Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameuagiza Uongozi wa Wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali Pemba kufuatilia na kuhakikisha kamati za skuli zinazoundwa zinazingatia sifa na vigezo vya kusimamia maendeleo ya skuli.
Ameyasema hayo katika hafla ya ugawaji wa zawadi kwa wananfunzi waliofaulu mchipuo na vipawa katika jimbo la kiwani kwa mwaka wa mosomo 2025/2026 hafla iliyofanyika katika skuli ya sekondari Kiwani, Mkoa wa Kusini Pemba.
Amesema kamati za skuli zinazoundwa ni lazima ziwe na wajumbe wenye sifa, vigezo, utayari na uzalendo wa kujitoa katika kufuatilia maendeleo ya skuli na kutatua changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika skuli kwa maslahi mapana ya wanafunzi.
Mhe. Hemed amewataka walimu wakuu wa skuli za kiwani kushirikiana na kukaa pamoja katika kujadili namna ya kupata mafanikio zaidi katika sekta ya elimu ili skuli zote ziweze kufaulisha kwa viwango vya juuu.
Amefahamisha kuwa mkakati wa viongozi wa Jimbo la Kiwani ni kujikita zaidi katika kuimarisha skuli za msingi ili kuwajengea wanafunzi uwezo na uelewa zaidi na kuwa Imara wanapofikia ngazi ya sekondari na vyuo vikuuu.
Aidha, amesema kwa kushirikiana na viongozi wenzake wataendelea kutatua changamoto zinazowakabili walimu ikiwemo uhaba wa walimu na kuziangali stahiki zao ili kutoa motisha kwa walimu hao waweze kusomesha kwa moyo thabiti utakaotoa matokeo chanya kwa wananfunzi hao.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ndugu Mohammed Nassor Salim amesema Serikali ya Awamu ya nane inaendelea kuboresha na kuimarisha miundombinu ya elimu kwa kujengwa skuli za kisasa zenye kukidhi mahitaji yote ya kufundishia na kujisomea jambo litakalochangia kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu nchini.
Amewaomba walimu wakuu kuzipitia upya kamati zao za skuli kwa kuangalia changamoto, vikwazo na uhitaji ili ziweze kufanya kazi kwa karibu na jamii sambamba na kutimiza malengo ya kukuza na kuimarisha sekta ya elimu.
Nae Mbunge wa Jimbo la kiwani Mhe. Hija Hassan Hija amesema katika Uongozi wao wamekubaliana kuwa kipaombele cha kwanza ni sekta ya elimu ili kuhakikisha wanakuza na kuimarisha sekta ya elimu jimboni humo kwa kuziondoa changamo zinazowakabili walimu na wanafunzi wa skuli za kiwani.
Mhe. Hija amesema Uongozi wa Jimbo la Kiwani umejipanga kukutana na kufanya mazungumzo na walimu wote waliomo jimboni humo ili kujadili kwa kina namna bora ya kukuza ufaulu kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya msingi hadi Sekondari.
Akizungumza kwa niaba ya walimu wakuu wa skuli zote za kiwani, Mwalimu Mkuu wa skuli ya Chanjaani Msingi Mwalimu Omar Juma Said amesema Serikali ya awamu ya nane imefanikisha kutatua changamoto ya kuingia skuli kwa mikondo mitatu pamoja na kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na sasa wanafunzi wanaingia mkondo mmoja wa masomo kwa idadi a wanafunzi 45 kwa kila daradani.
Mwalim Omar memshukuru mwakilishi wa jimbo la kiwani Mhe. Hemed Suleiman Abdulla pamoja na viongozi wenzake kwa kuendelea kulipa kipaombele jimbo la kiwani katika sekta ya elimu kwa kuziondoa changamoto nyingi zilizokuwa zikiikabili sekta hio ikiwemo kuwasaidi wanafunzi wanaoishi dakhalia, kutoa Photocopy Mashine kwa skuli zote za Kiwani pamoja na kuwapatia vifaa vyote vya kusomea wanafunzi waliofaulu mchipuo na vipawa.
Nao Wanafunzi walipatiwa zawadi hizo wameushukuru Uongozi wa jimbo la Kiwani kwa moyo wao wa upendo kwao na kujali juhudi walizochukua ili kuhakikisha wanafaulu kwa viwango vya juu jambo ambalo litazidisha ari na hamasa hasa kwa wanafunzi wanaongidia darada la saba na wanaotarajiwa kufanya mitihani yao ya Taifa katika ngazi mbali mbali.
Wamewaahudi viongozi hao na familia zao kuwa watasoma kwa bidii na ari kubwa ili kuweza kufikia malengo waliojiwekea hususan ya kuja kuwatumikia wananchi wa kiwani kupitia taaluma zao.
Katika hafla hio Mwakilishi wa jimbo la Kiwani kwa niaba ya viongozi wenzake waliwazawadia wanafunzi waliofaulu mchipuo na vipawa sare za skuli, viatu, mikoba ya skuli, viafa mbali mbali vya kusomea na fedha taslimu kwa ajili ya maandalizi mengine yatakayohitajika katika masomo yao.


No comments:
Post a Comment