HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 21, 2014

UCHAGUZI WA MARUDIO WA SERIKALI ZA MITAA KATIKA KATA YA KWEMBE WAVUNJIKA

Askari Polisi wakiondoka na sanduku la kupigia kura baada ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Mtaa wa King’azi Kata ya Kwembe jijini Dar es Salaam kuvunjika  leo kutokana na vurugu zilizowahusisha mawakala wa CCM na Chadema na kusababisha masanduku manne ya kupigia kura kuvunjwa. (Picha na Francis Dande)
Askari Polisi wakiondoka na sanduku la kupigia kura baada ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Mtaa wa King’azi Kata ya Kwemba jijini Dar es Salaam kuvunjika  leo kutokana na vurugu zilizowahusisha mawakala wa CCM na Chadema na kusababisha masanduku manne ya kupigia kura kuvunjwa.
 Msimamizi wa Uchaguzi katika Kata ya Kwembe aliyetambulika kwa jina moja la Magwiza (kulia) akitoa maelezo kwa maofisa wa Polisi waliofika katika kituo hicho baada ya kutokea vurugu.
 Hali ilikuwa hivi nje ya chumba cha kupigia kura baada ya maofika wa polisi kufika.
 Kamanda E.M. Tille akizungumza na simu ili kupata muhafaka wa kituo hicho.
 Maofisa wa Polisi wakijadiliana jambo.
 Baada ya msimamizi wa uchaguzi kuahirisha uchaguzi huo maofisa wa polisi na wadau wengine wakitoka nje.
 Msimamizi wa uchaguzi, Magwiza (katikati) akitondoka baada ya kuahirisha uchaguzi huo mpaka baada ya miezi mitatu.
Wafuasi wa Chadema wakipaza sauti baada ya uchaguzi kuahirishwa.
 Wafuasi wa Chadema wakiwa katika mkusanyiko baada ya uchaguzi kuahirshwa tena kwa muda wa miezi mitatu.
 Wafuasi wa Chadema wakiwa katika mkusanyiko baada ya uchaguzi kuahirshwa tena kwa muda wa miezi mitatu.
Askari wakiondoka katika eneo la tukio.
 

Na Mwandishi Wetu



*Polisi Dar waondoka na maboksi ya kura baada ya kuvurugika

*Mabomu ya machozi yarindima

Na Mwandishi Wetu
UCHAGUZI wa marudio wa Serikali za Mitaa, uliofanyika sehemu mbalimbali nchini leo, umeibua vurugu kubwa pengine kuliko hata zile zilizotokea kwenye uchaguzi wa Desemba 14 mwaka huu.
Katika maeneo mengi nchini, uchaguzi huo wa marudio umevunjika na vurugu kubwa zimetokea kiasi cha kusababisha Polisi kuingilia kati na kurusha mabomu ya machozi.
Sababu za kuvunjika kwa uchaguzi wa jana zinafanana na zile za Desemba 14 za uzembe wa wasimamizi wa uchaguzi ambao ni wakurugenzi wa halmashauri ambapo wakurugenzi sita wa halmashauri walitimuliwa kazi, watano kusimamishwa, watatu kupata onyo kali na watatu onyo la kawaida kwa madai ya kusababisha kuvurugika kwa uchaguzi huo.
Katika uchaguzi uliofanyika katika Mtaa wa King’azi Kata ya Kwembe wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaaam, umeahirishwa tena kwa mara ya pili baada ya kutokea vurugu.
Vurugu hizo zimesababisha wanachama watatu wa Chama Cha Maendeleo (Chadema), kukamatwa na polisi kwa madai kuwa ndio chanzo cha kuvurugika kwa uchaguzi huo.
Kauli ya kuahirisha uchaguzi huo, ilitolewa jijini jana na  Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi huo, aliyetambulika kwa jina moja la Magwiza.
Magwiza, alisema ameamua kuahirisha uchaguzi huo baada ya kubaini kutoweka kwa amani katika eneo hilo kutokana na mvutano uliotokea kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chadema.
Chadema walisema hakuna sababu ya kurudia uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa kwani alikwishapatikana Desemba 14 mwaka huu ambapo Donath Mtemekele (Chadema), aliibuka mshindi.
Viongozi wa Chadema, walisema kwa kuwa katika uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa Mtaa wiki iliyopita ulikwenda vizuri na mshindi kupatikana kihalali, lakini uchaguzi wa wajumbe ndio uliovunjika, hivyo hakuna sababu ya kurudia uchaguzi wa nafasi Mwenyekiti.
Katika uchaguzi wa wiki iliyopita, Mtemekele wa Chadema  alipata kura 312 na mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Eric Mandani  aliambulia kura 207 na mawakala wote waliridhika na matokeo hayo ya nafasi ya Mwenyekiti.
Wakati Chadema wakipinga uchaguzi wa nafasi  ya Mwenyekiti kurudiwa, CCM nao walipinga wakitaka uchaguzi wa nafasi hiyo pia urudiwe kama ule wa nafasi za wajumbe ambao wiki iliyopita haukufanyika kabisa.
Vurugu zilizuka baada ya kuanza kuhesabiwa kura za wagombea nafasi za ujumbe.
Aliyeanzisha vurugu hizo alikuwa Mandari wa CCM ambaye alimvamia mgombea wa Chadema wa nafasi ya ujumbe,  Stephen Mgombozi na kumrushia maneno kwamba alikuwa ana mtafuta sana na kuanza kumshambulia kwa kumpiga na kupiga teke sanduku la kura.
Baada ya hapo hali ya amani ilitoweka kwani vurugu zilikuwa kubwa kwa baadhi ya wafuasi na viongozi wa vyama hivyo hasimu kuchapa makonde hali iliyowalazimu Polisi kuingilia kati.
Akizungumzia vurugu hizo Magwiza, alisema mawakala wawili wa Chadema wanashikiliwa na Polisi kwa madai ya kuvunja masanduku manne ya kura na hivyo kusababisha vurugu zaidi kutoka kwa wafuasi na viongozi wa CCM.
Alisema tafrani hiyo iliwafanya Polisi kuwatawanya wapiga kura kwa mabomu ya machozi na risasi za moto hewani.
Aidha, baada ya vurugu hizo aliwasiliana na Msimamizi wa Uchaguzi, Mussa Natty, ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kuhusu hali hiyo.
“Hii amri ya kuahirisha chaguzi ni agizo la Mkurugenzi lakini hata hivyo tulishauriana na vyama vyote viwili na tumetiliana saini ya makubaliano ya kuahirisha uchaguzi huu hadi utapotangazwa tena,” alisema Magwiza.
Alisema uchaguzi huo utafanyika tena kama uchaguzi mdogo ambao utapangiwa siku ya kufanyika na Ofisi ya Tawala za Miokoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Hata hivyo, Msimamizi huyo, alisubiri kutoa tangazo hilo hadi alipofika Kamanda Polisi wa Operesheni Tile, ambaye alipewa taarifa na msimamizi huyo kisha Mkurugenzi wa Manispaa hiyo.
Katika eneo hilo kulikuwa na kikosi cha polisi huku wakiwa wamejihami na silaha za moto na mabomu ya machozi ambao walifika hapo wakiwa katika magari mawili.
Katika kituo cha uchaguzi cha Kigogo Fresh Pugu,  hadi majira ya saa saba mchana, wananchi walikuwa hawajaanza  kupiga  kura na hakuna sababu zilizotolewa.

1 comment:

  1. Hali ilikuwa tete kwelikweli. Tunaomba watakaosimamia uchaguzi huu kama utakuwepo watende haki! Sisi tumechoshwa na fujo tunataka maendeleo basi

    ReplyDelete

Pages