
Maalim Seif akihutubia katika mkutano wa hadhara huko Mkokotoni. (Picha na Salmin Said,
OMKR)
2.
Katibu Mkuu wa CUF, Mhe. Maalim Seif Sgarif Hamad (katikati), Naibu
Katibu Mkuu CUF Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui na Mwenyekiti wa CUF
Wilaya ya Kaskazini 'A' Bakari Makame akipandisha bendera za CUF wakati
wa uzinduzi wa tawi jipya la Tazari.Katibu Mkuu wa CUF, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akiweka tofali kusaidia ujenzi wa hodhi la maji safi na salama linalojengwa na wananchi wa kijiji cha Kivunge, Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja.
Wanachama na wafuasi wa CUF wakimsikiliza Katibu Mkuu wao alipokuwa
akihutubia kwenye mkutano wa hadhara Mkokotoni.
Khamis Haji, OMKR
Katibu Mkuu
wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Zanzibar imepata
athari kubwa kwa kukosa fedha za wafadhili kutokana na wizi wa zaidi ya shilingi
bilioni 320 katika akaunti ya Tegeta Escrow uliohusisha baadhi ya viongozi serikalini.
Maalim Seif
ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alisema hayo alipokuwa
akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CUF katika viwanja vya Mkokotoni,
jimbo la Tumbatu mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema miongoni
mwa miradi inayotajwa kuathirika kutokana na uamuzi wa wafadhili kusitisha
misaada kufuatia kashfa hiyo ni mradi wa Millenium Challenge Corporation unaopata
ufadhili kutoka Marekani, ambao unasaidia huduma za umeme pamoja na ujenzi wa
barabara kwa uapnde wa Zanzibar.
Alieleza
kuwa Zanzibar pia inanufaika na misaada ya kibajeti na ile inayotolewa na Mfuko
wa Dunia (Global Fund) maeneo ambayo pia yameathirika kutokana na uamuzi wa
wafadhili hao ambao hawakuridhishwa na wizi wa fedha katika sakata hilo la
Escrow.
“Zanzibar
tumeathirika sana kuna miradi mingi imesitishwa kwa kashfa hiyo ya Escrow,
lakini pia hakuna Mzanzibari hata mmoja aliyetajwa kunufaika na fedha hizo,
tungekuwa na Mamlaka ya kujiamulia mambo yetu yasingetokea hayo”, alisema
Maalim Seif.
Katika hatua
nyengine, Maalim Seif amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa ya
kuwatisha wananchi wanaoamua kukihama chama cha Mapinduzi na kujiunga na
upinzani.
Akizindua
matawi mapya ya CUF, katika vijiji vya Kivunge, Tazari na Nungwi katika Wilaya
ya Kaskazini ‘A’ Unguja amesema amesikitishwa kusikia kuna baadhi ya viongozi wanatoa
vitisho hivyo ambavyo ni kinyume na Katiba ya nchi.
Maalim Seif
alisema hayo baada ya wanachama wa CUF katika kijiji cha Tazari kusema kwamba wamechukua
uamuzi mgumu wa kujiunga na CUF na kufungua tawi katika eneo hilo, kwa sababu
kwa miaka mingi wamekuwa wakitishwa na kunyimwa uhuru wa kujiunga na chama
zaidi ya CCM.
“Kitendo cha
kufungua tawi hapa Tazari ni cha kihistoria, kwa miaka yote haikuwezekana na
tumekuwa tukitishwa na tukiaminishwa kuwa chama pekee cha kujiunga ni CCM”,
alisema Katibu wa tawi hilo, Simai Uyobi katika risala ya wanachama wa tawi
hilo.
Maalim Seif
aliwataka wananchi wasiogope kujiunga na CUF na kukihama chama cha CCM kwa
sababu kujiunga na chama wanachotaka ni haki yao.
“Hakuna
mwenye haki ya kukuzuieni kujiunga na chama mnachokipenda, nasema yoyote
atakayekuja kukupeni vitisho niambieni tu nitapambana naye”, alisema Maalim
Seif.
Katika kijiji
cha Tazani ambacho kwa miaka mingi ni miongoni mwa ngome za chama cha CCM
katika mkoa wa Kaskazini Unguja, wanachama wapya 40 walipewa kadi za CUF baada
ya kuzirejesha za CCM.
Akihutubia mara
baada ya kuzindua tawi la CUF Nungwi, Katibu Mkuu huyo alisema wananchi wa
Zanzibar wanapaswa kulinda hadhi na heshima ya Zanzibar na waikatae Katiba
inayopendekezwa pale watakapoletewa kwa ajili ya kuipigia kura ya maoni.
“Najua
hakuna Mzanzibari asiyeumwa na Zanzibar, haya mambo ya kushabikia sera za vyama
na kuididimiza Zanzibar hayana maana, Wazanzibari tuungane tuitetee Zanzibar
yetu”, alisema Maalim Seif.
Alisema
vyama vya siasa huanzishwa na kufa, lakini nchi ndiyo inayobaki, hivyo ni
wajibu wa wananchi bila kujali itikadi zao kulinda heshima ya nchi badala ya
kukumbatia vyama.
“Vyama vya
siasa ni mambo ya kupita hamkumbuki zamani kulikuwa na Afro Shirazi Party,
Hizbu, TANU na Umma Party vyama hivyo leo viko wapi, lakini Zanzibar ipo na
wala haitakufa”, alisema.
Aidha,
aliwataka wanachama wa CUF kujenga matawi na ofisi za kisiasa kwa kile
alichoeleza kuwa chama hicho ni kikubwa na kinapaswa kujenga taswira njema
kutokana na mipango yake ya maandalizi ya kushika dola katika uchaguzi mkuu ujao.
Katika
risala ya wanachama wa CUF jimbo la Tumbatu iliyosomwa kwenye mkutano wa
hadhara na Othman Hazir Othman walisema wamesikitishwa na kitendo cha Mbunge wa
jimbo la Tumbatu wakati wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba alipowasemea kuwa wananchi
wa jimbo hilo wanaunga mkono muundo wa Muungano wa Serikali mbili.
Othman
alisema wananchi walio wengi katika jimbo hilo wanaelewa kuwa muundo wa Muungano
wa Serikali mbili ndicho kitanzi cha Zanzibar, hivyo hawawezi kuuunga mkono na
wanataka Zanzibar yenye mamlaka kamili.
No comments:
Post a Comment