HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 21, 2014

TANESCO KUTATUA KERO ZA WANANCHI
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Umeme (TANESCO), Felchesmi Mramba, amewataka wafanyakazi kutumia vema mafunzo wanayopata katika chuo cha shirika hilo, yawe chachu ya kuimarisha miundombinu ili kuondoa tatizo la kukatika katika kwa umeme.

Kauli hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam juzi, wakati alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari kuhusu jitihada za shirika hilo za kuanzisha chuo hicho ambako awali hawakua nacho.

Mramba, alisema wafanyakazi hao wanapaswa kujua mafunzo hayo wanayopata ni kwa ajili ya kuwajengea uwezo ambao watalazimika kuutumia katika kuboresha huduma za shirika hilo, ili liweze kuaminika zaidi na wadau wa huduma hiyo.

Aliyataja mafunzo yanayotolewa katika chuo hicho kuwa ni ya mafundi mchundo, mafundi sadifu na mwengine ambako yanatolewa kwa muda wa miezi mitatu.

“Tunajua kuwa kuendesha mafunzo ni gharama lakini shirika limejipanga katika kuhakikisha kwamba linawapatia mafunzo wafanyakazi wake wote ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ueledi na maarifa zaidi,”alisema Mramba.

Mramba alisema mafunzo hayo yanaendeshwa kwa ushirikiano wa serikali ya Tanzania na Japani kupitia (JICA), ambayo imekua ikichangia wataalamu na vifaa kwa sehemu kubwa katika chuo hicho.

Muakilishi wa JICA, Yasunori Onishi, alisema, wanatambua jitihada za serikali  ndio maana wakaamua kushirikiana nayo katika mradi huo wa mafunzo, ambayo anaamini yatasaidia kuboresha kiwango cha uzalishaji wa huduma hiyo ya umeme nchini.

Henry Sanga ambaye ni mfanyakazi wa TANESCO, alisema mafunzo hayo yameweza kuleta mageuzi makubwa kiutendaji kwani awali hawakua na uwezo wa kutambua mara moja kwa mfano kujua mkoa wa Dar es Salaam una nguzo ngapi.

Aliongeza kuwa baada ya kuanzishwa mafunzo hayo, hivi sasa mafundi hao wanao uwezo wa kutambua hususan kutumia vifaa hivyo walivyoletewa na Wajapan hao, hivyo kuliomba shirika liendelee na utaratibu huo kwani unasaidia kukuza maarifa ya wafanyakazi wake.

No comments:

Post a Comment

Pages