HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 07, 2014

NGORONGORO HEROES KUREJEA LEO
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngongoro Heroes) inarejea nchini leo (Aprili 7 mwaka huu) kutoka Kenya ambapo jana (Aprili 6 mwaka huu) ilicheza mechi ya michuano ya Afrika.

Ngorongoro Heroes ambayo itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 8.25 mchana kwa ndege ya Kenya Airways ilitoka suluhu na wenye Kenya katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kanyetta uliopo mji wa Machakos.

Timu hizo zitarudiana jijini Dar es Salaam wiki tatu baadaye ambapo itakayofuzu itacheza raundi ya pili dhidi ya Afrika Kusini. Fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 zitachezwa mwakani nchini Senegal.

TIMU YA WATOTO WA MITAANI YATWAA UBINGWA WA DUNIA
Timu ya Taifa ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania imetwaa ubingwa wa Dunia wa Watoto wa Mitaani baada ya jana (Aprili 6 mwaka huu) kuilaza Burundi mabao 3-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa jijini Rio de Janeiro, Brazil.

Mshambuliaji Frank William alifunga mabao matatu katika mechi hiyo iliyochezwa uwanja mkongwe na maarufu wa klabu ya Fluminense huku mgeni rasmi akiwa Waziri wa Fedha wa Uingereza, George Osborne.

Tanzania ilipata tiketi ya kucheza fainali baada ya kuitandika Marekani mabao 6-1 ambapo hadi mapumziko ilikuwa mbele kwa mabao 4-0.

Burundi ilipata tiketi ya kucheza fainali baada ya kuifunga Pakistan mabao 4-3 katika mechi ya nusu fainali ya pili.

Timu ya Tanzania inarejea nchini Alhamisi (Aprili 10 mwaka huu) ambapo itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 10 jioni kwa ndege ya Emirates.

BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO

SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages