Na Mwandishi Wetu, HANDENI
KIKUNDI cha ngoma cha selo kilichopo katika kijiji cha
Kweingoma, wilayani Handeni, mkoani Tanga, kimesema kimepania vikali Desemba 13
mwaka huu kufanya balaa katika tamasha la Handeni Kwetu 2014, litakalofanyika
wilayani hapa.
Shauku ya kikundi hicho imetolewa na Kiongozi wao Zaina
Selemani, alipozungumzia umuhimu wa tamasha hilo, ambalo mwaka jana walishindwa
kushiriki kutokana na wasanii wake wengi kukabiliwa na mambo ya kifamilia,
ikiwamo kuugua na kuuguliwa.
Akizungumza kwa furaha kubwa, Zaina alisema ngoma ya selo ni
nzuri inayoshawishi kuangalia wasanii wanapokuwa jukwaani, hivyo mashabiki na
wadau wote watapata burudani nzuri.
“Mwaka huu tutashiriki kwa nguvu zote kwasababu ni tamasha
lililoanza vizuri kwa mkoa huu wa Tanga, maana vikundi vingi kutoka sehemu
mbalimbali za Handeni na mkoa wa Tanga vinashiriki,” alisema.
Naye Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema kuwa
kwa siku kadhaa walikuwa wakifanya ziara kadhaa katika vijiji ambavyo vina
vikundi vya ngoma za asili ili vishiriki, hususan vile ambavyo mwaka jana
havikushiriki.
“Tunataka kuongeza wigo wa vikundi kutoka ndani ya Tanga na
nje pia, ukizingatia kuwa tunahitaji tamasha lenye nguvu na mguso pia ili
kukuza sekta ya utamaduni na uchumi wa nchi yetu,” alisema Mbwana.
Tamasha la Handeni Kwetu lililopangwa kufanyika Desemba 13
katika Uwanja wa Azimio (Kigoda Stadium), ni moja ya matukio makubwa mkoani
Tanga yanayokutanisha mamia ya watu kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania.
No comments:
Post a Comment