Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ameungana na viongozi wa mataifa mbali mbali duniani na maelfu ya
wananchi wa Afrika Kusini Kuadhimisha Kumbukumbu ya Kifo cha aliyekuwa kiongozi
mashuhuri wa Afrika Kusini na duniani, Mheshimiwa Nelson R Mandela.
Maelfu kwa maelfu
ya wananchi wamehimili mvua kubwa iliyokuwa inanyesha kwa nguvu kwenye Uwanja
wa Michezo wa FNB mjini Johannesburg kumwaga Mzee Mandela ambaye alikuwa ishara
kuu ya upinzani wa siasa za ubaguzi wa rangi za makaburu wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa
Mandela ambaye alifariki duniani Ijumaa iliyopita, Desemba 5, 2013, alikuwa
Kamanda wa Jeshi la Ukombozi la Chama cha African National Congress la Umkhoto
we Sizwe akafungwa jela kwa uhaini kwa miaka 27 na utawala wa Makaburu.
Baada ya kutoka
jela mwaka Februari 1990, Mzee Mandela alichaguliwa kuwa Rais wa Kwanza wa
Afrika Kusini ya mwaka 1994. Lakini Mheshimiwa Mandela alitumikia kipindi
kimoja tu cha miaka mitano na kukataa kutumikia kipindi cha pili.
Kiasi cha
viongozi 91 kutoka sehemu duniani wamehudhuria Kumbukumbu hiyo iliyokuwa na
kila aina ya mchanganyiko wa hisia – wengine wakiwa na majonzi na wengine
wakicheza na kuimba kwa muda wote wa shughuli hiyo iliyochukua kiasi cha jumla
ya saa tano.
Mbali na Rais
Kikwete ambaye amefuatana na Mama Salma Kikwete, marais wengine mashuhuri
duniani waliohudhuria Kumbukumbu hiyo ni Mheshimiwa Barack Obama wa Marekani,
Mheshimiwa Francois Hollande wa Ufaransa, Waziri Mkuu wa Uingereza, Mheshimiwa
David Cameroun na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Ban Ki Moon.
Kumbukumbu hiyo
pia ilihudhuriwa na viongozi wa zamani wa Marekani wakiwemo marais watatu wa
zamani wa Marekani – Mheshimiwa Jimmy Carter, Mheshimiwa Bill Clinton na
Mheshimiwa George W Bush na mawaziri wakuu wawili wa zamani wa Uingereza,
Mheshimiwa Tony Blair na Mheshimiwa Gordon Brown.
Rais Kikwete
kesho, Jumatano, Desemba 11, 2013, ataungana na viongozi wenzake katia katika
kutoa heshima za mwisho na kuuaga rasmi mwili wa Marehemu Mandela ambao
utawekwa kwenye Majengo ya Urais wa Afrika Kusini ya Union Buildings mjini Pretoria.
Kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais – Pretoria, Afrika Kusini
No comments:
Post a Comment