Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandhi wa habari jijini Dar es salaam kuhusu mchakato wa upigaji kura za wasanii wa Kilimajaro Music Award.
Na Clezencia Tryphone
WAKATI Tuzo za wasanii za Kilimanjaro Music Award
zikitarajiwa kutimua vumbi Mei 3 mwaka huu, wadau wa muziki nchini wametakiwa
kuitumia vema wiki ya mwisho ya upigaji kura katika kinyang’anyiro hicho cha (KTMA
2014).
Lengo kubwa la kuwataka wadau kupiga kura hasa wiki hii ni kuwawezesha
wasanii, bendi na wateule wengine kushinda ili waweze kufanikiwa kupata tuzo
katika ‘Usiku wa Tuzo’ utakaotimua vumbi katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa Meneja wa Bia ya Kilimanjaro ambao ni
wadhamini wakuu wa shindano hilo, kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa
(Basata), George Kavishe, mchakato umeenda vizuri tangu Aprili Mosi ulipoanza
hadi sasa, ambako majaji watatumia wiki hii kutoa asilimia zao 30.
“Kuna asilimia 70 ya kura za wadau zinaendelea kupokelewa,
lakini pia majaji nao wataitumia wiki hii kufanikisha asilimia 30 ya maamuzi
yao kwa wateule. Tunawasisitiza mashabiki wahakikishe wanatumia fursa
iliyosalia ili kufanikisha ushindi kwa wasanii/vikundi wavipendavyo,” alisema
Kavishe.
Aliongeza kuwa, mchakato huo uko chini ya majaji waliobobea 15
wanaoufahamu vema muziki, ambao baadhi yao ni waalimu na wanamuziki mahiri,
hivyo haki itatendeka na washindi wa kweli watapatikana.
Alisema, anaimani kubwa na majaji hao kwani hakuna mtu
anayemfahamu jaji mpaka sasa, na kama kuna mtu anahitaji kuwatambua majaji
anaweza kuwaona na kutoa sababu maalumu ya kutaka kuwafahamu majaji hao na wao
kumpatia orodha nzima.
Huku Mwakilishi wa Kampuni ya Auditax, Straton Makundi,
alibainisha kuwa, lengo la kuwepo kwa majaji hao katika mchakato huo ni
kusimamia haki katika mchakato, kutoa miongozo ya upigaji kura, kutunza
kumbukumbu na kuhesabu kura zote.
No comments:
Post a Comment