HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 30, 2015

CRDB YAPATA FAIDA YA BIL. 95.6 BAADA YA KODI 2014

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dk. Charles Kimei akizungumza katika kongamano la wawekezaji wa benki hiyo lililofanyika jijini Dar es Salaam. (Picha na Francis Dande)
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dk. Charles Kimei akizungumza katika kongamano la wawekezaji wa benki hiyo lililofanyika jijini Dar es Salaam. 
Baadhi ya wawekezaji wa benki ya CRDB wakiwa katika kongamano hilo.
Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa akizungumza katika kongamano la Wawekezaji wa Benki ya CRDB.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Mh. Martin Mmari (kushoto) akisalimia na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo anayeshughulika na Uendeshaji na Huduma kwa Wateja, Saugata Bandyopadhyay.
Baadhi ya washiriki wa kongamano la wawekezaji wa benki ya CRDB wakiwa katika kongamano hilo leo.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Huduma Shirikishi wa Benki ya CRDB, Esther Kitoka akibadilishana mawazo na Prof. Mohamed Warsame (katikati).

NA FRANCIS DANDE


BENKI ya CRDB imetangaza kupata faida  ya shilingi za Tanzania bilioni 95.6 kwa mwaka wa fedha wa 2014, ikiwa ni ongezeko la asilimia 13.4, kutoka faida ya shilingi bilioni 84 iliyopatikana kwa mwaka wa fedha wa 2013.

Akizungumza katika kongamano la wawekezaji wa benki hiyo lililofanyika katika Hoteli ya Hyatt jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki  hiyo, Dk. Charles Kimei, amesema kuwa amana za wateja  wa benki hiyo zimeongezeka kwa asilimia 12.1, kutoka shilingi bilioni 3,024 mwaka 2013 na kufikia shilingi trilioni 3.309 mwaka 2014.

Aidha,  Dk. Kimei alisema pia kuwa  mikopo kwa wateja iliongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 2.545 kutoka shilingi trilioni 1.993 za mwaka 2013.

Dk. Kimei aliongeza kusema kuwa pamoja na mafanikio  hayo, benki pia ilijipatia matokeo mengi mazuri kwa mwaka 2014, ikiwa ni pamoja na mapato yatokanayo na riba, yaliyoongezeka na kufikia shilingi bilioni 371.7 ikilinganishwa na shilingi  bilioni 304.8 mwaka 2013.

Aliongeza kuwa mapato yasiyotokana na riba yaliongezeka na kufikia shilingi bilioni 121.5 kutoka shilingi bilioni 92.8 mwaka 2013.

Akizungumzia ujenzi wa matawi, Dk. Kimei alisema matawi mapya 20 ya kutolea huduma  ili kusogeza huduma karibu za wateja  yalijengwa.

Vilevile alisema mashine mpya za kutolea fedha (ATM) ziliongezwa, usajili wa mawakala wapya 575  wa Fahari Huduma hivyo  kufikisha  jumla ya  mawakala 1,067 wa Fahari Huduma  nchini kote. 
Pia uboreshaji wa mitambo ya kutolea  huduma  ya Core Banking System na mfumo wa mikopo ilikuongeza ufanisi na kupunguza  gharama za uendeshaji ulifanyika.

 Dk. Kimei alisema benki hiyo pia imeendelea kuwa raia mwema  kwa kulipa kodi ya mapato ya shilingi bilioni 36.6 kwa mwaka 2014.

 Akizungumzia kuhusu gawio kwa wana hisa, Dk. Kimei alisema  kuwa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo imependekeza  kwa Mkutano Mkuu wa Wanahisa  gawio la shilingi 15 kwa kila hisa  kutoka gawio la shilingi 14 kwa kila hisa lililotolewa mwaka  2013.

 “ Bodi imependekeza  kutengwa  kaw jumla ya shilingi bilioni 32.7 ambayo ni asilimia  34  ya faida baada ya kodi kwa ajili ya gawio kwa wanahisa wetu. Hili  niongezeko la asilimia  7 zaidi ukilinganisha na shilingi bilioni 30.5  zilizotengwa  kwa dhumuni hilo  mwaka  2013, alisema Dk. Kimei.

“Mkutano  Mkuu wa Mwaka wa Wanahisa  hisa wetu unaotarajiwa kufanyika  Mei 9,  2015 jijini Arusha ndio utakaopitisha  rasmi azimio  la kukubaliana na pendekezo  hilo la gawio la hisa,” alisema.

Akizungumzia kuhusu  mipango ya baadaye, Dk. Kimei alisema kuwa  kutegemeana na  maafikiano ya Mkutano Mkuu wa Wanahisa, Bodi ya Wakurugenzi imependekeza  na kuazimia  kuongeza mtaji kwa kuingiza katika  Soko la Mitaji la Dar es Salaam zaidi ya hisa 435,306,435 ili ziuzwe kwa wanahisa wa sasa na kujiongezea  mtaji utakaotumika katika mipango mbalimbali ikiwamo kuendeleza  sera  ya upanuaji wa mtandao wa benki  ili kuwafikia wateja wengi zaidi.

Vilevile ukuaji wa sekata mbalimbali ikiwemo wafanyabiashara wadogo wadogo na  wakubwa. Pia kuwekeza zaidi katika Teknohama ili kuongeza ufanisi na kupunguza  gharama za uendeshaji na kuwapunguzia gharama wateja wa benki hiyo na kuongeza wigo wa kupanuka kimataifa.

No comments:

Post a Comment

Pages