HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 08, 2015

SHIRIKA LA TAIFA LA HIFADHI YA JAMII (NSSF) LAANZA MCHAKATO WA KUWASAKA WENYE VIPAJI VYA MPIRA WA MIGUU


Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 26/01/2015 Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lilisaini mkataba maalum na timu ya Real Madrid ya Nchini  Hispania ya kuanzisha na kuendesha kituo cha michezo (NSSF- REAL MADRID Sports Academy) kwa lengo la kuibua, kuendeleza na kukuza vipaji kwa mpira wa miguu. Shirika la NSSF litajenga kituo hicho katika eneo la Mwasonga Kigamboni nje kidogo ya mji wa Dar es Salaam na wataalamu kutoka timu ya Real Madrid watatoa mafunzo kwa vijana wa umri wa miaka13 hadi 19 kwa madhumuni ya kukuza mpira wa miguu nchini, kupata wachezaji bora wanaouzika nje na ndani ya nchi pamoja na kulipatia mapato shirika na nchi kwa ujumla.

Akizungumza na Waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya Habari Nchini, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Dr. Ramadhani K. Dau alisema mradi huo ukiwa kama sehemu ya uwekezaji wa NSSF ulianza maramoja baada ya kusaini mkataba.  NSSF imeanza utaratibu wa kuwabaini vijana walengwa ambapo kwa kuanzia utafutaji wa vipaji vya mpira wa miguu utaanzia mkoa wa Dar es Salaam kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 14. 

Utafutaji wa vipaji utafanyika kiwilaya kwa Wilaya za mkoa wa dar es salaam na utakuwa unafanyika  katika viwanja vya Karume. Zoezi hilo litakuwa linafanyika kati ya saa 1 asubuhi hadi saa 9 alasiri  kwa tarehe zilizoainishwa.

Uandikishaji  wa washiriki utakuwa unafanyika siku za mwisho wa wiki ili kutoathiri wanafunzi watakaopenda kushiriki na utaanza rasmi tarehe 14 na 15,na tarehe 22 na 23  Februari 2015, na kufuatiwa na michezo ya majaribio tarehe 28 Februari,na Tarehe 1 Machi 2015 kwa wilaya  zote za mkoa wa Dar es salaam ambapo kituo kitakuwa viwanja vya Karume kuanzia saa moja asubuhi hadi saa 9 alasiri.

 Zoezi la Uandikishaji halitahusisha gharama zozote kwa washiriki, na uandikishaji wa washiriki utafanyika kwa kujaza fomu maalum na kupewa namba ya ushiriki na kila mshiriki atapata fursa ya kucheza katika awamu mbili za dakika 30. Kwa kuanzia washiriki watatakiwa kuja na vifaa vyao vya michezo. 
 
Zoezi la awali litafanywa na wataalam wa ndani ya nchi ambapo Vijana 500 kati ya wote watakaofanyiwa majaribio  wataingia katika awamu ya pili ya majaribio na  watadahiliwa na wataalamu kutoka Klabu ya Real Madrid na hatimaye kupatikana vijana 30 amabo ndio wataingia katika  shule maalum ya mafunzo kwa awamu ya kwanza. Wakati wa uandikishwaji washiriki watatakiwa kuja na wazazi/walezi wao wakiwa na vitambulisho vyao,na kijana husika awe na Cheti  halisi cha kuzaliwa  na kopi  yake pamoja na picha mbili za pasport  rangi ya blue.Muda wa uandikishaji na majaribio unaweza kuongezwa kulinagana na mahitaji.

Shirika la NSSF linatoa wito kwa vijana kujitokeza kwani ni fursa kwao ya kuweza kujiendeleza kimichezo na kujiajiri katika tasnia hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages