Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Salum Mayanga ametangaza majina ya wachezaji 16 waliochaguliwa katika maboresho ya timu ya Taifa Taifa Stars kwenye hoteli ya Hill View jijini Mbeya.
Wachezaji hao ni kipa Benedicto Tinoko Simwanda (Temeke), mabeki wa kati; Emma Namwondo Simwanda (Temeke) na Joram Nason Mgeveje (Iringa). Walinzi wa pembeni ni Omari Ally Kindamba (Temeke), Edward Peter Mayunga (Kaskazini Pemba) na Shiraz Abdallah Sozigwa (Ilala).
Viungo ni Yusuf Suleiman Mlipili (Temeke), Said Juma Ally (Mjini Magharibi), Abubakar Ally Mohamed (Kusini Unguja), Hashim Ramadhan Magona (Shinyanga), Omari Athumani Nyenje (Mtwara) na Chunga Said Zito (Manyara).
Washambuliaji ni Mohammed Seif Saidi (Kusini Pemba), Ayoub Kasim Lipati (Ilala), Abdurahman Othman Ally (Mjini Magharibi), Paul Michael Bundara (Ilala). Wachezaji wa U 20 ni Mbwana Mshindo Musa (Tanga) na Bayaga Atanas Fabian (Mbeya).
Alisema mpango huu wa kuboresha timu ya Taifa ambayo inadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ni endelevu na kusisitiza kuwa hata wale 18 walioachwa watafuatiliwa na TFF na kuitwa panapokuwa na mahitaji.
“Hawa wote wapo kwenye database ya TFF na hawataachwa tu hivi hivi wapotee,” alisema kocha Mayanga.
Wachezaji ha0 waliingia kambini mjini Tukuyu, Machi 21 mwaka huu na wamefanya mazoezi kwa pamoja kwa karibu wiki nne sasa kabla ya kuchujwa.
Wachezaji 16 waliochaguliwa wanatarajiwa kuondoka Tukuyu kesho (Aprili 18 mwaka huu) na kwenda kwenye kambi ya Taifa Stars katika Hoteli ya Kunduchi ambapo wataungana na wachezaji wa Taifa Stars wa siku zote.
Baadaye watachujwa tena ili ipatikane timu moja ya Taifa iliyoboreshwa.
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjro Premium Lager inaunga mkono utaratibu huu wa maboresho ya Taifa na imewekeza zaidi ya dola milioni 2 kwa mwaka kudhamini Taifa Stars. Huu ndio udhamini mkubwa zaidi ambao Stars imewahi kupata tangu kuanzishwa kwa TFF.
LIGI YA MABINGWA WA MIKOA KUANZA MEI 10
Michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) itakayochezwa kwa ligi ya mkondo mmoja katika vituo vitatu vya timu tisa kila kimoja inatarajia kuanza Mei 10 mwaka huu.
Timu ya kwanza kutoka katika kila kituo ndiyo itakayopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2014/2015. Kwa vile ligi hii haina mdhamini, hivyo timu zitajigharamia kwa kila kitu.
Vituo vitakavyotumika kwa ajili ya RCL, kanuni pamoja na ratiba vitatangazwa kabla ya kuanza kwa ligi hiyo. Pia kituo kitakachoteuliwa kwa ajili ya ligi hiyo, timu yake haitapangwa katika kituo husika ikiwa ni moja ya njia ya kuhakikisha kanuni ya mchezo wa kiungwana (fair play) inazingatiwa.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment