiasi kikubwa, hivyo waumini wajiandae kwa tamasha hilo ambalo litazungumzia zaidi amani.

Msama anasema tamasha hilo limedhaminiwa na gazeti la Dira ya Mtanzania, linatarajia kushirikisha waimbaji Solomon Mukubwa (Kenya), Eiphraim Sekeleti (Zambia), Liliane Kabaganza (Rwanda) na Solly Mahlangu Obrigado (Afrika Kusini) wakati Tanzania itawakilishwa na Rose Muhando, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, John Lissu, New Life Band na Edson Mwasabwite.

Aidha Msama alitaja viingilio kwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ni shilingi 20,000 kwa VIP A, VIP B 10,000, viti vya kawaida shilingi 5000 na watoto shilling 2000 huku kwa mikoani ni shilingi 5000 kwa wakubwa na watoto shilingi 2000.
  
Baadhi ya mikoa ambayo inatarajia kufikiwa na tamasha hilo, wakuu wake walitoa matamko ambayo ni  mwenendo wa mafanikio ya kufanikisha tamasha hilo kama ifuatavyo:

DODOMA 
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk Rehema Nchimbi  anasema tamasha hilo litazamwe kama fursa ya kuwakutanisha pamoja na kuondoa tofauti zao za kiimani na kuitangaza amani tuliyoasisiwa na baba wa Taifa Mwalim Julius Kambarage Nyerere,” ni maneno ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi.

Mkoa wa Dodoma ambao ni Makao Makuu ya Chama na Serikali pia ndio mkoa ulio katikati ya nchi ambao unaunganisha mikoa yote ya Tanzania bara ambao pia una sifa ya ukarimu kwa wageni na ni nafasi pekee kwa watakaoshiriki katika tamasha hilo kujionea utalii ulioko katika mkoa huo.

Dk. Nchimbi anasema tamasha hilo linatakiwa liwe ni nafasi muhimu kwa kila mmoja na kuondoa tofauti  mbele ya Mungu  ambaye anatukutanisha pamoja kwa sababu lengo lake ni umoja.
Dk. Nchimbi anasema waumini wajitokeze kwenye tamasha hilo bila kutazama atakayepanda jukwaani na badala yake tutazame maadili ya nyimbo ambazo zitamzungumzia na kumtukuzia Mungu kwa mambo mema.

Dk. Nchimbi anasema siku hizi kuna baadhi ya waimbaji wanatoka nje ya mstari kwa kuimba nyimbo za burudani zaidi na kuachana na maadili ya dini na kutinga kwenye jamii zaidi kiburudani.

Mkuu huyo wa Mkoa anasema kupitia tamasha hilo ni mahali pa kurudisha  uhai na afya kati ya wanaoishi na Virusi vya Ukimwi na kuondoa unyanyapaa kupitia nyimbo za dini jamii itasahau madhila yanayomsumbua.

Nchimbi anasema mkoa wa Dodoma ni tunu ambayo inatakiwa kutumiwa ipasavyo  na wageni watakaofika mkoani humo kwa ajili ya kupata neno la Mungu.

Anasema wananchi wa Dodoma watumie nafasi hiyo kuwakutanisha watu mbalimbali ili wajisikie wapo nyumbani  ili warudi mkoani humo kwa mara nyingine  kwa ustaarabu ambao haupatikani mahali popote hapa nchini.

Anasema ili kufanikisha maendeleo hayo inatakiwa tutazingatie panapotuunganisha na kutuweka pamoja  na kuachana na yanayotutenganisha yanayotokana  na migogoro  ambayo inayochafua taswira ya maendeleo ya jamii.

Tamasha hilo ni nafasi kwa waimbaji  kuonesha vipaji vyao na kuwekeza ili kujipatia vipato ambavyo vitafanikisha kutambulika kimataifa ambako wanatakiwa kuonesha ubunifu  kwani kila aliye hai ana kipaji ambacho amezaliwa nacho alichopewa na Mungu.

MOROGORO
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera amepongeza hatua ya waandaaji wa tamasha hilo kuutambua mkoa huo kwamba unastahili kuwemo katika orodha ya mikoa itakayopata huduma ya neno la Mungu kupitia waimbaji watakaoshiriki.

Bendera aliyasema hayo juzi katika mahojiano na mwandishi wa makala hii na kueleza kwamba wanalisubiri  tamasha hilo kwa hamu hasa ukizingatia litaongeza chachu ya pato la mkoa huo na Taifa kwa sababu wageni watafanya shughuli mbalimbali kabla na baada ya tukio hilo.

Bendera anasema ni furaha iliyoje kusikia tamasha kama hilo kufanyika mkoani kwake kwa sababu litachangia maendeleo ya mkoa huo.

Bendera anasema Tamasha la Krismas litachangia vijana kujifunza mengi kutoka kwa waimbaji wa nje ya Tanzania na waimbaji wa hapa nchini ambao wamepiga hatua ya maendeleo katika nyanja ya muziki wa Injili ambao wanaitangaza vilivyo nchi yetu.

Bendera anasema tamasha la Krismas litapunguza safari kwa wakazi wa mkoa wa Morogoro ambao wamepanga kusafiri kwenda mikoa mingine kwa ajili ya sherehe hizo, hivyo anatoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kukaa mkao wa kula kwa ajili ya tamasha hilo.

“Morogoro ni mmoja wa mikoa ambayo ina vivutio vingi, hivyo tamasha hilo litachochea kutangazika kwa vivutio hivyo ili wageni waendelee kutembelea mkoa huo ambao ni mojawapo ya mikoa ambayo inasifika kwa amani,” alisema Bendera.

Aidha Bendera anasema kupitia tamasha hilo, mkoa utakuwa na mzunguko mkubwa wa fedha ambao utaongeza pato la Taifa na mwananchi wa Morogoro kuanzia Desemba 23 hadi mwanzo wa mwaka ujao kutoka shughuli mbalimbali yakiwemo matamasha kama hilo.

Bendera anasema wanajipanga kufanya ukarimu kwa wageni watakaofika katika tamasha hilo ili warudi kwa mara nyingine katika matukio mengine ili kufanikisha maendeleo ya mkoa huo kimapato.
Mkuu huyo wa mkoa alitumia fursa hiyo kuwataka waandaaji wa tamasha hilo, kumpa taarifa mapema ili aweze kuomba ufadhili katika maeneo mbalimbali ya wadau ili liendane na sikukuu hiyo.

ARUSHA
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo amewapongeza waandaaji wa tamasha hilo kwa kusema kuwa hakuna kitu kizuri kama kuwakutanisha Watanzania pamoja kwa lengo la kuiombea amani ya Taifa idumu.

“Nampongeza sana Alex Msama na pia namuomba aje Arusha haraka ili tuzungumze niwasaidie kulifanikisha tamasha hilo hapa Arusha na pia niwape wadau wengine ambao watawasaidi kufanikisha kwa ufanisi zaidi kwa sababu watu wa Arusha nawafahamu na kwamba wanapenda sana matamasha” anasema Mulongo.

Mulongo anasema hilo ni jambo jema machoni pa Mungu na kwamba litawafanya Watanzania wakutane kwa pamoja na kutafakari mienendo yao kwa mwaka mzima unaokwisha.

“Mimi naomba wafanye tamasha kubwa ambalo halijawahi kutokea hapa Arusha, mimi nipo tayari kuwasaidi kwa lolote, chochote wanachokihitaji kwa ajili ya kufanikisha tamasha hilo ambalo maudhui yake ni kulinda amani na kuiendeleza kwa sababu huweza kwenda kuabudu kama hakuna amani, natamani sana kuonana na Alex Msama kwa ajili ya mazungumzo ya maandalizi ya huku mkoani kwangu Arusha” anasema Mulongo na kuongeza kuwa 
“Mkoa wa Arusha ni mkubwa na unawafanyabiashara wengi wanaopenda ibada na matamasha ya kumsifu Mungu, hivyo mimi pia ni muumini wa hili hivyo nipo tayari na ninalipokea Tamasha la Krismas kwa mikono miwili na ninamuombea Alex asikengeuke aka hairisha kuja Arusha” anasema Mulongo.

Historia inaonyesha kuwa mji wa Arusha ulianzishwa enzi za utawala wa Wajerumani katika mwaka 1890 ukiwa na eneo la 1.5 km.  Kati ya mwaka 1890 na 1906 mji uliendelea kupanuka na wakati huo huo ambapo uliojulikana kama miaka ya kuleta amani kwa sababu ya umuhimu wa sehemu hii kijeshi na kiserikali.

Meneja wa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Rish Urio anasema tamasha la Krismasi ni  siku mtambuka kwa waumini wa dini mbalimbali kwani ni sherehe  ya kuzaliwa Yesu Kristo, hivyo ni nafasi pekee kwa waumini kukutana na kufikisha neno la Mungu kwa njia ya nyimbo na mapambio.


Urio anasema waumini mbalimbali ni nafasi yao kupata ladha tofauti za nyimbo mbalimbali  kutoka kwa waimbaji wa ndani na nje ya Tanzania ambao wote kwa pamoja wanafikisha neno la Mungu kupitia nyimbo sambamba na amani kwa nchi majirani na Tanzania ambazo zitafikisha neno la Mungu.  

No comments:

Post a Comment

Pages