HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 28, 2014

NBS YAWATAKA WADAU WA MAENDELEO KUTUMIA KANZA KATIKA KUTOA TAKWIMU ZA KILIMO

Na Mwandishi Wetu

OFISI ya Taifa ya Takwimu imewataka watunga Sera, taasisi, mashirika, na wadau mbalimbali wa maendeleo kuitumia Kanza  (Data base), rasmi ya takwimu za Chakula na Kilimo iliyoanzishwa kwa lengo la kutoa takwimu za Kilimo kutoka katika maeneo mbalimbali.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu wakati wa ufunguzi wa semina ya kuhamasisha matumizi ya Kanza hiyo jijini Dar es salaam, Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu wa ofisi hiyo, Gabriel Madembwe amesema upatikanaji wa taarifa za sekta ya Kilimo na Chakula kutoka katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji hapa nchini umerahisishwa kupitia Kanza hiyo inayopatikana kupitia tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya www.nbs.go.tz

Alisema takwimu zilizo katika Kanza hiyo zitaiwezesha serikali, watunga sera na wadau mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi kufanya maamuzi sahihi wakati wa kupanga mipango ya maendeleo katika jamii na kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya kilimo nchini.

Madembwe, alisema matumizi ya Kanza hiyo yanawarahisishia wadau hao
kupata taarifa za Kilimo na chakula kwa urahisi zilizokusanywa kutoka katika taasisi mbalimbali na wizara zinazohusika na sekta ya Kilimo hapa nchini.

Alisema matumizi mfumo huo yataondoa hali iliyokuwepo hapo awali ya ugumu wa upatikanaji wa takwimu kutokana na mtawanyiko watakwimu hizo na kuwataka wadau wote wa sekta hiyo walio katika ngazi ya maamuzi kuielewa na kutumia.

Alifafanua kuwa takwimu zinazowekwa katika Kanza hiyo zinahusu Kilimo, Uvuvi, Biashara, Uzalishaji na upatikanaji wa chakula katika mikoa mbalimbali ya Tanzania na kuongeza kuwa kazi ya uwekaji na uhuishaji wa takwimu hizo inafanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa ushirikiano wa wataalam kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera na Mipango, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Oswald Luboha, alisema mfumo huo wakiteknolojia ulianzishwa mwaka 2005 na kuzinduliwa rasmi mwaka 2012 kwa lengo la kuweka pamoja takwimu za kilimo ili wadau wa sekta ya Kilimo waweze kuzipata kwa urahisi popote walipo nchini.

Aidha, lifafanua kwa kusema kuwa ushiriki wao katika semina hiyo kulitokana na ukweli kwamba wizara hiyo, ndio watoaji wakubwa wa takwimu za kilimo, kilimo kiko chini ya wizara hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages