Mkurugenzi
Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Adam Mayingu, akizunfumza wakati wa semina
ya siku moja iliyoandaliwa na Mfuko huo kwa maafisa rasilimali watu kutoka
wakala za serikali iliyofanyika mjini Bagamoyo mkoa wa Pwani.
Mmoja
wa washiriki wa semina hiyo, akizungumza.
Katibu Mkuu Ikulu, Peter Ilomo, (Kulia), akiongozana na
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Gabriel Silayo, wakati wa
mapumziko ya chai baada ya kufungua semina ya siku moja iliyoandaliwa na Mfuko
huo kwa maafisa rtasilimali watu huko Bagamoyo mkoani Pwani.
Baadhi ya maofisa wa PSPF wakiwa katika picha ya pamoja.
Katibu
Mkuu Ikulu, akitoa hotuba ya ufunguzi wa Semina ya siku moja iliyoandaliwa na
Mfuko wa Pensheni wa PSPF, kwa maafisa rasilimali watu huko Bagamoyo mkoani
Pwani, Alhamisi Oktoba 16, 2014. Warsha hiyo ililenga kuwapatia elimu waajiri
kuhusu huduma mbalimbali zitolewazo na Mfuko huo kwa wanachama wake.
Washiriki
wa semina wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa na wataalam wa
Mfuko wa Pensheni wa PSPF, kuhusu huduma mbalimbali zitolewazo na Mfuko huo.
Washiriki
wa semina wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa na wataalam wa
Mfuko wa Pensheni wa PSPF, kuhusu huduma mbalimbali zitolewazo na Mfuko huo kwa
wanachama wake, Semina hiyo ilifanyika mjini Bagamoyo.
Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Ikulu Bw. Peter Ilomo amewashauri watanzania
kujiunga na Mpango wa Uchangiaji wa Hiari wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF ili
kujiongezea kipato na hatimaye kuishi ya staha.
Bw. Ilomo alisema hayo Mjini Bagamoyo wakati wa semina iliyoandaliwa na
Mfuko wa Pensheni wa PSPF kwa ajili ya Maafisa Rasilimali Watu kutoka wakala
mbalimbali za Serikali
Kutokana na mabadiliko kwenye sekta ya
hifadhi ya jamii, PSPF ilianzisha Mpango wa Uchangiaji wa Hiari maarufu kama
PSS ili kuweza kuwahudumia Watanzania wote ambao wanahitaji huduma za hifadhi
ya jamii ambao walikosa fursa hiyo huko nyuma.
“Mpango huu ni mkombozi kwani unazidi
kukuongezea kipato na kukufanya uishi maisha yenye staha sasa na hata wakati wa
ustaafu wako. Mpango huu pia unatoa ruksa kwa mtu asiye raia wa Tanzania lakini
anafanyakazi hapa nchini kihalali kuwa mwanachama” alisema Bw. Ilomo.
Akizungumzia juu ya ujio ya kanuni moja ya
ukokotoaji wa mafao, Bw. Ilomo alisema, “Kuwepo kwa kanuni moja ya ukokotoaji
mafao ni changamoto kwa Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii, kwa kuwa kigezo kikubwa cha kuvutia wanachama kitakuwa ni ubora
katika huduma na mafao ya muda mfupi. Hivyo, nawaagiza watendaji wote wa PSPF kuhakikisha
mnatumia vyema fursa hii kutoa elimu sahihi kwa watendaji hawa muhimu katika
utumishi wa umma hapa nchini”.
Kutokana na Wizara ya Kazi na Ajira kutangaza
kuwa Mifuko yote ya Hifadhi ya itakuwa ikitoa mafao yanayolingana, alisema wanachama wa PSPF waliokuwepo hadi tarehe
30/6/2014 watalipwa kwa utaratibu wa zamani na wote walioajiriwa kuanzia Julai
1, 2014 watalipwa mafao yao kwa mujibu wa kanuni mpya.
Katibu Mkuu huyo kutoka ofisi ya Rais
aliipongeza PSPF kwa kuandaa semina hiyo na kuongeza, “ Semina hizi ni muhimu kwani zinatoa fursa ya kuonana na wadau na
kutoa ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali kwa manufaa ya Mfuko na wanachama
wake”.
Awali akizungumza katika semina hiyo
Mkurugenzi Mkuu wa PSPF Bw. Adam Mayingu aliwahakikishia washiriki wote wa
semina hiyo kwamba PSPF itahakikisha inafikia dira yeke ambayo ni kuwa mtoa
huduma bora wa hifadhi ya jamii nchini, na kufanyakazi kwa mujibu wa dhima ya
Mfuko ambayo ni kutoa huduma zenye ushindani katika sekta ya Hifadhi ya Jamii
kwa wateja wake kwa kutumia watumishi wenye ari ya kazi na teknolojia inayofaa.
Katika kuhakikisha inafikia dira yake na
kuishi dhima yake, Bw. Mayingu aliahidi
kwamba PSPF itaendelea kutekeleza majukumu yetu ya utendaji wa kila siku
ikiongozwa na uwajibikaji, wajibu, muitikio, nidhamu, juhudi, uwazi na
unyenyekevu kwa wote.
No comments:
Post a Comment