HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 07, 2014

MREMA AIGOMEA MANISPAA YA KINONDONI

Na Mwandishi Wetu

MGOGORO wa Manispaa ya Kinondoni Dar es Salaam, kugawa Eneo la Barabara ya Keko, Mikocheni ‘A’ Mtaa wa Tindiga kwa Kampuni ya Trans Auto Express Ltd, imeingia katika sura mpya.

Mgogoro huo umefikia hatua hiyo baada ya mmiliki wa Kampuni hiyo, kugomea amri ya Manispaa iliyomtaka kubomoa na kusitisha ujenzi katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa barua ya Manispaa ya Kinondoni iliyoandikwa na Mhandisi wa Manispaa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo ya Machi 28 mwaka huu, uongozi huo ulitoa Notice ya siku tatu, kwenda kwa Ephraem Mrema ikitoa amri kwa Kampuni ya Trans Auto Express Ltd, kutekeleza agizo hilo.

Sehemu ya barua hiyo ilimtaka mmiliki wa kampuni hiyo kuvunja ukuta uliojengwa kiwanja namba 269 na 272, ambao unaziba barabara inayoanzia nyuma ya shule ya Awali ya Feza, inayotokea kwa Rais Mstaafu Ally Hassan Mwinyi, pamoja na kubomoa structure zote zilizojengwa ndani ya eneo la Tindiga na kuifanya sehemu hiyo kubaki kama zamani.

Barua hiyo ili mwagiza Mrema ambaye aliwahi kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD), kuvunja kwa hiyari yake ujenzi huo, vinginevyo Manispaa itachukua jukumu la kuvunja kwa nguvu pamoja na uongozi wa kampuni hiyo, kupelekwa mahakamani ili kulipa fidia ya gharama zitakazojitokeza kutokana na ubomoaji huo.

Uchunguzi wa awali uliyofanywa mara baada ya maofisa wa Ardhi kutoka Manispaa ya Kinondoni kubandika tangazo, pamoja na kuweka alama za X katika kuta, mahali hapo, haikuchukua muda tangazo hilo liliondolewa kisha, ukuta kupigwa rangi ili kufuta alama za X na maandishi yaliyokuwa yakisomeka ‘bomoa’.

 Alipotafutwa kwa simu Mrema  ili kujibu madai ya kukaidi amri ya iliyomtaka kubomoa na kusitisha ujenzi katika eneo hilo, pia  kubandua tangazo na kufuta alama za X na maandishi Bomoa.

Mrema, alijibu kwa kifupi kuwa hajui  kitu chochote kinachoendelea na yupo nje ya mkoa wa Dar es Salaam.

“Sijui kitu chochote kuhusu suala hilo na mimi niko nje ya mkoa wa Dar es Salaam,” alisema Mrema na kukata simu.

Akizugumzia kitendo hicho Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Mussa Natty, alisema kuwa kama Mrema amefanya hivyo, ujumbe utakuwa umemfikia na kuahidi kulifuatilia suala hilo kwa kina kupitia mhandisi wa Manispaa, kujua ni hatua gani za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya mtu aliyefanya kosa hilo.

“Taratibu zetu kisheria zinatuelekeza kwamba kama kumebainika mtu yeyote kufanya ujenzi katika maeneo yasiyotakiwa kisheria na kutokufuata kanuni za mipango miji, hatua ya kwanza kutoa notice ambayo itaambatana na kupewa siku tatu ili aweze kutekeleza agizo hilo kwa hiyari yake,” Natty alisema.

Kwa mujibu wa wa taarifa zilizopo ndani ya manispaa hiyo, siku hizo tatu alizopewa Mrema zimekwisha na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi yake hadi sasa.

Kufuatia  Manispaa kutochukua hatua katika jambo hilo, inaamaanisha kuwa manispaa hiyo imekiuka sheria za Mipango Miji inayotaka kutekeleza agizo walilolitoa kuanzia siku ya mwisho ya notice.


Hata hivyo, imebaini kuwa uongozi wa Manispaa hiyo umeshindwa kutekeleza agizo la notice hiyo kwa kile kinachodaiwa kuwa ni vitisho vinavyotolewa na Mrema kuwa kampuni hiyo ina hisa na vigogo wa  Ikulu.

No comments:

Post a Comment

Pages