Na Lucy Ngowi
POSTAMASTA Mkuu wa
Shirika la Posta Tanzania, Deos Mndeme amesema kuwa, amepokea risala ya
wafanyakazi hivyo atafanyia kazi masuala yaliyomo kwa kuzingatia sheria, kanuni
na taratibu ili kudumisha utawala bora.
Mndeme alisema hayo
alipokuwa akipokea maandamano ya wafanyakazi wa Makao Makuu na Mkoa wa Dar es
Salaam ya kuadhimisha siku ya wafanyakazi duniani.
Alisema anaamini kuwa
uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu ni msingi imara katika kutekeleza
kauli mbiu ya Mei Mosi mwaka huu inayosema, ‘ utawala bora utumike kutatua kero
za wafanyakazi,’.
“Nawasihi wafanyakazi na
viongozi wa ngazi zote tuendeleze ushirikiano na mshikamano katika kuitekeleza
kwa vitendo kaulimbiu ya mwaka huu,” alisema Mndeme.
Awali, Mjumbe wa Chama
cha Wafanyakazi wa Mawasiliano (Teuta), Edwin Tibanywana alisema kuwa,
wafanyakazi wanafanya kazi katika hali ngumu inayochangiwa na maslahi duni,
hivyo imekuwa ni kichocheo kikubwa cha kuwanyima hamasa ya kufanya kazi.
“Mishahara ni duni
haiendani na maisha ya binadamu kwa sasa,” alisema na kuongeza kuwa, wakati
wafanyakazi wa chini wanataabika wakubwa wanaweka mipango thabiti ya maisha
yao.
Alisema kuwa, shirika
hilo lina majengo mengi ambayo kuna wapangaji lakini hakuna juhudi
binafsi za kukusanya kodi hali inayolirudisha nyuma.
No comments:
Post a Comment