Baada ya kutafakari kwa uangalifu na kwa umakini
mkubwa kuhusu chanzo halisi cha hoja yenyewe ya kutaka kumuondoa Spika wa EALA
madarakani, tuligundua mambo yafuatavyo:
1. Hoja
hii haina maslahi ya Tanzania na iko kinyume na malengo ya ushirikiano ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC). Tumebaini kuwa hoja yenyewe ni sehemu ya "mchezo mchafu" wa ajenda ya siri ya
kujaribu kuweka mbele maslahi ya baadhi ya wanachama wachache wa jumuiya badala
ya kuzingatia maslahi mapana ya EAC.
2. Tuhuma
mbalimbali zilizotajwa dhidi ya Spika wa EALA kuhusu yeye kuonesha upendeleaji,
ujeuri na mapungufu mengine ya uongozi zimegundulika kuwa hazina mashiko na wala
mantiki .
3. Kitendo
ambacho kimetushtua ni kuwa kumekuwa na majaribio kadhaa ya baadhi ya Wabunge
wa EALA kutoka nje ya Tanzania na viongozi wa Sekretarieti ya EAC kutaka
kulazimisha sahihi za baadhi ya Wabunge wa Tanzania zitumike kinyume na
utaratibu kuunga mkongo Azimio tajwa (kitu ambacho tunakipinga kwa nguvu zote).
Hii inadhihirisha kuwepo kwa ajenda ya siri katika sakata hilo dhidi ya maslahi
ya Tanzania na jumuiya kwa ujumla.
4. Kufuatia malumbano yaliyoibuka katika kikao
cha Bunge cha mwezi Machi huko Arusha, sisi Wabunge wa Tanzania tulipokea maoni
na masikitiko mengi kutoka kwa wana Afrika Mashariki na viongozi kwa ujumla
wakitusihi kumaliza tatizo hili kwa njia ya amani na utulivu, lakini jitihada
zetu ziligonga ukuta. Hatua hii ilizidi kutudhihirisha kuwepo kwa ajenda ya
siri.
Ikumbukwe kuwa azimio la kutaka kumuondoa
Spika madarakani awali lilipangiwa kuwasilishwa katika kikao cha Bunge la EALA
cha mwezi Machi 2014 huko Arusha lakini liligonga mwamba baada ya kuibuka
mabishano ya kisheria, hali iliyopelekea kuahirishwa kwa kikao hicho.
Hoja hii ililetwa tena kwenye vikao vingine
vya EALA, lakini baada ya kutafakari kwa makini kuhusu chanzo halisi cha mzozo
huu, idadi kubwa ya Wabunge kutoka Tanzania (7 kati ya 9) waliamua kwa pamoja
kuipinga hoja hii kwani imekosa mashiko na haizingatii maslahi ya Tanzania na
maslahi mapana ya jumuiya kwa ujumla.
Aidha, wabunge watatu wa EALA kutoka
Tanzania ambao awali waliunga mkono hoja hii waliamua baadae kuipinga kwa kutoa
sahihi zao kwa hiari yao wenyewe na walimwandikia barua Katibu wa Bunge wa EALA
kumueleza maamuzi yao kwa mujibu wa utaratibu mnamo tarehe 29 Mei 2014. Barua
hizo za Wabunge wa Tanzania wa EALA kutoa sahihi zao kwenye hoja hiyo zilipokelewa
rasmi na Katibu wa Bunge.
Wabunge hao wa EALA kutoka Tanzania
walitumia haki zao za kikanuni kuondoa sahihi zao kama inavyoeleza katika
kanuni ya 9 (2) ya Kanuni na Utaratibu wa Uendeshaji wa Bunge (Rules of
Procedure of the Assembly) inayosema: "Azimio la kumuondoa Spika
madarakani halina budi kuambatana na sahihi zisizopungua nne kutoka kila nchi
mwanachama."
Hoja yenyewe ya kumuengua Spika wa EALA ni
batili kisheria kwa kuwa haikuwasilishwa Bungeni ndani ya siku 7 tangu
ilipopelekwa kwa Katibu wa Bunge na pia imekosa sahihi za kuungwa mkono na
wabunge wanne kutoka kila nchi mwanachama wa EAC kama kanuni zinavyotamka.
Uamuzi wa Wabunge wa EALA kutoka Tanzania
kuondoa sahihi zao kwenye hoja hiyo ni lazima uheshimiwe na kila mtu kwa kuwa
wanatekeleza haki yao ya kidemokrasia.
Tunaomba uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
kwa ngazi zote ikiwemo Sekretarieti ya jumuiya kuheshimu maamuzi ya Wabunge wa
EALA kutoka Tanzania. Ikumbukwe kuwa hapo awali, wabunge wa 5 wa EALA kutoka
Tanzania kati ya jumla ya wabunge wote 9 wa Tanzania walionesha kuunga mkono
hoja hii. Baada ya kubaini kuwepo kwa “mchezo
mchafu” na ajenda ya siri, Wabunge watatu wa EALA kutoka Tanzania waliondoa
sahihi zao na hivyo basi kufanya idadi kubwa ya Wabunge kutoka Tanzania (7 kati
ya 9) kuipinga hoja hii batili.
Wabunge wa EALA wameshapoteza muda mwingi,
fedha na rasilimali nyingine mpaka sasa kwenye hoja hii isiyo na tija ya
kujaribu kumng'oa madarakani Spika wa EALA. Sasa hatuna budi kuweka jitihada
zetu kwenye kazi muhimu ya kutetea maslahi ya raia wapatao milioni 140 wa
Afrika Mashariki.
Hatuwezi kuwahudumia raia wa Afrika
Mashariki kwa kuweka mbele ajenda za siri na kujishughulisha kwenye siasa za
malumbano. Wananchi wa Afrika Mashariki wanataka kuona faida halisi kutoka
kwenye jumuiya yao. Tuna imani na Spika wa sasa wa Bunge la EALA kuwa ni
kiongozi sahihi wa kuongoza Bunge hilo.
Tunaamini kuwa hakuna tija yoyote kwa
Wabunge wa EALA kuendelea kupoteza fedha za walipa kodi wa Afrika Mashariki kwa
kujadili hoja hii batili. Badala yake, Wabunge wa EALA wana kazi ngumu ya
kusimamia maslahi ya wananchi wa jumuiya wanaotaka kupata elimu bora, maji safi
na salama ya kunywa, uhakika wa chakula, afya bora, miundombinu ya kisasa na
maendeleo ya kiuchumi -- siyo siasa za ulaghai.
Tunatoa wito pia kwa Wabunge wenzetu wa
EALA kutoka nchi nyingine wanachama na kwa viongozi wa Sekreterieti ya EAC
kutojihusisha na ajenda zozote za siri za kujaribu kumng'oa Spika wa sasa wa
EALA aliyepo madarakani kisheria. Wananchi wa Afrika Mashariki wanastahili
zaidi ya hayo.
Njia pekee ya kufikia maslahi yetu ya
pamoja ni kwa kutumia ushirikiano, badala ya kuendekeza malumbano na siasa za chuki
na kututenganisha. Sisi Wabunge saba
bado tunasisitizia AMANI NA UTULIVU kwani bila ya hivyo hakuna maendeleo na
ustawi wa jamii.
Tamko hili limetolewa Dar es Salaam tarehe
9 Juni 2014 na Wabunge wafuatao:
Mhe. Adam Kimbisa, Mwenyekiti wa Wabunge wa
EALA wa Tanzania
Mhe. Shy-rose Bhanji, Katibu wa Wabunge wa
EALA wa Tanzania
Mhe. Charles Makongoro Nyerere, Mbunge wa
EALA
Mhe. Maryam Ussi, Mbunge wa EALA
Mhe. Bernard Murunya, Mbunge wa EALA
Mhe. Twaha Taslima, Mbunge wa EALA
Mhe. Angellah Kizigha, Mbunge wa EALA
Mwenyekiti wa Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) wa Tanzania, Adam Kimbisa, akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu sakata la kutaka kumvua madaraka Spika wa Bunge hilo. Kulia ni mbunge wa bunge hilo, Twaha Taslima na Katibu wa Wabunge wa EALA, Shy-Rose Bhanji.
Katibu wa Wabunge wa EALA, Shy-Rose Bhanji akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu sakata la kutaka kumvua madaraka Spika wa Bunge hilo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) wa Tanzania, Adam Kimbisa na mbunge wa bunge hilo, Twaha Taslima.Mbunge wa bunge hilo, Twaha Taslima akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini dar es Salaam leo.Wabunge wa Jumiya ya AfrikaMashariki (EALA), wakitoka katika ukumbi wa Idara ya Habari jijini Dar es Salaam, baada ya mkutano wao na waandishi wa habari. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Wabunge wa Jumuiya hiyo kutoka Tanzana, Adam Kimbisa, Katibu wa Wabunge wa EALA, Shy-Rose Bhanji (katikati) na mbunge wa bunge hilo Twaha Taslima.
Mwenyekiti wa Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) wa Tanzania, Adam Kimbisa, akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu sakata la kutaka kumvua madaraka Spika wa Bunge hilo. Kulia ni mbunge wa bunge hilo, Twaha Taslima na Katibu wa Wabunge wa EALA, Shy-Rose Bhanji.
Katibu wa Wabunge wa EALA, Shy-Rose Bhanji akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuhusu sakata la kutaka kumvua madaraka Spika wa Bunge hilo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) wa Tanzania, Adam Kimbisa na mbunge wa bunge hilo, Twaha Taslima.Mbunge wa bunge hilo, Twaha Taslima akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini dar es Salaam leo.Wabunge wa Jumiya ya AfrikaMashariki (EALA), wakitoka katika ukumbi wa Idara ya Habari jijini Dar es Salaam, baada ya mkutano wao na waandishi wa habari. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Wabunge wa Jumuiya hiyo kutoka Tanzana, Adam Kimbisa, Katibu wa Wabunge wa EALA, Shy-Rose Bhanji (katikati) na mbunge wa bunge hilo Twaha Taslima.
No comments:
Post a Comment