HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 24, 2014

TAMASHA LA MICHEZO YA MAJESHI YA NCHI ZA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI, ZANZIBAR TANZANIA

Mzunguko wa nane wa tamasha la michezo ya Majeshi na Utamaduni kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki imefunguliwa rasmi tarehe 20 Augusti 2014  na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe.  Balozi Ally Seif Iddi  katika Uwanja wa Amaan mjini Unguja.Kaulimbiu ya michezo hii ni Jamii Moja, Hatma moja kupitia Michezo ya Majeshi na Utamaduni 2014,ambapo nchi shiriki ni wenyeji Tanzania,Burundi,Kenya,Rwanda na Uganda.
 
Washiriki wa Tamasha hilo ambao ni nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki walipita mbele ya mgeni rasmi kwa gwaride maalum na kutoa heshima wakiwa wamebeba bendera za mataifa ya nchi zao, huku wakishangiliwa na maelfu ya watazamaji waliofurika uwanjani hapo.
 
Sherehe hizo za ufunguzi pia zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki  pamoja na Mkuu wa Majeshi wa Tanzania Jenerali Davis Aldolf Mwamunyange pamoja na wawakilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
 
Katika ufunguzi huo mgeni rasmi alisema lengo la michezo hii ni kuyaweka pamoja majeshi ya nchi za jumuia ya Afrika mashariki ikiwa na dhana ya kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa majeshi haya.Mgeni rasmi aliwataka pia wanamichezo wote kuzingatia nidhamu ndani na nje ya viwanja vya michezo.
Aliongeza kuwa kupitia michezo hii tutaweza kuijenga jumuiya tunayoitaka kwa uthamani wake na umuhimu wake,tunataka kuendelea kuijenga jumuia itakayokuwa ikijali ustawi wa jamii iliyo ndani na nje ya jumuiya ili hatimaye nchi zetu ziwe sehemu salama kwa ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.
 
 
Baada ya nasaha hizo ulifuata mchezo wa mpira wa miguu kati ya Tanzania na Burundi ambapo Tanzania lishinda magoli 3 -1 magoli ya JWTZ yakifungwa na Aidani Michael katika dakika ya 13,goli la pili likifungwa na Abdalah Mussa katika dakika ya 25 na Amosi Mgisa akifunga goli la tatu katika dakika za nyongeza.Na goli la Burundi likifungwa na Francis katika dakika ya 45 kipindi cha kwanza.
 
Siku ya Alhamisi tarehe 21 August 2014  kulifanyika michezo saba, ambapo Tanzania ilicheza michezo miwili, mchezo wa pete Tanzania ilicheza na Burundi katika uwanja wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) na kushinda magoli 113- 10 na katika uwanja wa Gymkhana kulikuwa na mchezo wa mpira wa Kikapu  Tanzania na Rwanda  na JWTZ kushinda mchezo huo kwa magoli 67 – 56.
 
Siku ya Ijumaa tarehe 22 Agosti  2014 kulifanyika michezo saba, katika uwanja wa Amaan JWTZ (Tanzania) ilicheza na Rwanda na kupata ushindi wa magoli 2-0, na katika mpira wa pete Tanzania ilimenyana na Rwanda na kushinda kwa kishindo kwa magoli 95- 12, aidha katika uwanja wa Gymkhana Tanzania ilicheza na Burundi katika mpira wa kikapu na kushinda magoli 54-51 na katika uwanja wa Migombani Tanzania ilicheza na Kenya na kupoteza mchezo huo kwa kufungwa magoli 26- 20.
 
Siku ya Jumamosi Augusti 24 kulifanyika mbio za nyika kwa wanaume kilometa 12 na wanawake kilometa 8. Praiveti Ismail Juma wa JWTZ (Tanzania) aliweza  kuibuka mshindi wa kwanza baada ya kukimbia  kwa muda wa dakika 36;49;33 akifutiwa na koplo Kipimo Kimutai wa Kenya aliyetumia mda wa dakika 37;12;06 huku mshindi wa tatu akiwa Muhitila Felisiani wa Rwanda akitumia dakika 37;20;17.
 
Katika mbio za nyika kilometa 8 wanawake  Kenya ilifanikiwa kushika nafasi zote tatu za juu huku praiveti Jackline Sakilu wa Tanzania akishika nafasi ya nne, na katika uwanja wa migombani ulifanyika mpira wa mikono  kati ya Tanzania na Burundi na Tanzania kushinda kwa magoli 25 -20. Michezo hiyo itaendelea siku ya Jumatatu tarehe 25 Agosti 2014 katika viwanja mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Pages