Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari, Katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibara asubuhi hii, kuhusu moja ya maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM, ya kuwataka wanaotaka kuwania urais kupitia CCM na wapambe wao kuacha kueneza taarifa za uongo kwenye vyombo vya habari na kwamba atakayebainika kufanya hivyo atachukulia hatua kali za kinidhamu.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akisisitiza jambo katika mkutano huo na waandishi uliofanyika katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Znzibar asubuhi hiii.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Mwaka huu 2015 ni mwaka wa
uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge, Rais wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano. Hii ni kwa mujibu wa katiba ya
nchi. Ratiba ya mchakato wa kuwapata wagombea wa CCM kwa nafasi hizo
haijatolewa bado.
Itakumbukwa Kamati Kuu iliyopita
ya tarehe 13/01/2015, iliyoketi Kisiwandui Zanzibar ilipitisha ratiba ya
shughuli za kawaida za Chama kwa mwaka 2015 na kupanga kushughulikia
ratiba ya mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM vikao vijavyo.
Pamoja na kutotolewa kwa ratiba
hiyo, bado zimekuwepo harakati nyingi za wanaotaka kuteuliwa na CCM
kugombea nafasi mbalimbali hasa ya urais wa Jamhuri ya Muungano.
Harakati hizo baadhi halali, nyingi haramu.
Pamoja na kutaadharishwa mara
nyingi juu ya madhara ya harakati hizo kwa umoja na mshikamano wa Chama
bado baadhi yao wamekuwa wakiendelea na harakati hizo.
Kwa muda sasa kumekuwepo na uzushi
mwingi juu ya baadhi ya wanaotaka kuwania nafasi hizo kujadiliwa na
hata kuchukuliwa hatua na vikao vya chama. Maneno haya kwa sehemu kubwa
yamekuwa yakisambazwa na wagombea wenyewe au wapambe wao.
Uzushi huu, hauna nia njema kwa
CCM, unalengo la kukigawa Chama na kuonyesha kama vile Chama hakina kazi
nyingine ila kujadili na kushughulika na watu hao. Kwa mara nyingine
CCM inapenda kuwataadharisha wagombea hao na wapambe wao kujiepusha na
kusambaza taarifa zisizokuwa za kweli. Kwa kuwa vitendo hivi vinakigawa
Chama chetu.
CCM haitasita kuchukua hatua kali
dhidi ya wote wanaosambaza taarifa hizi. Ni vyema wagombea wakawadhibiti
wapambe wao na wakajichunga wenyewe dhidi ya hujuma hizi kwa Chama
kwani zitawapotezea sifa ya kugombea.
Wengi wa wanaosambaza taarifa hizi
ni wagombea au wapambe wasiojiamini kutokana na matendo yao, ambayo
hata wao wana mashaka na uadilifu wao. Hatuoni sababu ya mgombea
anayefuata sheria, kanuni na taratibu za Chama kuhofia kuchukuliwa hatua
kila vikao vya Chama vinapofanyika.
Ukitenda kwa haki huna haja ya kuogopa vikao na kuzusha uongo na uzushi usio na ukweli. CCM inaamini matendo haya hayatajirudia.
Aidha Chama Cha Mapinduzi
kinawaomba wanachama na wananchi kuzipuuza taarifa zinazosambazwa kwa
kuvinukuu vyanzo visivyo rasmi, kama kuna hatua au taarifa kwa umma juu
ya hatua yoyote katika mchakato huu basi itatolewa na wasemaji halali wa
Chama na si kutoka vyanzo vya barabarani.
Itakumbukwa pia baada ya Kamati
Kuu iliyopita kukutana tulitangaza kufanyika kwa kikao cha Kamati Ndogo
ya Maadili kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kimaadili kwenye sakata
la Escrow kwa viongozi wa Chama walioko kwenye vikao vya Chama vya
maamuzi.
Jana kumekuwepo na harakati nyingi
za vyombo vya habari na watu binafsi kujaribu kupata taarifa ya nini
kimetokea kwenye kikao hicho cha Maadili.
Tunapenda kuwakumbusha kuwa kwa
mujibu wa taratibu taarifa za kilichotokea kwenye kikao cha Kamati Ndogo
ya Maadili huwa hazitolewi kwa umma mpaka baada ya kufikishwa kwenye
Kamati Kuu.
Hivyo basi tunawaomba kutulia na kusubiri taarifa rasmi baada ya kufikishwa kwenye Kamati Kuu kuliko kuhangaika sasa hivi, jambo linaloweza kusababisha kuokotwa kwa habari za barabarani ambazo nyingi si za kweli. Tulieni subirini taarifa rasmi.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Hivyo basi tunawaomba kutulia na kusubiri taarifa rasmi baada ya kufikishwa kwenye Kamati Kuu kuliko kuhangaika sasa hivi, jambo linaloweza kusababisha kuokotwa kwa habari za barabarani ambazo nyingi si za kweli. Tulieni subirini taarifa rasmi.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na;-
Nape Moses Nnauye
Katibu wa Itikadi na Uenezi.
20/01/2015
No comments:
Post a Comment