HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 02, 2015

TFF MBIONI KUPATA MDHAMINI FDL

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liko mbioni kupata mdhamini wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL). Tunatarajia mdhamini huyo atakuwa tayari kwa ajili ya msimu wa 2015/2016.

Ligi Daraja la Kwanza inashirikisha timu 24 zinazocheza katika makundi mawili ya timu 12 kila moja kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.

Timu zinazocheza FDL msimu huu ni African Lyon (Dar es Salaam), African Sports (Tanga), Ashanti United (Dar es Salaam), Burkina Faso (Morogoro), Friends Rangers (Dar es Salaam), Geita Gold (Geita), Green Warriors (Dar es Salaam), JKT Kanembwa (Kigoma), JKT Mlale (Ruvuma) na JKT Oljoro (Arusha).

Nyingine ni Kimondo (Mbeya), Kinondoni Municipal Council (Dar es Salaam), Kurugenzi (Iringa), Lipuli (Iringa), Majimaji (Ruvuma), Mwadui (Shinyanga), Panone FC (Kilimanjaro), Polisi Dar es Salaam, Polisi Dodoma, Polisi Mara, Polisi Tabora, Rhino Rangers (Tabora), Toto Africans (Mwanza), na Villa Squad (Dar es Salaam).

KIPA BORA WANAWAKE AZAWADIWA 500,000/-
Kipa bora wa michuano ya Kombe la Taifa la Wanawake, Belina Julius wa Temeke amezawadiwa sh. 500,000 na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara.

Dk Mukangara alitoa zawadi hiyo baada ya mechi ya fainali ya michuano iliyomalizika jana kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam. Dk Mukangara alikuwa mgeni rasmi kwenye fainali hiyo.

Temeke ndiyo walioibuka mabingwa wa michuano hiyo iliyofanyika kwa mara ya kwanza nchini baada ya kuilaza Pwani bao 1-0 katika fainali iliyoonyeshwa moja kwa moja (live) na televisheni ya Azam.

Ilala ilifanikiwa kutwaa baada ya kuichapa Kigoma mabao 3-0. Bingwa amepata sh. milioni tatu, makamu bingwa sh. milioni mbili wakati mshindi wa tatu ameondoka na sh. milioni moja katika michuano hiyo iliyodhaminiwa na kampuni ya Proin.

MECHI ZA MWISHO FDL SASA FEB 8 NA 10
Mechi za raundi mbili za mwisho za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa makundi yote mawili zimerudishwa nyuma kutokana na maombi ya klabu hizo kupungaza gharama za kuendelea kuziweka kambini timu zao.

Hivyo, Februari 8 mwaka huu kundi A litacheza mechi zake za raundi ya 21 wakati zile za raundi 22 ambayo ndiyo ya mwisho zitafanyika Februari 13 mwaka huu. Mechi za Februari 8 ni KMC vs African Lyon, Kurugenzi vs African Sports, Majimaji vs JKT Mlale, Kimondo vs Friends Rangers, Ashanti United vs Villa Squad, Polisi Dar vs Lipuli.

Februari 13 mwaka huu ni African Lyon vs Polisi Dar, Kurugenzi vs Lipuli, Kimondo vs Majimaji, JKT Mlale vs Ashanti United, Friends Rangers vs African Sports, na Villa Squad vs KMC.

Kwa upande wa kundi B wataanza mechi za raundi 22 Februari 10 mwaka huu ili kupisha mechi za viporo za Polisi Mara zinazomalizika Februari 5 mwaka huu. Hivyo, Februari 10 mwaka huu itakuwa ni Burkina Faso vs JKT Kanembwa, Mwadui vs Polisi Tabora, Polisi Dodoma vs Green Warriors, Rhino Rangers vs JKT Oljoro, Panone vs Polisi Mara, Geita Gold vs Toto Africans.

Raundi ya 22 itachezwa Februari 15 mwaka huu kwa mechi kati ya JKT Kanembwa vs Green Warriors, Mwadui vs Burkina Faso, Polisi Tabora vs JKT Oljoro, Polisi Dodoma vs Panone, Toto Africans vs Rhino Rangers, na Geita Gold vs Polisi Mara.   

RAMBIRAMBI MSIBA WA KATIBU IRFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa ya msiba wa Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IRFA), John Ambwene Mwakalobo uliotokea jana (Februari 1 mwaka huu) mkoani Iringa baada ya kuanguka akiwa nyumbani kwake.

Msiba huo ni pigo kwa wadau wa mpira wa mpira wa miguu kwani wakati wa uhai wake, Mwakalobo alitoa mchango mkubwa akiwa kiongozi. Mwaka 2011 alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa IRFA, kabla ya 2012 kushinda nafasi ya Katibu Msaidizi.

Alizaliwa Februari 4, 1954 na kupata elimu ya sekondari katika shule ya Azania, Dar es Salaam na baadaye mafunzo ya ualimu kwenye Chuo cha Ualimu Mpwapwa mkoani Dodoma. Alianzia kazi ya ualimu Newala mkoani Mtwara kabla ya kuhamia mkoani Iringa mwaka 1981. Alistaafu mwaka 2013.

TFF inatoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu, na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IRFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwa msiba huo.

Marehemu anatarajiwa kuzikwa kesho (Februari 3 mwaka huu) kwao Kyela mkoani Mbeya. Ameacha mke, watoto wanne na mjukuu mmoja. Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.
  
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments:

Post a Comment

Pages