HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 09, 2014

KIINGILIO MECHI YA NGAO YA JAMII 5,000

Kiingilio cha chini kwenye mechi ya Ngao ya Jamii kuashiria uzinduzi wa msimu mpya wa Ligi kati ya Azam na Yanga itakayochezwa Jumapili (Septemba 14 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000.

Mechi hiyo itaanza saa 10 kamili jioni, na kiingilio hicho cha sh. 5,000 ni kwa viti vya rangi ya kijani na bluu vitakavyochukua jumla ya watazamaji 36,000 katika uwanja huo wenye viti 57,558.

Viingilio vingine katika mechi hiyo ambayo itatumia tiketi za elektroniki ni sh. 10,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 20,000 kwa viti vya VIP C na B wakati viti vya VIP A kiingilio ni sh. 30,000.

MWAMUZI LUGENGE KUAGWA LEO
Mwamuzi wa daraja la kwanza (class one), Luteni Godwill David Lugenge aliyefariki dunia juzi (Septemba 7 mwaka huu) kwa ajali ya gari katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga anaagwa leo (Septemba 9 mwaka huu).

Mwili wa marehemu ambao umehifadhiwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi (GMH) Lugalo, baadaye leo saa 6 mchana utapelekwa nyumbani kwa kaka yake Kimara Bucha jijini Dar es Salaam ambapo shughuli za kuaga zitafanyika kabla ya safari ya kwenda mkoani Njombe kwa ajili ya mazishi.

Luteni Lugenge ambaye mwishoni mwa wiki alishiriki mitihani ya utimamu wa mwili kwa waamuzi wa Ligi Kuu, akiwa na ndugu yake Christopher Alexander Lunyungu katika gari dogo walipata ajali hiyo wakati wakienda mkoani Kilimanjaro.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambalo limetoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kwenye shughuli ya kuaga itawakilishwa na mjumbe wake wa Kamati ya Utendaji ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Saloum Umande Chama.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Luteni Lugenge, Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu nchini (FRAT) na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Bwana ametoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe


BONIFACE WAMBURA
KNY KATIBU MKUU
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages