Umati wa wakimbiaji wa umbali wa Km. 21 wakianza mbio hizo jijini Dar es salaam leo. (Picha na Francis Dande)
Mshindi wa mbio za Uhuru
Marathon za Km. 42, Jamini Ikai kutoka Kenya akimaliza mbio hizo kwa kutumia
saa 2:33:35.
Mshindi wa pili wa mbio za Km. 42 kwa upande wa wanaume, Steven Silvester kutoka Tanzania akimaliza mbio hizo.
Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal akifuatilia kwa umakini mbio za Uhuru Marathon kwenye viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam. Kulia ni mratibu wa mbio hizo, Innocent Melleck na kushoto ni waziri wa habari, vijana, utamaduni na michezo Dk. Fenela Mukangara.
Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal akizungumza jambo na mratibu wa mbio hizo Innocent Melleck kwenye mashindano ya riadha ya mbio za Uhuru Marathon zilizofanyika kwenye viwanja vya leaders Club jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal akizungumza jambo na mratibu wa mbio hizo Innocent Melleck kwenye mashindano ya riadha ya mbio za Uhuru Marathon zilizofanyika kwenye viwanja vya leaders Club jijini Dar es Salaam.
Mshindi wa mbio za km 21 kwa wanawake, Jacqueline Sakilu ambaye ni mwajiri wa wa jeshi la wananchi wa Tanzania ambae ameshinda na kujinyakulia kiasi cha shilingi milioni moja.
Na Mwandishi Wetu
MBIO ndefu za Uhuru, Uhuru Marathon, zilifanyika jana kwa kuanzia na kumalizikia katika Viwanja vya Leaders vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam huku Watanzania na Wakenya wakichuana vilivyo na kugawana nafasi za ushindi.
Katika mbio za kilomita 42 upande wa wanaume mshindi alikuwa ni Jamini Ikai kutoka Kenya aliyetumia saa 2:33:35, akifuatiwa na Steven Sylvester wa Tanzania akitumia saa 2:42:05, nafasi ya tatu ilishikwa na Alex Sanka aliyetumia saa 2:44:14 toka Tanzania pia, akifuatiwa na James Shigela aliyetumia saa 2:47:40 na watano akiwa Getuni Gumali aliyekimbia saa 2:52:88.
Kwa upande wa wanawake nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Thabita Kibeti wa Kenya aliyekimbia saa 3:24:50, akifuatiwa na Naumi Jepkosgei wa Kenya pia aliyekimbia saa 3:45:09 na nafasi ya tatu ilitwaliwa na Banuelia Brighton wa Tanzania aliyekimbia saa 4:05:36.
Katika kilomita 21 upande wa wanaume nafasi ya kwanza na pili ilienda Kenya pale Elijah Tirop alipokimbia kwa saa 1:06:12, akifuatiwa na Wilson Tuitoe aliyekimbia saa 1:06:38, watatu akiwa Eliah Daudi wa Tanzania aliyetumia saa 1:07: 10, Hilary Kepchumba wa Kenya akishika nafasi ya nne kwa kukimbia saa 1:07: 12 na ya tano ikaenda kwa Wilbert Peter wa Tanzania aliyetumia saa 1:08:56.
Kwa upande wa wanawake nafasi ya kwanza ilikamatwa na Jacqueline Juma wa Tanzania aliyekimbia saa 1:15:25:06, Anjela Temu wa Kenya alitwaa nafasi ya pili kwa kukimbia saa 1:16:01:85, Catherine Range wa Tanzania alikimbia saa 1:17:33:82, Mary Mangegeia aliyekimbia saa 1:18:26:80 na Agnes Chepete akikimbia saa 1:23:21:85 wote hawa kutoka Tanzania.
Washindi wa mbio ndefu kwa upande wa mbio za kilomita 42 kwa upande wa wanaume na wanawake kila mmoja aliondoka na Sh milioni 2, kwa upande wa mbio za kilomita 21 kwa wanaume na wanawake kila mmoja alipata Sh milioni 1.
Mshindi wa pili kilomiita 21 kwa wanaume na wanawake walipata Sh 700,000 huku kilomita 42 wakiondoka na Sh milioni 1 kwa kila mmoja.
Mshindi wa tatu kilomita 21 kwa wanaume na wanawake kila mmoja alipata Sh 500,000 na kilomita 42 walipata Sh 600,000 washindi wa nne kwa kilomita 21 na 42 kwa wanawake na wanaume kila mmoja aliondoka na Sh 300,000 wakati yule aliyeshika nafasi ya tano kwa kilomita 21 wanawaume alipata Sh 150,000 na kilomita 42 ilikuwa Sh 200,000 huku walemavu kumi wakipata Sh 100,000.
Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal alisema, amefurahishwa mno na wazo la kuanzisha mbio hizo, ambalo ni kulinda na kudumisha Amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu, huku akionya wale wote wanaotaka kuleta chokochoko.
“Tanzania imesaidia sana kupigania uhuru wa nchi mbalimbali, hivyo hatuwezi kukubali eti sisi tugawanyike vipande hiyo haitakubalika na naamini vijana mnaona, mnasikia na kuwajua wanaoleta chokochoko hizo,” alisema, huku washiriki wakisimama pia kuomboleza kifo cha Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Awali, Katibu wa Kamati ya Mbio hizo, Innocent Melleck alitumia pia fursa hiyo kuiomba Serikali kuwasaidia zaidi, kwani mwakani wanataka kulisambaza katika mikoa mbalimbali ili kudumisha umoja wa Kitaifa.
“Mheshimiwa Makamu wa Rais mwakani ni miaka 50 ya Muungano tunatarajia kuanza maandalizi mapema na tutafanya uzinduzi rasmi Butiama mkoani Mara, ikiwa ni kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kasha tutafanya matamasha kama hayo katika kanda sita tofauti kabla ya kumalizia kwenye mbio za Uhuru tarehe 8 Desemba jijini Dar es Salaam, kwa umemwakilisha Mheshimiwa Rais, tunaomba utuwakilishie hili kwake ili tupate sapoti ya serikali katika jambo hili la kudumisha Amani na umoja wa kitaifa tuliorithishwa na waasisi wa taifa hili,” alisema Melleck.
Akijibu hilo, Makamu wa Rais alimwagiza Katibu Mkuu na Waziri mwenye dhamana ya michezo kuhakikisha hilo linatekelezeka.
Mbio za Uhuru zilidhaminiwa na GrandMalt, Konyagi, Kibuku, Mwananchi Communications, Sayona, CocaCola, KAPARI, Clouds FM, Uhuru FM, TBC 1, TBC Taifa, Integrated Communications, Night Support, Tindwa Medical, Forever Living na SamSung.
No comments:
Post a Comment