Mheshimiwa Spika, nilijiunga na Bunge lako tukufu mwaka 2005 nikiwa
kijana mdogo mwenye malengo ya kupaza sauti ya vijana kwenye masuala
yanayohusu nchi yetu na pia kutetea maslahi ya wananchi wa Jimbo la
Kigoma Kaskazini na Mkoa wa Kigoma.
Katika kudumu kwangu kama mbunge nililelewa na kukuzwa na chama cha
siasa cha CHADEMA ambacho kupitia chama hiki niliingia Bungeni. Chama
hiki kilinilea na kunikuza tangu nikiwa na umri wa miaka 16 na kupitia
chama hiki nimejifunza mambo mengi sana. Nimeijua nchi yangu, nimejua
siasa na nimejulikana ndani na nje ya nchi. Nitakuwa mwizi wa fadhila
nisipotoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa CHADEMA na viongozi ambao
nimefanya nao kazi muda wote nikiwa mwanachama na kiongozi.
Mheshimiwa Spika, Chama kilinikuza kama mwanasiasa lakini watu wa
Kigoma Kaskazini ndio walionipa kiti hiki ninachokalia kama Mbunge. Juzi
nilipokuwa nyumbani nilipata fursa ya kuwashukuru rasmi wananchi kwa
imani waliyonipa kuwatumikia kwa vipindi viwili mfululizo. Wengi wenu
ndugu zangu wabunge mnafahamu, mihula miwili sio jambo la mchezo, sio
lelemama. Mola atawalipa wananchi wa Kigoma kwa imani kubwa
walioionyesha kwangu na kuniwezesha kulitumikia Taifa langu kwa namna
nilivyolitumikia.
Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii leo kuzungumzia suala la muda
mrefu sasa la kutoelewana kati yangu na chama changu na hivyo kuleta
msuguano kati ya wananchi walionichagua kuwawakilisha na chama
nilichopitia na kupeperusha bendera yake wakati wa uchaguzi mkuu. Licha
ya msimamo wangu wa siku zote kwamba wananchi pekee waliomchagua
mwakilishi wao ndio wawe na mamlaka ya kumwondoa kwenye uwakilishi
mchaguliwa huyo, mfumo wetu wa kikatiba na mfumo wetu wa kisiasa haupo
hivyo na umeamua vinginevyo.
Mheshimiwa Spika, kwamba chama cha siasa kinaweza kumvua uanachama
mwanachama wake na hivyo kupoteza kiti chake cha uwakilishi wa wananchi
wake ni moja ya makosa makubwa ya kikatiba ambayo tumeendelea
kuyakumbatia, nimekuwa nikipinga na nitaendelea kupinga udikteta wa
vyama dhidi ya utashi wa wananchi.
Mheshimiwa Spika, licha ya upinzani wangu mkali wa vifungu kandamizi
vya kikatiba, kama mzalendo ninaiheshimu Katiba yetu na mfumo wetu wa
sasa na ninaheshimu uamuzi wa mahakama dhidi ya kesi yangu na sitakata
rufaa. Hatua itakayofuata ni uamuzi wa chama changu na baadhi ya
viongozi wameshatangaza kwa umma kupitia vyombo vya habari kunivua
uanachama ingawa sijapewa taarifa rasmi.
Mheshimiwa Spika, ningeweza kukata rufaa kuhusu maamuzi ya mahakama
kwani kuna sababu lukuki ya kushinda rufaa hiyo. Lakini ninadhani
nimepigania haki zangu kwa muda mrefu sasa. Nimepigania kupanua wigo wa
demokrasia ndani ya chama changu kwa muda mrefu sasa. Lakini ugomvi huu
hauna manufaa kwa pande zote husika, kwa hakika unatuumiza wote.
Mimi ni
mwanademokrasia. Naamini katika siasa za ushindani ndani ya chama na
katika mfumo mzima wa siasa kitaifa. Lakini sitakuwa tayari kudhoofisha
harakati na kazi kubwa walizofanya wanamageuzi waliotutangulia kwa
kuendeleza ugomvi unaotuumiza. Hivyo niko tayari kukubali kukaa pembeni.
Ninaamini kuwa mapambano ya kuleta mabadiliko ya kweli na demokrasia
katika nchi yetu Tanzania ni makubwa kuliko mimi, kuliko kiongozi yoyote
wa Chadema na kuliko wanachama wa Chadema.
Mapambano haya ya mabadiliko
si kwa ajili ya kizazi hiki tu bali kwa vizazi vijavyo. Ndiyo maana
siku zote nimesema Nchi kwanza, vyama baadae. Kuona makundi yanajitokeza
ndani ya harakati hizi, na kuwa na uhasama mkubwa uliopindukia,
unawakatisha tamaa wananchi wanaotutumaini kuleta siasa iliyo tofauti na
siasa za sasa. Muda umefika wa kupiga mstari na kuanza upya. Hivyo
nimeamua kuwa nitatii maamuzi ya chama ya kunivua uanachama na
kung’atuka ubunge.
Mheshimiwa Spika, naomba niweke wazi kuwa nimefikia uamuzi huu kwa
utashi wangu mwenyewe na nimepewa Baraka zote na wananchi wangu na wazee
wa Jimbo la Kigoma Kaskazini. Najua Watanzania wengi ambao
nimewatumikia kwa moyo wangu wote katika kipindi cha miaka hii 10
wanaweza wasikubaliane na uamuzi huu. Hata hivyo Watanzania wajue kuwa
mfumo wetu wa siasa na katiba unatoa nguvu kwa vyama vya siasa kudhibiti
wabunge wake.
Naamua hivi kwa sababu wenzangu ndani ya chama ambao
nimehangaika nao usiku na mchana kujenga chama na kukifisha hapa kilipo
hawapo tayari kufanya kazi tena na mimi. Nimesoma na kusikia kauli
nyingi zinazoweka wazi kuwa hawanitaki ndani ya chama. Nimejitahidi kwa
njia zangu zote kuona kama tunaweza kuendelea kufanya kazi pamoja ya
kujenga mfumo madhubuti wa vyama vingi nchini lakini imekuwa ngumu kama
mwanachama mwenzao. Ninaheshimu uamuzi wao huo.
Mheshimiwa Spika, kwa miaka kumi hii si yote niliyafanya sahihi, yapo
ambayo niliyakosea kama mwanadamu katika kufanya kazi kwangu, kwa namna
yeyote ile naomba radhi Watanzania wote kwa yote ambayo sikuyafanya kwa
usahihi. Mimi ni binadamu, kiumbe dhaifu, sijakamilika. Ni Mola peke
yake amekamilika.
Mheshimiwa Spika, siwezi kuanza maisha yangu mapya bila ya
kulishukuru Bunge lako tukufu, Bunge la Tisa chini ya Mzee Samwel Sitta
na Bunge la Kumi chini yako Mama Anna Simamba Makinda. Bunge limekuwa ni
nyumbani kwangu kwa takribani muongo mmoja.
Nimekuzwa, nimejifunza,
nimepambana, nimefurahi na nimelia ndani ya Bunge hili. Kwa pamoja
tumepigania maslahi ya wananchi wetu na kupingana na kufanya mambo kwa
mazoea na hivyo kuleta mabadiliko kadhaa. Ni kipindi hiki ambapo wabunge
tumekuwa na sauti, Bunge la Tisa lilijenga ‘Bunge lenye Meno’ katika
kupambana na ufisadi. Bunge la Kumi limejenga ‘Bunge lenye nguvu’ katika
mfumo wa Bajeti ya nchi yetu. Kupitia Bunge hili tumeweka misingi ya
kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, wakati Bunge la Tisa litakumbukwa kwa hoja ya
Buzwagi iliyopelekea nchi yetu kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo
wa uendeshaji wa sekta ya madini (Sera mpya ya Madini na Sheria mpya ya
Madini ) na hivyo mapato ya sekta ya madini kuongezeka kutoka Tshs 32
bilioni kwa mwaka mpaka Tshs 450 bilioni kwa mwaka hivi sasa; Bunge la
Kumi litakumbukwa kwa hoja maalumu ya Tegeta Escrow iliyopelekea mfumo
wetu wa maadili ya Viongozi kupitia Baraza la Maadili kuanza kufanya
kazi kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa katika miaka iliyopita. Mimi
kuwa sehemu ya mabunge yaliyotekeleza hatua hizo za mabadiliko ni jambo
la kujivunia sana.
Mheshimiwa Spika, kwa familia yangu, wajumbe wa PAC, tumekuwa nguzo
kubwa ya kujenga uwajibikaji wa Serikali kwa Bunge na wananchi. Napenda
kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa kuniunga mkono na kwa kunipa
ushirikiano kama Mwenyekiti wao. Changamoto na malezi mliyonipa kwa
miaka yote hii yamejenga Mtanzania mmoja mwenye dhati ya kuitumikia nchi
yake, muda wowote, wakati wowote na kwa namna yeyote ile bila woga wala
upendeleo. Nawashukuru kwa kujitoa kwenu kwa nchi yetu na dhamira isiyo
na mawaa ya kujenga Taifa imara zaidi.
Nitaendelea kuwatumikia wananchi wa Kigoma Kaskazini na Taifa langu
hata kama nimelazimika kuachia nafasi yangu ya ubunge kwa kipindi hiki
kilichosalia kwa kusimamia ukweli, kutetea demokrasia ya kweli na
kupigania maendeleo ya kweli kwa mwananchi wa kawaida bila ubaguzi
wowote.
Mheshimiwa Spika, Kwa CHADEMA, licha ya tofauti zetu ambazo zimekua
kiwango cha kutosameheka, najivunia kwa fursa mliyonipa kuwa sehemu ya
Baraza hili la Taifa ambalo leo ninalihutubia kwa mara ya mwisho kama
mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Fursa iliyonifanya niweze kuitumikia nchi
yangu na mkoa wangu wa Kigoma. Inawezekana tusiweze kuelewana katika
masuala ya uongozi, misingi na itikadi, lakini ninaamini tunapaswa
kuelewana na kukubaliana katika kubwa ya kuijenga nchi yetu kuwa Taifa
linalojitegemea na lisilo na aina yeyote ya ubaguzi. Taifa lenye uchumi
shirikishi wenye kuzalisha ajira na kuondoa umasikini, ujinga na
maradhi, Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Na ni matumaini yangu
kuwa tutakuwa bega kwa bega katika harakati hizi katika siku zijazo.
Yaliyopita si ndwele tugange yajayo, nafasi hii ya kihistoria tuliyopewa
haihitaji siasa za ubinafsi na unafsi! Uzalendo wetu utapimwa kwa uwezo
wetu wa kuweka tofauti zetu binafsi pembeni kwa lengo lililo kubwa
zaidi yetu.
Mheshimiwa Spika, Mwisho kwa wananchi wa Jimbo langu, wana Kigoma na
raia wote wa Tanzania ambao kwa ridhaa yao nimekaa katika viti hivi kwa
miaka takribani kumi, nawahakikishia kuwa dhamira yangu kuwatumikia, nia
yangu na sababu za kutoa utumishi wangu kwenu vimekuwa na nguvu zaidi
kuliko wakati mwingine wowote ule. Huu ni mwanzo mpya. Ngugi aliandika
‘a grain of wheat’ kwa maana ya kwamba ‘Ili Mbegu iweze kumea lazima ife
kwanza’.
Asanteni sana.
Asanteni sana.
No comments:
Post a Comment