Mkurugenzi wa Kampuni ya Insights Productions Limited, Marion Elias (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya maonesho makubwa ya keki yanayotarajia kufanyika jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mratibu wa Matangazo na Uhusiano wa Umma wa kampuni ya SSB, Mohammed Ramadhan wazamini wa maonesho hayo na kulia ni Meneja Bidhaa za Azam, Abubakar Suleiman.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
KAMPUNI ya Insights Productions Limited kwa udhamini wa Kampuni ya Azam Tanzania imeandaa maonesho makubwa ya keki yanayotarajia kufanyika jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa uandaaji na utayarishaji wa keki. Maonesho hayo yatajulikana kama 'Azam World of Cakes Exhibition'.
Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kampuni ya Insights Productions Limited, Marion Elias alisema maonesho hayo yanatarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali binafsi, makampuni na taasisi waandaaji wa keki nchini Tanzania ikiwa ni sehemu ya kubadilishana uzoefu na kujifunza ubunifu zaidi wa shughuli hizo.
Bi. Elias alisema dhumuni la maonesho hayo ambayo yanatarajiwa kufanyika Desemba 6, 2014 jijini Dar es Salaam ni pamoja na kusherehekea taaluma ya uokaji keki kwa kuonesha ubunifu na utaalam wa utengenezaji na upambaji wa keki bidhaa inayopendwa na watu wengi na kutumika katika shughuli anuai za kijamii.
Alisema washiriki wa tamasha hilo mbali na kushindanisha na kuonesha bidhaa zao za keki pia wanatarajia kupata semina ya mafunzo juu ya utengenezaji bora wa keki ikiwa na lengo la kuboresha zaidi taaluma zao.
Alisema washiriki hao pia watafanya maonesho ya utayarishaji wa vyombo vya kutengenezea keki, utayarishaji wa unga wa ngano kwa ajili ya kupikia keki, kutambua unga bora wa keki, uchanganyaji wa unga na viungo vingine kwa ajili ya uboreshaji wa radha ya keki.
Alisema maonesho mengine yatakayofanywa na wadau hao wa keki ni pamoja na uhifadhi bora wa keki kwa muda mrefu bila kuharibika na washiriki kuonesha maumbo mbalimbali ya keki yenye mvuto kwa watumiaji wa keki na jamii nzima.
Alisema maonesho hayo yanayodhaminiwa na Azam watengenezaji wa unga bora kwa ajili ya kutengenezea bidhaa hiyo, yatawashindanisha wadau wa uandaaji keki na pia washindi watakao tajwa na majaji wa maonesho watajipatia fedha
taslimu na bidhaa mbalimbali.
"...Onesho hili litahusisha jamii yote inayojishughulisha na utengenezaji wa keki, upambaji wa keki, wauzaji wa keki na wanaojishughulisha na bidhaa mbalimbali zinazotumika kutengeneza keki kama vile unga wa ngano wa Azam,"
alisema Mkurugenzi wa Insights Productions Limited, Bi. Elias.
Akifafanua zaidi Mkurugenzi huyo alisema onesho hilo litajumuisha bekari na hoteli mbalimbali, Vyuo vya taaluma ya hotelia toka Tanzania na majirani (Afrika Mashariki) pamoja na watengenezaji keki binafsi. Wananchi watakaotembelea maonesho hayo ambayo hayata kuwa na kiingilio watapata fursa ya kujionea aina na mitindo mbalimbali ya utengenezaji wa keki pamoja na kuonja bidhaa hiyo kwenye maonesho ambayo yatafanyika Serena Hoteli jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia maonesho hayo Mratibu wa Matangazo na Uhusiano wa Umma wa kampuni ya SSB, Mohammed Ramadhan alisema Azam ikiwa ni kampuni inayotengeneza unga bora wa kutengenezea keki imeamua kudhamini ikiwa ni ishara ya kutambua taaluma hiyo ya uokaji keki nje na ndani ya Tanzania.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment